Masharti matano ya Trump yatakayoamua hatima ya Iran

Chanzo cha picha, Reuters/Getty Images
- Author, Mariam Mjahid
- Nafasi, Mwandishi BBC Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Vyombo vya habari vya Marekani na Israel vinaripoti kuwa utawala wa Trump kwa usaidizi wa Pakistan umeikabidhi Iran mpango wa kusitisha mapigano wenye pointi 15.
Rais Trump anasisitiza kuwa utawala wake unazungumza na "watu wanaofaa na sahihi" nchini Iran, na kwamba wanataka "sana" makubaliano ya kumaliza mzozo wa wiki nne.
Siku ya Jumanne alidokeza "tuzo muhimu sana" iliyotolewa kwa Marekani na wapatanishi wa Iran kuhusiana na mafuta na gesi, na Mlango wa bahari wa Hormuz.
Saa chache baadaye, Iran iliuambia Umoja wa Mataifa kwamba "meli zisizo na maadui" zitaruhusiwa kupita kwenye Mlango wa Bahari.
Wakati huo huo, Pentagon inatarajiwa kupeleka vikosi vya ardhini Mashariki ya Kati, kulingana na mshirika wa BBC wa Marekani, CBS News.
Haya yakijiri, hizi ndio baadhi ya vipengee ambavyo Marekani imewasilisha kwa Iran kama njia moja ya kutatua mzozo unaoendelea mashariki ya kati.
Masharti ya Trump kwa Iran ili kusitisha mapigano
Yaliyomo katika mpango wa hoja 15 ambao Donald Trump anadai kuutumia Iran hayajatolewa rasmi.
Hata hivyo, vyombo vya habari vya Israel na Marekani vinadai kwamba vinafahamu baadhi ya masharti yake.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kituo cha habari cha Israel, Channel 12, kinasema mpango huo unajumuisha mahitaji yafuatayo:
- Uharibifu wa vituo vya nyuklia vya Natanz, Isfahan, na Fordow
- Ufuatiliaji wa uwazi wa shughuli za nyuklia za Iran na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA)
- Kuachana na makundi ya kijeshi ya wakala katika eneo na kuacha kuwapatia fedha na silaha
- Kufutwa kwa uwezo wa nyuklia uliopo
- Ahadi ya kutojaribu kupata silaha za nyuklia
- Kusitisha utayarishaji wa vipengele vya nyuklia ndani ya ardhi ya Iran na kukabidhi vifaa vyote vilivyotayarishwa kwa IAEA
- Kuhakikisha Kipenyo cha Hormuz kipo wazi na kuunda "eneo huru la baharini"
- Maamuzi ya mwisho kuhusu mpango wa makombora yameahirishwa hadi baadaye, lakini yatakuwa na idadi na wigo mdogo ili kuwa na uwezo wa kinga tu.
Wakati huohuo, Pentagon inatarajiwa kutuma maelfu ya wanajeshi kutoka kikosi maalumu cha Jeshi la Marekani, 82nd Airborne Division, kwenda Mashariki ya Kati, kwa mujibu wa Reuters. Hatua hiyo itaoongeza nguvu za kijeshi za Marekani huku Rais Donald Trump akizungumza kuhusu uwezekano wa makubaliano na Tehran kuhusu kumaliza vita.
Reuters iliripoti kwa mara ya kwanza tarehe 18 Machi kuwa utawala wa Trump ulikuwa unafikira kutuma majeshi zaidi, hatua ambayo ingeweza kupanua uwezekano wa kuhusisha operesheni ndani ya ardhi ya Iran.
Hatua kama hiyo ingeongeza hatari katika mzozo ambao tayari umeshaingia wiki ya nne na kuathiri masoko ya kimataifa. Maafisa hao, waliokuwa wakizungumza kwa sharti la kutotambulika, hawakutoa maelezo ya mahali ambapo wanajeshi hao watapelekwa au lini watapofika katika eneo hilo.
Kuhusu hili, msemaji wa White House, Anna Kelly alisema "Kama tulivyoeleza, Rais Trump daima ana chaguo zote za kijeshi kwenye mikononi yake,".
Hadi sasa, hakuna uamuzi uliofanywa kutuma majeshi ndani ya Iran yenyewe, alisema chanzo kimoja, lakini hatua hii itaongeza uwezo wa Marekani kwa ajili ya operesheni zinazoweza kufanyika baadaye katika eneo hilo.
Iran itafaidika na nini?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kile ambacho Iran inaweza kupokea:
- Msaada wa Marekani wa kuendeleza mradi wa nyuklia wa kiraia huko Bushehr kwa ajili ya uzalishaji wa umeme
- Kuwekewa kizuizi cha kuondolewa kwa vikwazo vyote
- Kuondolewa kwa tishio la kuongeza vikwazo
Pia kuna ripoti kuhusu uwezekano wa mapumziko ya mapigano ya mwezi mmoja wakati wa mazungumzo, lakini hili halijathibitishwa na Ikulu ya Marekani haijatoa maelezo yoyote kuhusu jambo hilo.
Maafisa wa Iran wanasema kwamba hakuna mazungumzo yanayoendelea na Marekani na kwamba hawatakubali masharti yoyote.
Msemaji wa Makao Makuu ya Khatam al-Anbiya ya Iran, ambaye ni kamanda mkuu wa kijeshi wa nchi hiyo (bila kutaja jina la Marekani na Trump) amezungumzia kuhusu "taifa lenye nguvu kubwa duniani" - akisema "usiite kushindwa kwako makubaliano".
Ebrahim Zolfaghari amesema katika ujumbe wa video uliochapishwa na vyombo vya habari vya Iran leo kwamba "je, kiwango cha mgogoro wenu wa ndani kimefikia hatua ambapo mnajadiliana wenyewe?"
"Hautaona uwekezaji wako katika eneo hilo wala bei za zamani za mafuta tena, hadi utakapoelewa kwamba utulivu katika eneo unahakikishwa na mkono wenye nguvu wa vikosi vyetu vya kijeshi. Utulivu huja kupitia nguvu," Zolfaghari alisema.
Aliongeza kwamba "mtu kama sisi hatuwezi kufikia makubaliano na mtu kama wewe. Sio sasa, wala milele".
Israel imesema nini kuhusu mpango huo wa pointi 15 wa Trump?

Waziri wa Uchumi wa Israel, Nir Barkat, amewaambia BBC kwamba "labda" siyo jambo la kawaida kwamba Iran itakubali mpango wa hoja 15 unaodaiwa kuwasilishwa na utawala wa Marekani, akuelezea kama "mzuri kwenye karatasi," lakini ukihitaji dhamana ili utekelezwe.
Alisema kuwa mfumo wa Iran "hautabadilika," na malengo makuu ya Israel katika vita ni kuwaacha Wairani "bila silaha za nyuklia, bila makombora na bila makundi ya wakala."
"Ikiwa tutafikia lengo hilo kesho kwao kuinua bendera nyeupe au kusaini mkataba na kujizatiti kwa mkataba huo, au tutahitaji mashambulizi ya ziada dhidi ya mfumo wa Iran, ikiwemo kile ninachoamini Rais Trump anapanga… Nina imani kwamba Rais Trump na Waziri Mkuu Netanyahu wako sawa kuhusu malengo haya na tutayafanikisha kwa njia moja au nyingine," alisema.
"Kwa upande mmoja, labda Trump anafungua mazungumzo, lakini pia anaweka wanajeshi katika eneo, na kwa msingi anaeleza kwa wananchi wa Iran kwamba tunamaanisha biashara," alisema.
"Ninaamini mwishoni mwa duru hii, tutafanikisha malengo haya, iwe kwa mkataba au bila mkataba."
Kuhusu swali la kama Israel na Marekani wako sambamba kuhusu mpango wa hoja 15 yenyewe, alisema: "Tuaachie kuwa dhahiri."
Alipoulizwa moja kwa moja kama Israel ilihusika katika kuandaa mapendekezo hayo, alitazama chini, kuinua mikono yake huku akitabasamu kidogo, na kubaki kimya.
Duru ya mazungumzo kati ya Marekani na Iran itafanyika wapi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Qatar imetangaza kwamba "haishiriki" katika juhudi zozote za upatanishi wa moja kwa moja kati ya Marekani na Iran, ikibainisha kwamba inaunga mkono "njia za kidiplomasia" zinazolenga kukomesha vita, kulingana na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar Majid Al-Ansari.
"Kwa sasa hakuna juhudi za moja kwa moja za Qatar zinazohusiana na upatanishi kati ya pande hizo mbili," Al-Ansari alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari wa kila wiki katika Wizara ya Mambo ya Nje, akielezea kwamba "lengo la Qatar katika hatua ya sasa ni kuilinda nchi na kushughulikia hasara zinazotokana na mashambulizi mbalimbali ambayo imekabiliwa nayo
Alibainisha kwamba msimamo wa Qatar tangu siku ya kwanza ya vita "umekuwa wazi, kwamba vita hivi lazima vimalizike kwa njia za kidiplomasia, na huu ndio msimamo wetu kuhusu migogoro yote duniani.
Wkati huo huo, Mwanadiplomasia wa Iran anayefahamu uwezekano wa mazungumzo kati ya Iran na Marekani ameiambia BBC News Urdu kuwa kuna "uwezekano mdogo wa mazungumzo hayo."
"Ikiwa uamuzi wa mwisho utafikiwa (kuhusu mazungumzo hayo), Pakistan inaweza kuwa moja ya maeneo ya kuyafanyia majadiliano," alisema, kwa sharti la kutotajwa jina.
"Tunangoja maelezo kutoka Wizara yetu ya Mambo ya Nje."
Kwanini mashambulizi bado yanaendelea kushuhudiwa Tehran

Chanzo cha picha, Getty Images
Licha ya migongano katika malengo ya Marekani, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amefafanua wazi kuwa nchi yake itaendelea kushambulia Iran na mshirika wake, Hezbollah, kusini mwa Lebanon.
Katika ujumbe mfupi wa video, alionya:"Tutalinda maslahi yetu kwa gharama yoyote."
Iran bado ina uwezo wa kulipiza kisasi dhidi ya Israel, huku shambulio lake la hivi karibuni la makombora lilisababisha shimo kubwa katika eneo la makazi mjini Tel Aviv.
Maafisa wanasema shambulio hilo lilitumia takriban kilo 100 za vilipuzi.
"Kwa sasa ninaona bango karibu nami lenye picha ya Donald Trump akiwa na bendera ya Marekani na maneno: 'Bwana Rais, fanya hili ulifanikishe.'"
Inaonekana kuwa Israel haina mpango wa kumaliza mzozo huu hivi karibuni.
Usiku wa kuamkia leo Jumanne ya tarehe 25 mwezi Machi 2026, mashambulizi kati ya Israel na Iran yanaendelea, huku jeshi la Israel likitoa onyo kwa wakazi wa kusini mwa Lebanon kuondoka katika maeneo yao kutokana na hatari ya mashambulizi zaidi.
Aidha, wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, inatarajiwa kupeleka wanajeshi kutoka kikosi cha 82nd Airborne kwenda Mashariki ya Kati, kwa mujibu wa taarifa ya CBS News.
Kwa sasa, dunia inafuatilia kwa makini maendeleo ya mazungumzo haya.














