'Wewe si dada yangu tena' - Vita vyachochea migogoro ndani ya familia za Iran

    • Author, Ghoncheh Habibiazad
    • Nafasi, BBC News Persian
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Alimwambia: "Wewe si dada yangu tena," naye akamjibu: "Nenda zako kuzimu."

Mabishano haya kati ya mwanaume na dada yake katika mji mmoja karibu na Tehran - yaliyoshuhudiwa na kusimuliwa na ndugu yao - yanaonyesha kwa uwazi migogoro mikali inayozuka ndani ya familia na marafiki wakati mashambulizi ya Marekani na Israel yanaendelea.

Ndugu huyo, tunamwita Sina, anasema kuwa familia yao ilipokusanyika hivi karibuni nyumbani kwa bibi yao, hisia zililipuka haraka na kufichua mgawanyiko mkubwa uliopo.

Mjomba wake, ambaye ni mwanachama wa Basij (kikundi cha kujitolea kinachotumiwa mara nyingi kukandamiza upinzani nchini Iran), alikataa hata kumsalimia dada yake tumbo moja ambaye anapinga serikali iliyopo madarakani.

Baada ya mabishano yao, mjomba huyo "alikaa kimya sana… kisha akaondoka mapema," anasema Sina.

Yeye na vijana wengine wa Iran wameelezea matukio ya kihisia sana huku mgawanyiko ukizidi kuongezeka kutokana na vita.

Hata miongoni mwa wanaopinga serikali, kuna tofauti kubwa za maoni kuhusu kama vita hivi vitasaidia au vitaharibu juhudi za kuleta mabadiliko.

Licha ya serikali kukata huduma ya intaneti, BBC imeweza kuendelea kuwasiliana na baadhi ya Wairani wachache waliopata njia za kubaki mtandaoni.

Nchini Iran, mtu anaweza kufungwa jela kwa kuzungumza na vyombo fulani vya habari vya kimataifa. Hata hivyo, katika kipindi hiki cha vita cha takriban mwezi mmoja, watu hawa wamekuwa wakituma ujumbe wa maandishi mara kwa mara na wakati mwingine kupiga simu za sauti na kutumia BBC.

Mwanzoni walihisi mshtuko na hofu, lakini sasa wanajaribu kuzoea hali hiyo, kubadilisha maeneo wanapoishi na ratiba zao za kila siku.

Wanasimulia maisha yao ya kawaida katikati ya vita, kufanya mazoezi ya yoga huku wakisikia milipuko, kula keki ya siku ya kuzaliwa peke yao, au kwenda kwenye kahawa zisizo kuwa na watu wengi.

Pia, katika maelezo ya kibinafsi zaidi, wameeleza jinsi vita hivi vinavyoathiri mahusiano yao. Majina yote yaliyotumika yamebadilishwa.

Mwishoni mwa mwezi Machi, Wairani walisherehekea Nowruz, sikukuu ya mwaka mpya wa Kiajemi inayoadhimisha kuanza kwa majira ya kuchipua, na huwa ni wakati wa familia kukutana pamoja.

Sina, mwenye umri wa miaka ya ishirini, anapinga serikali ya kidini na anaunga mkono mashambulizi ya Marekani na Israel, akiamini yataisaidia kuangusha serikali hiyo.

Anasema mjomba wake, ambaye ni mwanachama wa Basij, hakuwa akihudhuria mikusanyiko ya familia kwa Nowruz miaka ya karibuni, lakini safari hii alikuja, jambo lililowashangaza wengi. "Kwa kawaida hatuzungumzi naye, wala na watoto wake," anasema Sina.

Anasema hajaongea sana na mjomba wake tangu maandamano makubwa ya mwaka 2022 baada ya kifo cha Mahsa Amini akiwa mikononi mwa polisi, akituhumiwa kutovaa hijabu ipasavyo.

Hivi majuzi, Iran iliona ukandamizaji ambao haujawahi kushuhudiwa na Basij na vikosi vingine vya usalama dhidi ya maandamano yaliyoenea nchini kote mnamo Desemba na Januari.

Takriban waandamanaji 6,508 waliuawa na 53,000 kukamatwa, kulingana na Shirika la Habari la Wanaharakati wa Haki za Kibinadamu (HRANA) lenye makao yake nchini Marekani.

Sina anasema kuwa mjomba wake aliwahi kusema kwa hasira kwamba hata kama watoto wake mwenyewe wangeshiriki maandamano na kuuawa, asingekwenda hata kuchukua miili yao.

Hata hivyo, sasa anaonekana "kuogopa kufa" katika vita hivi na ameanza kujaribu kurekebisha mahusiano na baadhi ya wanafamilia, hasa mama yake - bibi yake Sina.

Katika sherehe za Nowruz, yeye na mke wake "walionekana wanyonge na wasio na matumaini," anasema Sina. "Sikubishana nao. Wanapaswa kuwa gerezani."

Kwa upande mwingine, kijana mwingine aitwaye Kaveh kutoka Tehran alisherehekea Nowruz peke yake.

Anasema uhusiano wake na dada yake ambaye pia ni mwanachama wa Basij ulikuwa tayari mgumu. Baada ya kushiriki maandamano ya 2022, dada yake alianza kumkosoa na hata hakuonyesha huruma kwa marafiki zake waliouawa.

Kaveh amekuwa akiwapatia marafiki na familia intaneti kupitia Starlink, huduma ya satelaiti ya SpaceX.

Nchini Iran, kutumia au kumiliki vifaa hivyo kunaweza kukupeleka jela hadi miaka miwili.

Mwanzoni aliungana na familia kusherehekea, lakini baadaye aliondoka na aliporudi aligundua dada yake alikuwa amezima mtandao wake wa Starlink. Alipomuuliza, ugomvi ulizuka.

"Siwezi kumvumilia tena… niligombana naye na kuondoka," anasema.

"Nilikuwa na hamu sana ya sherehe za Nowruz… nilitaka kuwa na familia," alisema alipokuwa akirejea nyumbani peke yake. "Lakini sasa sina ile hisia tena."

Wairani wengi hawana kabisa intaneti. Vifaa vya Starlink ni ghali na pia ni haramu, hivyo wanaovitumia ni wachache wenye uwezo. Wengine wachache hutumia VPN.

Wengi wanaozungumza na BBC Persian wanaipinga serikali ya Iran, lakini hata miongoni mwao kuna tofauti kubwa kuhusu vita hivi.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu, watu 1,900 wameuawa nchini Iran na mashambulizi ya Marekani na Israel, huku HRANA ikiweka jumla ya watu 3,400, zaidi ya 1,500 kati yao wakiwa raia.

Maral, mwanafunzi wa miaka ya ishirini kutoka Rasht, anasema anachoshwa na baba yake kwa kuendelea kuunga mkono vita.

Yeye ni mfuasi mwenye shauku wa Reza Pahlavi, mwana mfalme wa Iran kabla ya mapinduzi ya 1979.

Pahlavi sasa anaishi Marekani na amejiweka kama kiongozi wa mpito wa nchi hiyo. Anaunga mkono mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran licha ya vifo vinavyoongezeka, akielezea mashambulizi hayo kama "uingiliaji kati wa kibinadamu" na hivi karibuni akiitaka Marekani "kusalia mkondo".

Amepata umaarufu nchini Iran katika miezi ya hivi karibuni kama kiongozi wa upinzani, na baadhi ya waandamanaji katika maandamano ya Januari wakiimba jina lake.

"Nataka tu vita hivi viishe haraka iwezekanavyo," anasema Maral. "Watu wengi wa kawaida wamekufa."

Anasema "hukasirika" kwa sababu baba yake "ana matumaini makubwa", hata mabomu yanapoanguka.

"Tunajaribu kuzungumza naye, lakini anaendelea tu kuhusu 'Mfalme, Mkuu," anasema.

"Baba yangu anaishi katika dhana hii kwamba Iran itafungua mipaka yake na ndani ya miaka mitano kila kitu kitajengwa upya, kila kitu kitakuwa sawa. Anashawishiwa na propaganda za Israel kwamba nchi hizo mbili zitakuwa marafiki."

Baba na mama yake mara nyingi hubishana juu ya Pahlavi, anaongeza.

Wakati huo huo, Tara kutoka Tehran anasema familia yake ilimkosoa mwanzoni kwa kupinga vita.

"Wote wanaunga mkono mashambulizi… mama na dada yangu waliniambia: 'Hujapoteza mtu yeyote, ndiyo maana unapinga vita.'"

Lakini Tara anasema: "Hata katika vita hivi, maelfu ya watu wasio na hatia wanaweza kufa bila hata kukumbukwa."

Hata hivyo, anasema, mtazamo wa dadake - kama ule wa Wairani wengine kadhaa ambao BBC imesikia kutoka kwao - umepungua huku mashambulizi yakiendelea. Hivi majuzi, baada ya eneo la karibu kugongwa, anasema dada yake alisema tu: "Natumai vita viishe hivi karibuni."

Licha ya tofauti zao, familia bado hujaribu kuwa pamoja kila wanapokwenda.

Kwa sababu, kama anavyosema Tara: "Angalau tukishambuliwa, tutakufa pamoja."

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi