Hatima ya mazungumzo ya Marekani na Iran katika kivuli cha kutoaminiana

ol

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock

Muda wa kusoma: Dakika 4

Wakati Donald Trump aliposema wiki hii kwamba Marekani na Iran zilifanya "mazungumzo mazuri na yenye tija" kuhusu kukomesha vita, majibu ya Iran yalikuwa ya haraka na ya moja kwa moja.

Maafisa wa Iran walikana mazungumzo yoyote yaliyofanyika. Msemaji mmoja wa jeshi hata alidhihaki dai hilo, akisema Wamarekani wamekuwa "wakijadiliana wenyewe."

Kutoelewana kuko wazi. Washington inazungumzia maendeleo katika mazungumzo; Tehran inakataa kabisa. Lakini hili halihusu tu kutokubaliana; pia inaonyesha kutoaminiana.

Kutokuaminiana huko kunatokana na matukio ya hivi karibuni.

Mwaka uliopita, mazungumzo kati ya pande hizo mbili yaliongeza matumaini ya kupunguza mvutano, huku duru ya mwisho ya mazungumzo ikisemwa na mwenyeji Oman kuwa ilishughulikia wasiwasi wa Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Lakini mazungumzo hayo yalifuatiwa na mashambulizi ya kijeshi ya Israel na Marekani dhidi ya Iran.

Kwa mtazamo wa Iran, mazungumzo hayajapunguza uwezekano wa kutokea vita; yamefanyika kabla tu ya vita. Ndiyo maana madai ya Trump yanashukiwa.

Lakini kukataa kwa Iran hakumaanishi kwamba inapinga mazungumzo. Kuna mengi zaidi yanayoendelea.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hata maafisa wanaounga mkono diplomasia wako chini ya shinikizo. Kwani kujaribu kuleta mazungumzo tena, itakuwa hatari. Hakuna ishara kwamba wakati huu mazungumzo hayo yataleta hali tofauti.

Hata kabla ya chapisho la Trump kwenye Truth Social siku ya Jumatatu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi alisema Iran haitafuti mazungumzo au kusitisha mapigano na iko tayari kuendelea na mapigano.

Msemaji wa Serikali ya Iran alikataa pendekezo hilo lenye vipengele 15, akisema: "Maneno ya Trump ni uongo na hayapaswi kuzingatiwa."

Lakini hii haimaanishi kwamba mlango umefungwa kabisa.

Siku ya Jumatano, Araghchi aliiambia televisheni ya taifa kwamba "taarifa tofauti" zimewafikia viongozi wakuu wa nchi - na "ikiwa msimamo unahitaji kuchukuliwa, hakika utaamuliwa."

Pia alisema sera ya Iran kwa sasa ni kuendelea "kujitetea", na Tehran "haina nia ya kujadiliana kwa sasa".

Hali ya sasa nchini Iran, ya mashambulizi na uharibifu wa miundombinu muhimu, huenda ndio sababu ya kutumia lugha kali ili kuweka masharti kuliko kukataa diplomasia kabisa.

Misimamo mikali na wastani

Siasa za ndani za Iran zinafanya mambo kuwa magumu zaidi.

Rais Masoud Pezeshkian, akiungwa mkono na makundi yenye msimamo wa wastani, dhidi ya maafisa wenye msimamo mkali wanaopinga mazungumzo.

Wakati huo huo, hata sauti hizo za wastani zinapata shida kupendekeza mazungumzo katika hali ya sasa.

Pia kuna shinikizo kutoka nje ya serikali.

Baadhi ya makundi ya upinzani yanakataa makubaliano yoyote na Jamhuri ya Kiislamu, na yameunga mkono mashambulizi kwa matumaini kwamba vita hivyo vitasababisha kuanguka kwa utawala na mabadiliko ya utawala.

Wakati huo huo, asasi za kiraia na wanaharakati wa haki za binadamu wana wasiwasi kwamba makubaliano yanaweza kuipa serikali mamlaka zaidi ya kukabiliana na wapinzani wao, hasa kwa vile vikwazo tayari vimesitishwa wakati wa vita.

Msimamo wa Iran si kuhusu itikadi pekee; pia ni kuhusu mkakati.

Tangu mzozo huo ulipozidi, Tehran imeonyesha kuwa inaweza kuvuruga mtiririko wa nishati duniani kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz. Kufunga au kupunguza shughuli katika njia hii kumeathiri sio tu masoko ya mafuta na gesi bali pia minyororo mipana ya usambazaji.

Hilo linaipa Iran nguvu.

Pengo kati ya Iran na Marekani

k

Chanzo cha picha, Reuters

Ripoti zinasema pendekezo la Trump, lilifikishwa kwa Iran kupitia Pakistan, na masharti yake ni magumu kwa Iran kuyakubali. Yanajumuisha kanuni kali kuhusu uwezo wa nyuklia wa Iran, programu za makombora, na usaidizi wake kwa washirika wa kikanda, ikikubali hayo Iran itaondolewa vikwazo na kupewa usaidizi kuhusu nishati ya nyuklia kwa matumizi ya kiraia.

Hata kwa wale walio tayari kwa makubaliano, suala kubwa zaidi ni kuaminiana. Makubaliano ya awali hayajadumu.

Mkataba wa nyuklia wa 2015 kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani, uliofikiwa baada ya miaka mingi ya mazungumzo, hatimaye ulivunjika wakati Marekani chini ya Trump ilipoachana na mkataba huo. Tehran ina shaka kwamba mkataba wowote mpya hauwezi kudumu.

Kwa hivyo, pengo kati ya pande hizo mbili linaendelea kuongezeka.

Kwa Washington, kuzungumzia kuhusu mazungumzo kunaweza kutimiza malengo ya kisiasa na kidiplomasia.

Kwa Tehran, kukataa mazungumzo husaidia kulinda msimamo wake na pia kunaonyesha mashaka yao dhidi ya Marekani.

Kwa sasa, pengo kati ya matumaini ya Marekani na kukataa kwa Iran lina uwezekano mkubwa wa kubaki.

Kulimaliza pengo hili kutahitaji zaidi ya maneno. Itahitaji dhamana kwamba mazungumzo hayatasababisha migogoro - jambo ambalo Trump anaweza pia kuhitaji kulionyesha nyumbani, baada ya kuahidi kumaliza vita, sio kuanzisha vita Mashariki ya Kati.