Je, kauli za Trump kuhusu kujiondoa NATO zina maana gani kwa muungano huo?

Maafisa wa jeshi la wanamaji la Romania kutoka katika kikosi cha Jeshi la Wanamaji la Romania 'King Ferdinand' wakifuatilia shabaha ya ufyatuaji wa risasi wa moja kwa moja wa jeshi la wanamaji la NATO 'Sea Shield 26' katika Bahari Nyeusi.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Muungano wa Nato wenye umri wa miaka 77 sasa una wanachama 32, lakini nguvu ya jeshi la Marekani ni muhimu sana.
    • Author, Lyse Doucet
    • Nafasi, Chief international correspondent
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Miongoni maonyo yote aliyonayo Rais Trump, kuiondoa Marekani katika muungano wa kijeshi wa NATO ni mojawapo ya vitisho ambavyo amekuwa akivitumia mara kwa mara.

Sasa analirejea tena onyo hillo.

Alipoulizwa na gazeti la Uingereza la Telegraph iwapo anafikiria upya uanachama wa Marekani katika NATO, alisema: "Naam… ningesema [suala hilo] limevuka hatua ya kufikiria upya," huku akilalamika tena kwamba washirika wake hawakujiunga na operesheni za kijeshi za Marekani, pamoja na Israel, dhidi ya Iran.

"Naona tu inapaswa kuwa jambo la moja kwa moja," alisisitiza katika mahojiano hayo.

Matamshi makali ya Trump yanaonesha tena kutokuelewa kwake jinsi muungano huu wa wanachama 32 unavyofanya kazi.

Kifungu cha 5 cha NATO kinawajibisha wanachama wake katika ulinzi wa pamoja. Shambulio dhidi ya mwanachama mmoja huchukuliwa kuwa shambulio dhidi ya wote; hata hivyo, utekelezaji wa kanuni hii huhitaji makubaliano ya pamoja. Aidha, mkataba wa mwaka 1949 ulilenga migogoro katika Ulaya na Amerika Kaskazini pekee.

Mwanachama mmoja baada ya mwingine amesita kujiunga na vita ambavyo hawakushirikishwa katika kuvipanga, hasa kwa kuwa bado hawaelewi malengo yake kutokana na ujumbe unaokinzana kutoka kwa utawala wa Trump.

Kifungu cha 5 kimewahi kutumika mara moja tu, kufuatia mashambulizi ya tarehe 11 Septemba mwaka 2001 nchini Marekani.

Trump pia aliitaja Ukraine katika mahojiano hayo, akisema: "Tumekuwa pale moja kwa moja, ikiwemo Ukraine."

Baada ya uvamizi mkubwa wa Urusi dhidi ya Ukraine mwezi Februari 2022, Rais wa wakati huo wa Marekani Joe Biden alichukua jukumu la kuongoza katika kuratibu mwitikio wa serikali mbalimbali za Magharibi, akiamini kuwa hatua za Rais Putin zilikuwa tishio kwa wote.

NATO kama muungano ilitoa msaada, lakini iliepuka hatari ya kuhusika moja kwa moja kama upande katika mzozo huo.

Hata kabla ya Trump kuingia Ikulu ya White House mnamo 2017, mara kwa mara alipuuza Nato kama "chui wa karatasi," akaielezea kama "ya kizamani", na akasema kwamba "ilikuwa ikigharimu pesa nyingi" kwa Marekani.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwaka huu, Trump ameudharau muungano huo akisema kwamba Urusi ingekuwa imeikalia Ukraine yote kama Marekani isingekuwa mhimili mkuu wa utekelezaji ndani ya NATO.

Karibu aiondoe Marekani katika muungano huo mapema mwaka 2019, wakati wa muhula wake wa kwanza.

"Tuliona dalili wazi kwamba Trump alikuwa akijiandaa kutekeleza tishio lake," aliandika aliyekuwa Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg, katika kumbukumbu zake, On My Watch.

Stoltenberg alisimulia jinsi alivyojitokeza katika Fox News na kumpongeza Trump kwa kuwashinikiza washirika wa NATO kuongeza matumizi yao ya kijeshi.

Kwa mujibu wa simulizi lake, Trump alitambua mara moja pongezi hizo kupitia mitandao ya kijamii, na baadaye hakutoa hotuba ambayo Ikulu ya Marekani ilikuwa imeandaa kuhusu kujitoa kwa Marekani.

Kiini cha malalamiko ya Trump kilikuwa makubaliano ya mwaka 2014 kwamba nchi zinapaswa kutumia asilimia 2 ya pato lao la taifa (GDP) katika ulinzi; wakati huo, lilikuwa likichukuliwa kama mwongozo tu.

Matumizi ya kijeshi yameongezeka kwa kiasi kikubwa kwa karibu wanachama wote wa NATO, kwa baadhi ni kutokana na vitisho vya Trump, na kwa wengine ni kutokana na tishio linaloongezeka kutoka Urusi.

Mgogoro huu mpya utaimarisha tena azma ya nchi za Ulaya na Canada kuimarisha ulinzi wao na kujitegemea zaidi katika usalama wao. Hata hivyo, ukweli usiopingika ni kwamba nguvu ya kijeshi ya Marekani ina umuhimu mkubwa sana.

Bajeti ya kijeshi ya Marekani sasa inachangia takriban asilimia 62 ya matumizi yote ya ulinzi ya NATO, na Idara ya Ulinzi ya Marekani ina rasilimali na uwezo wa kijasusi ambao wengine bado hawawezi kulingana nao.

Trump amejifunga tai nyekundu na koti ya suti dhidi ya pazia la rangi ya dhahabu

Chanzo cha picha, Getty

Maelezo ya picha, Trump aliliambia gazeti la Telegraph la Uingereza kuwa anatafakari upya uanachama wa Marekani katika Nato

Safari hii, Waziri wake wa Mambo ya Nje, Marco Rubio, ambaye anajiita mfuasi wa zamani wa muungano huo, naye ametoa maoni.

"Nafikiri hakuna shaka kwamba, kwa bahati mbaya, baada ya mzozo huu kumalizika tutalazimika kuupitia upya uhusiano huu," aliiambia Fox News.

Akirejelea kambi za kijeshi za Marekani barani Ulaya, alisema kutotumika kwake "kulinda maslahi ya Marekani" kunamaanisha kuwa "NATO ni njia ya upande mmoja."

Uingereza hapo awali ilikataa kuruhusu ndege za kivita za Marekani kutumia kambi zake, lakini baadaye ilibadili msimamo na kusema zinaweza kutumika kwa "operesheni za kujihami."

Hata hivyo, kuchelewa huko kumeendelea kubezwa na Trump pamoja na waziri wake wa ulinzi, Pete Hegseth, ambaye hujiita "Waziri wa Vita."

Wamekuwa wakimkejeli Waziri Mkuu Keir Starmer wakisema si "Churchill" — wakimrejelea kiongozi wa Uingereza wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Jumanne, Italia ilikataa kuruhusu ndege za Marekani kutua zilipokuwa zikielekea Mashariki ya Kati kwa operesheni za kijeshi.

Hispania nayo imefunga anga lake kwa ndege za Marekani zinazotekeleza mashambulizi dhidi ya Iran.

Rubio aliongeza kuwa "mwishowe" ni Rais anayeamua suala hili.

Hata hivyo, si uamuzi wake pekee.

Bunge la Marekani lilipiga kura mwishoni mwa mwaka 2023 kupiga marufuku rais kujiondoa NATO bila idhini ya theluthi mbili ya Seneti au sheria maalum ya Bunge.

Viongozi wa NATO na hasa Katibu Mkuu wa sasa Mark Rutte watalazimika tena kutumia muda kumshawishi na kumbembeleza Trump kwamba ni kwa maslahi yake na ya Marekani kubaki katika muungano huo.

Rutte, kama Stoltenberg, hujulikana kama "mnong'onezaji wa Trump" kwa juhudi zake za hadharani na faraghani za kumuweka rais huyo asiye tabirika upande wao.

Rutte, aliyekuwa kiongozi wa Uholanzi, anaonekana kwa kiasi kikubwa kuwa alichangia kumrudisha nyuma Trump kutoka kwenye ukingo wa kutekeleza tishio lake la "kuichukua" Greenland, eneo lenye mamlaka ya ndani la Denmark, mwanachama wa NATO mapema mwaka huu.

Hata hivyo, Rutte pia amekosolewa na baadhi ya nchi wanachama kwa kuunga mkono kwa nguvu vita dhidi ya Iran, ambavyo alisema Trump anavifanya "kuifanya dunia nzima kuwa salama."

Lakini kipaumbele chake kikuu ni kudumisha umoja wa muungano huo wa miaka 77 wakati unakabiliwa na vitisho vinavyoongezeka nchini Ukraine, Mashariki ya Kati, na hata kutoka Ikulu ya Marekani.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid