Jinsi mkakati wa vita wa Iran ulivyowashangaza Marekani na Israel

Chanzo cha picha, Reuters

    • Author, Prabhat Pandey Role
    • Nafasi, Mwandishi BBC Hindi
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Wakati Marekani na Israel zilipoanzisha mashambulizi ya pamoja dhidi ya Iran tarehe 28 Februari, swali kubwa lilikuwa: vita hivi vingedumu kwa muda gani?

Hata hivyo, hali ilionekana kuendelea kwa siku, wiki, na sasa miezi, bila kuwa na muda maalum wa kumalizika kwa vita hivyo.

Katika hotuba yake ya hivi punde kwa wananchi wa Marekani, Rais Trump, kinyume na matarajio, hakuweza kuwasilisha mpango ulio wazi, lakini alisema kwamba "Marekani inakaribia kufikia lengo lake la kimkakati nchini Iran" na kwamba "mashambulio makali dhidi ya Iran yatatekelezwa katika wiki mbili hadi tatu zijazo."

Pia alitishia "kuirudisha Iran kwenye Enzi ya kizamani".

Soko la mafuta na hisa, ambalo lilikuwa na matumaini kuhusu hotuba yake kwa umma, lilijibu mara moja, na sio tu kwamba bei ya mafuta ilipanda kwa kasi duniani kote, lakini masoko ya Asia, ikiwa ni pamoja na yale ya Marekani, pia yalipungua.

Balozi wa zamani wa Marekani katika NATO, Ivo Dalder, akijibu hotuba hiyo, alisema kuwa kauli ya Trump imezua "mashaka kuhusu malengo ya vita" na kuacha maswali kadhaa muhimu bila majibu, ikiwa ni pamoja na kwa nini Marekani bado inaendelea na operesheni za kijeshi nchini Iran ilhali, kama Trump alivyosema, uwezo wa nyuklia, jeshi la majini na makombora ya Iran umeharibiwa.

Jambo moja liko wazi kutoka kwa kauli ya Rais Trump: vita vitaendelea.

Licha ya hasara kubwa katika hatua za awali, Iran bado inapigana kwa nguvu na inaendelea na vita.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mgogoro kati ya Marekani na washirika wake wa NATO katika vita hivi sasa unaonekana wazi, na Trump si tu anatoa kauli za juu juu kwa washirika wa NATO bali pia ametishia kujiondoa.

Licha ya vita kuendelea kwa zaidi ya mwezi mmoja, mwitikio wa wananchi wa Iran haukuwa kama Trump na Netanyahu walivyotarajia, licha ya viongozi hao kuwataka wananchi wa Iran waasi na kuipindua serikali.

Mashambulizi ya Iran dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani katika nchi za Ghuba hayakusababisha tu uharibifu mkubwa bali pia yaliathiri vibaya taswira ya nchi hizo kama maeneo salama.

Kwa mujibu wa wataalamu, muda mrefu wa vita hii umesababisha kupungua kwa imani ya nchi za Ghuba na Ulaya kwa Marekani katika suala la dhamana za usalama.

Kufungwa kwa Mlango wa Hormuz na Iran kumesababisha mgogoro mkubwa wa mafuta duniani. Nchi nyingi sasa zinaishinikiza Marekani na Israel kusitisha mara moja mzozo huo, na baadhi ya nchi zimekataa kutumia mlango huo kama kituo cha operesheni za kijeshi.

Wakati huo huo, Marekani iliwashutumu washirika wake kama Uingereza, Ufaransa, Italia, Hispania na Kanada kwa kutosaidia katika vita dhidi ya Iran.

Je, Marekani na Israel zilikabiliwa na shinikizo?.

Chanzo cha picha, Reuters

Ili kuelewa hili, tunapaswa kurejea siku za mwanzo za vita hii.

Shambulio la anga katika shule ya msingi ya wasichana katika mji wa Minab nchini Iran liliua watu kadhaa, wakiwemo wasichana wengi.

Ni kwa mara ya kwanza nchi nyingi za Ulaya, zikiwemo Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, Italia na China, zililaani shambulio hilo, na sauti za kupinga vita zikaanza kuongezeka.

Nchi nyingine kadhaa pia zililaani vikali shambulio hilo, zikiilaumu Marekani na Israel. Ikumbukwe kuwa hadi sasa hakuna kati ya Marekani wala Israel iliyokiri kuhusika na shambulio hilo.

Kwa jumla, vita hivi vilidumu zaidi ya wiki nne bila kumalizika, Mlango wa Hormuz ukafungwa, na dunia ikakumbwa na mgogoro wa mafuta. Hata baada ya kuuawa kwa kiongozi mkuu wa Iran, bado iliendelea kupigana na iliwasilisha masharti yake ya kumaliza vita.

Kadiri vita vinavyoendelea, Marekani na Israel zinakabiliwa na ukosoaji wa kimataifa.

Maandamano makubwa dhidi ya vita hiyo yamefanyika hata ndani ya Marekani yenyewe.

Hivyo basi, katika hali hii, je, Iran imefanikiwa kwa kiasi fulani kuunda mazingira yanayochochea uhasama dhidi ya Marekani na Israel kupitia mikakati yake ya kijeshi na kidiplomasia?

Chanzo cha picha, Reuters

Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kupitia akaunti yake ya Truth Social tarehe 23 Machi kwamba kulikuwa na mazungumzo mazuri sana kati ya Marekani na Iran kuhusu kumaliza vita, lakini wakati huo huo aliendelea kutoa vitisho vikali vya mashambulizi.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya kimkakati Brahma Chellani, "Trump alianza vita hii kwa lengo la kuipindua serikali ya Iran, lakini baada ya kushindwa kufikia lengo hilo la msingi, sasa anafanya mazungumzo na utawala ule ule aliokuwa anasema atauondoa. Mazungumzo ya Iran kimsingi ni ya kulazimishwa baada ya kutambua ukweli halisi."

Hamid Reza Azizi, mtafiti katika Taasisi ya Ujerumani ya Masuala ya Usalama na Kimataifa huko Berlin, aliandika uchambuzi wa mzozo wa hivi karibuni nchini Iran wenye kichwa "Jinsi Iran Ilivyobadili Mkakati Wake wa Vita."

Akizungumza katika taasisi ya Carnegie, alisema:

"Iran imeongeza gharama ya vita kwa Marekani na Israel mara nyingi kwa kulenga miundombinu muhimu kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani."

"Iran imeonyesha kwa makusudi vita hivi kama mzozo wa kikanda. Haiioni kama mzozo wa pande mbili tu."

"Hii ina maana kwamba Marekani na Israel zinaweza kushambuliwa kutoka maeneo mbalimbali kama Lebanon, Iraq na Ghuba ya Uajemi, na kulazimika kutumia bajeti yao ya kijeshi katika maeneo mengi. Aidha, Iran imeunda hali ya kutotabirika, hawajui shambulio linalofuata litatoka wapi."

Kwa mujibu wake, mkakati wa Iran haujajikita katika kushinda vita haraka, bali katika kuwachosha wapinzani wake.

"Inaonekana Iran haitaki kumaliza vita haraka, bali inaendelea kuweka shinikizo la kijeshi, kisiasa na kiuchumi kwa muda mrefu, ili kuifanya vita kuwa ghali si tu kwa wapinzani wake bali pia kwa washirika wao."

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid