Vita vya Iran vyachangia kupanda kwa bei ya kondomu

Chanzo cha picha, Reuters
Kampuni ya Carix, mojawapo ya kampuni kubwa ambazo hutengeneza mipira ya kondomu, imetangaza kuwa itaongeza bei ya bidhaa hizo kwa 30% au zaidi iwapo vita vitaendelea nchini Iran.
Kampuni hiyo iliopo nchini Malaysia, imesema vita vinavyoendelea Iran, vimefanya iwe vigumu kupata mali ghafi ya kutengeneza kondomu.
Goh Mia Kat, mkurugenzi wa Carex, alisema gharama ya kutengeneza kondomu hizo imepanda tangu vita kuanza.
Carex huzalisha zaidi ya kondomu billioni 5 kila mwaka na huuzia makampuni makubwa kama Durex na Trojan, ikiwemo na wizara za afya za serikali mbalimbali.
Goh alitoa taarifa hiyo katika mahojiano na shirika la habari la Reuters na Bloomberg.
Usambazaji wa mafuta duniani umeathiriwa na mgogoro unaoendelea nchini Iran, huku taifa hilo likitishia kushambulia meli zitakazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, kama hatua ya kujibu mashambulizi ya Marekani na Israel.

Chanzo cha picha, Getty Images
Vitisho hivyo vimesababisha njia hiyo muhimu ya majini kufungwa na kuvuruga usafirishaji wa bidhaa muhimu duniani.
Zaidi ya 20% ya mafuta yote duniani hupitia Hormuz, ikiwemo gesi na bidhaa zingine za petroli.
Kampuni ya Carix inategemea sana bidhaa za petroli ikiwemo ammonia ambayo hutumika kutengeneza ulimbo wa mpira, pamoja na silikoni.
Mahitaji ya kondomu yameongezeka kote duniani kwa 30% mwaka huu, na ongezeko hili limekuja pamoja na ongezeko la bei ya kusafirisha bidhaa kwa meli, na kuchelewesha usafirishaji wa bidhaa hizo ambako kumechangia upungufu wa kondomu kwenye soko.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Goh aliambia shirika la habari la Bloomberg kuwa "Katika nyakati hizi ngumu, mahitaji ya kondomu huongezeka kwa sababu ya sintofahamu kuhusu siku za usoni, haswa kuhusu ajira, na wengi wanazuia kupata watoto sasa ili kupunguza gharama"
Mkurugenzi huyo anasisitiza kuwa, kupanda kwa bei ya kondomu ni kutokana na athari za vita vya Marekani na Israel nchini Iran, na imechochea kupanda kwa bei ya chakula na bidhaa zingine.
Vita hivyo pia vimechangia kupanda kwa gharama ya safari za ndege,huku kuvurugwa kwa safari za meli zikisababisha kupanda kwa bei ya mbolea na madini ya helium ambayo hutumika kutengeneza vifaa vya kompyuta.
Kampuni za kutengeneza maji ya chupa pia zimepata shinikizo za kuongeza bei ya bidhaa hiyo kutokana na ukosefu wa mali ghafi ya kutengeneza chupa za maji.
Mapema mwezi huu Umoja wa Mataifa ilionya kuwa bei ya sukari, bidhaa za maziwa na matunda yatapanda bei kutokana na kuongezeka kwa gharama ya usafiri.
Bado haijulikani ni lini Marekani na Iran wataafikia makubaliano ya kumaliza vita hivyo baada ya mazungumzo yaliyokuwa yafanyike wiki hii yakikosa kufanyika, huku Trump akiongeza muda wa usitishaji mapigano.















