Dunia haina budi ila kujadiliana na Iran - Financial Times

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 4

Tunaanza uchambuzi wetu na gazeti la the Financial Times na habari yenye mada "Iran huenda ikaibuka kuwa na nguvu na ikawa hatari zaidi baada ya vita hivi"

Uchambuzi huo unasema kuwa Rais wa Marekani Donald Trump "amekuwa akitumia ujuzi kushinikiza adui wake kutumia nguvu walizonazo" na kuongezea kuwa vita vya kibiashara na China viliisha wakati Beijing ilizuia uuzaji wa madini yake adimu, na kuchochea Washington kupunguza ushuru waliowaekea.

Kulingana na uchambuzi huo wa Financial Times, njia sawia inatumika Iran, kuonyesha ubabe wake kupitia mlango wa bahari wa Hormuz kwa kutishia kuifunga.

Iran inatumia mlango wa bahari wa Hormuz kwa manufaa yake ili kuibuka na nguvu katika jukwaa la kimataifa baada ya vita kuisha.

Iran pia imeweza kusababisha uharibifu katika mataifa ya Ghuba kama vile Saudi Arabia na Falme za Kiarabu na kuhatarisha usalama wa mataifa haya.

Huenda Iran ikapata kipato zaidi kwa kutoza ada za ziada meli zinazopitia mlango wa bahari wa Hormuz.

Kwa kawaida zaidi ya meli 140 hupitia mlango huo wa bahari, na iwapo meli hizo zitatozwa ada zaidi, basi itaipa Iran faida ya mabilioni ya fedha.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Marco Rubio, amekosoa vikali ada zaidi inayotozwa meli zinazopita eneo hilo akisema ni kinyume cha sheria na haikubaliki.

Lakini njia mbadala ni ipi?

Uchambuzi huo unasema hakuna njia sahihi haswa, na kuwatuma wanajeshi wa Marekani kukiteka kisiwa cha Kharg hakutasuluhisha changamoto hiyo.

Wataalam wa masuala ya kijeshi wanasema jiografia ya eneo hilo la Hormuz, inaifanya kuwa vigumu kukidhibiti kikamilifu, haswa ukizingatia uwezo wa kijeshi wa Iran.

"Vita ambavyo havikufaa kuanza"

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Gazeti la Uingereza la The Guardian lilichapisha uchambuzi wenye mada "Vita vya Trump nchini Iran."

Gazeti hilo linasema kuendelea kwa vita vya Iran kwa wiki ya tano kunaonyesha kwamba vita hivyo vilianza bila mkakati wa kina.

Uchambuzi huo unasema kuwa semi za kukinzana kutoka kwa Rais Trump zimekuwa nyingi mno, na haziwezi kuficha upungufu wa mafuta na bidhaa unaoshuhudiwa duniani.

Hali hii ina uwezekano mkubwa wa kuwa mbaya zaidi, ikizingatiwa kutokuwepo kwa dalili zozote za ushindi wa haraka wa Marekani au,kuanguka kwa Iran.

Gazeti la The Guardian linaelezea hali hiyo kuwa inafanana zaidi na "vita vya kuchoshana," ambapo kila upande unatangaza mafanikio yake na kupuuza kushindwa kwake, huku ukisisitiza makosa ya mpinzani wake.

Gazeti hilo linaeleza kuwa vita hivyo havikupaswa kuanza kabisa, kwa kuwa tishio halikuwa la dharura na malengo hayakufafanuliwa wazi, jambo linalodhoofisha uhalali wake.

Donald Trump na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, wanabeba jukumu la kuanzisha mgogoro huo.

Gazeti hilo linasema njia bora zaidi ya kutatua vita hivyo ni kufanya mazungumzo bila masharti ya awali.

"Donald Trump anatoa vitisho vya kuongeza mvutano zaidi" gazeti hilo linasema, likiongezea kuwa hakuna dalili ya diplomasia kutumika kuleta , huku uimarishaji wa nguvu za kijeshi ukiendelea.

Uchambuzi huo unasema kuwa Washington inalenga kubadilisha utawala wa Iran, huku Tehran ikionekana kuwa bado iko imara.

Kwa mujibu wa wachambuzi, Marekani imekuwa ikiona mabadiliko ya utawala kama sehemu ya malengo yake ya kimkakati, wakati Iran inaona shinikizo hilo kuwa jaribio la kuingilia mamlaka yake na hivyo kulipinga vikali.

Katika muktadha unaohusiana, gazeti hilo linaamini kuwa mgogoro na Iran hauwezi kutenganishwa na vita vya Gaza, likibainisha kuwa kukosekana kwa suluhisho eneo la Gaza kunachochewa na Iran na washirika wake .

Gazeti hilo pia linamkosoa Donald Trump kwa msimamo wake wa kuiunga mkono Israel licha ya kile inachokiita "uhalifu wa kivita" dhidi ya Wapalestina, Lebanon na Iran, ikisema kuwa hali hiyo inadhoofisha uwezekano wa kupata suluhisho la kidiplomasia nchini Iran.

Gazeti hilo linahitimisha uchambuzi wake kwa kusema kuwa "njia yoyote ya kusitisha vita na Iran huenda isihusishe Tehran pekee, bali pia Gaza.

.

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock

Tunamalizia uchambuzi wetu na makala katika gazeti la The Wall Street Journal yenye mada "Dunia inahitaji Umoja wa Mataifa wenye nguvu zaidi."

Uchambuzi huo unasema kuwa kila uvunjaji wa sheria za kimataifa husababisha uvunjaji mwingine, ukitaja mfululizo wa migogoro kuanzia Afghanistan hadi Gaza, kupitia Iraq, Libya, Syria, Iran na Venezuela.

Gazeti hilo linasema ukiukwaji wa sheria za kimataifa unatokana na"ukimya wa baraza la ulinzi la Umoja wa Mataifa"

Gazeti hilo linasema matumizi ya kura ya turufu (veto) na wanachama wa kudumu yamegeuka kuwa chombo kinachotumika kama "kinga na silaha" nje ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, jambo linaloweka hatma ya mamilioni ya watu hatarini.

Gazeti hilo linasisitiza kuwa sheria zilizowekwa na mashirika ya kimataifa hazina tena uwezo wa kuzizuia nchi zenye nguvu, huku hali ya kutokuwepo kwa usalama ikiongezeka kutokana na kukosekana kwa mchango madhubuti wa taasisi hizo.