Je, tunaelekea katika vita vya tatu vya dunia?

Chanzo cha picha, Getty Images
Zaidi ya mwezi mmoja tangu Marekani na Israel kuanza vita dhidi ya Iran, wasiwasi umeanza kujitokeza iwapo mzozo huu wa Mashariki ya Kati unaweza kuongezeka na kuwa vita vikubwa zaidi.
Vita hivi havijaathiri Iran pekee, bali pia nchi kadhaa, ikiwemo Falme za Kiarabu, Iraq, Bahrain, Kuwait, Saudi Arabia, Oman, Azerbaijan, Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel, Cyprus, Syria, Qatar na Lebanon.
Swali ni je mzozo huu wa sasa unaweza kutanuka kutoka kiwango cha kikanda na kuwa vita kamili vya dunia?

Chanzo cha picha, Getty Images
Vita huwa vita vya dunia baada ya muda upi?
"Mara nyingi watu hufikiri kwamba vita hupangwa kwa umakini mkubwa na kwamba wanaohusika wanajua kikamilifu wanachokifanya," alisema Margaret MacMillan, profesa wa historia ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza, katika mahojiano na BBC Global Story.
"Kwa kweli, ukiangalia vita vya zamani Vita vya Kwanza vya Dunia mambo mengi yaliyoanzisha vita hivyo yalitokana na ajali na kutathmini wapinzani vibaya," alielezea Profesa MacMillan.
MacMillan anasema kuwa kuuawa kwa Franz Ferdinand, mjukuu wa mfalme wa Austria-Hungary Franz Joseph I, kulichochea mfululizo wa matukio uliosababisha Vita vya Kwanza vya Dunia mwaka 1914.
Ndani ya wiki chache, miungano ya kimataifa uliingiza Ulaya yote vitani.
Austria-Hungary dhidi ya Serbia, Ujerumani ikiunga mkono Austria, Urusi ikikusanya majeshi kusaidia Serbia, Ufaransa ikiunga mkono Urusi, na Uingereza pia ilijipata vitani.
Kilichofuata baadaye kiligeuka kuwa janga la kimataifa.

Chanzo cha picha, Stringer/Getty Images
Joe Maiolo, profesa wa historia ya kimataifa katika chuo cha King's College mjini London, anaelezea vita vya dunia kama vita vinavyohusisha mataifa yote makubwa.
"Katika Vita vya Kwanza vya Dunia, yalikuwa mataifa ya Ulaya. Katika Vita vya Pili vya Dunia, mataifa hayo yalijumuisha pia Marekani, Japani na China," aliiambia BBC.
Wengi bado wanaweza kusema kuwa mvutano wa sasa Mashariki ya Kati ni wa kikanda zaidi.
Lakini je, dalili ya kuongezeka kwa mzozo huu na kuwa mkubwa zaidi umeanza kujitokeza?
Katika mahojiano na BBC mwezi Februari, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema anaamini kuwa Rais wa Urusi Vladimir Putin ameanzisha vita vya tatu vya dunia, na njia pekee ya kukabiliana na hali hiyo ni kuweka shinikizo kali la kijeshi na kiuchumi ili kuilazimisha Moscow kusitisha uvamizi.
"Naamini kuwa Vladimir Putin tayari ameanzisha vita hivyo. Swali ni ni eneo gani ataweza kuliteka na ni njia gani ya kumzuia" alisema Zelensky

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hatari zipi zinaweza kutokea iwapo kutazuka vita vya tatu vya dunia?
"Nadhani nchi inayoweza kutanua mzozo huo zaidi ni Iran, au washirika wake kama vile waasi wa Kihouthi nchini Yemen," alisema Margaret MacMillan.
Kulingana na MacMillan, hatua zinazoweza kuchukuliwa na Iran kama kulenga njia za usafirishaji wa baharini au kufunga Mlango wa Hormuz zinaweza kuwa na athari za kimataifa, kwa kuvuruga usambazaji wa nishati na kuchochea mataifa makubwa kuingilia mzozo huo.
Aliongeza kuwa kuingilia kati kwa Marekani pia kunachochea hali kuwa mbaya zaidi kwani hata nchi zisizohusika moja kwa moja huathirika kiuchumi au kimkakati.
Aidha migogoro katika eneo moja inaweza kufungua fursa katika maeneo mengine.
Kwa mfano, China inaweza kuhesabu kuwa migogoro katika nchi za Magharibi unatoa nafasi kwao kuchukua hatua dhidi ya Taiwan, au Urusi ikaongeza uvamizi wake nchini Ukraine wakati dunia imeelekeza macho yake kwingine.
"Kila mara kuna hatari ya mzozo kusambaa hadi eneo moja kubwa, kwa sababu kwa kiasi fulani wahusika wanaweza kuona fursa ya kujinufaisha wakati wa machafuko.
Profesa Joe Maiolo anaamini kuwa mzozo huo utabaki kuwa wa kikanda na utahusisha nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba.
Hata hivyo, haamini kuwa China na Urusi zitavutwa kuingia vitani.
"Wazo kwamba tukio fulani linatokea duniani halafu China itaingia mara moja kuchukua Taiwan ni la kipuuzi kabisa."alisema
"Lakini tukizungumza kuhusu vita vya dunia, yaani Vita vya Tatu vya Dunia, sioni dalili zozote kwamba China au Urusi zinataka kuhusika moja kwa moja, na bila shaka Ulaya pia haitaki."
Profesa Maiolo naamini kuwa China ina mawazo mengine katika uhusiano wake wa kidiplomasia na Rais Donald Trump "Wakati mpinzani wako anafanya kosa kubwa la kimkakati, muache aendelee kulifanya," alisema.
Jukumu la viongozi

Chanzo cha picha, Getty Images
Margaret MacMillan anaelezea kuwa historia inaonyesha kwamba mara nyingi vita huchochewa na kiburi, kutaka kuheshimika, au hofu ya mpinzani.
Waziri Mkuu wa Ufaransa, Georges Clemenceau, alisema wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia kwamba kupata amani ni vigumu zaidi kuliko kuanzisha vita.
Kulingana na MacMillan, kiburi kinaweza kuwa sababu ya kiongozi kuanzisha vita akitoa mfano wa Vladimir Putin kuivamia Ukraine.
Baada ya kuivamia Ukraine miaka minne iliyopita, Rais Putin alitangaza kwamba lengo lake lilikuwa "kulemaza uwezo wa kijeshi na kuondoa udikteta" nchini Ukraine, ila Urusi inasema malengo yake ya kijeshi nchini humo bado hayaajafikiwa.
Diplomasia

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Ili vita kusitishwa, diplomasia hutumika kwa kiwango kikubwa.
"Unahitaji kuuelewa upande wa pil na unahitaji kuendelea kuwasiliana nao," Anasema MacMillan.
Umiliki wa silaha za nyuklia umekuwa jambo la kuzingatiwa katika vita vinavyohusu mataifa makubwa.















