Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi ujasusi wa Marekani na Uingereza ulivyopindua serikali ya Iran mwaka wa 1953
Mwezi Agosti tarehe 19, mwaka wa 1953, Waziri mkuu wa Iran aliyechaguliwa wakati huo Mohammad Mossadegh alipinduliwa , baada ya oparesheni iliyoendeshwa na majasusi wa Marekani wa CIA na Uingereza M16.
Mapinduzi haya yaliyoungwa mkono na Marekani na Uingereza, na yaliathiri maisha ya raia wengi wa Iran, na kuchochea Iran kuwa na sera ya kigeni ambayo inapinga mataifa ya magharibi, na kubadilisha mtazamo wa siasa za ukanda huo.
"Mapinduzi hayo yaliathiri kwa kina siasa za kisasa za Iran, na kuangushwa kwa Mossadegh kuliacha hasira na chuki, hasa dhidi ya Marekani na mataifa ya Magharibi kwa ujumla," alisema Simin Fadaee, mkuu wa Idara ya Sosholojia katika Chuo Kikuu cha Manchester nchini Uingereza.
Operesheni kabla ya Vita Baridi
Miaka 60 baadaye, mwaka wa 2013, CIA ilikiri kwa mara ya kwanza kuhusika katika mapinduzi dhidi ya Mohammad Mossadegh.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pia ilichapisha hati za siri.
Hati hizo zilitoa maelezo ya mapinduzi, ambayo CIA iliyaita Operesheni Ajax, huku MI6 ikiiita Operesheni Boot.
Moja ya hati hizo ilisema "mapinduzi ya kijeshi yaliyoangusha Mossadegh na serikali ya kitaifa ya Iran yalipangwa na kuidhinishwa na ngazi za juu zaidi za serikali." Hati zilizochapishwa na CIA zilisema.
Operesheni hiyo iliongozwa na afisa mkuu wa CIA, Kermit Roosevelt, mjukuu wa Rais wa zamazni Theodore Roosevelt.
Roosevelt aliandika utafiti wenye kichwa "Sababu zilizozosababisha mapinduzi dhidi ya Mossadegh," na kuhitimisha kwamba "mapinduzi nchini Iran yanawezekana."
Vita Baridi vilianza baada ya vita vikuu vya pili vya dunia, na katika miaka ya 1950, Iran ikawa eneo la kimkakati kwa mataifa ya Magharibi.
Kwanza, Iran ilikuwa nchi yenye utulivu kisiasa katika eneo hilo. Ilizuia Umoja wa Kisovyeti kufika eneo la Ghuba ya Uajemi na kupunguza kuenea kwa ukomunisti katika eneo hilo.
Pili, hifadhi tajiri ya mafuta ya Iran iliyogunduliwa mwaka 1909 iliendeshwa kwa kiasi kikubwa na Kampuni ya Mafuta ya Anglo-Iranian (AIOC) iliyo milikiwa na Waingereza, inayojulikana leo kama BP.
AIOC ilidhibiti uzalishaji wa mafuta kwa kutumia mikataba iliyoruhusu uzalishaji katika sehemu kubwa ya Iran.
Hata hivyo, kampuni hiyo iliingiwa na wasiwasi wakati Mohammed Mossadegh alipochaguliwa kuwa waziri mkuu mwaka wa 1951, baada ya uchaguzi wa kidemokrasia.
Kutaifisha mafuta
Iran wakati huo ilikuwa inaendeshwa kifalme, mfalme wa wakati huo akiwa Mohammad Reza Pahlavi aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo. Hata hivyo, uchaguzi wa Mohammad Mossadegh ulikuwa hatua kubwa katika demokrasia ya nchi hiyo.
Mossadegh alikuwa mwanasiasa wa mrengo wa kushoto, na alifafanua wazi kwamba lengo lake kuu lilikuwa kuwekeza kwenye mafuta ya Iran.
Hatua hii ilipokelewa vyema ndani ya Iran, lakini mataifa ya Magharibi hasa Uingereza yalionyesha wasiwasi mkubwa kuhusu mustakabali wa sekta ya mafuta, ambayo wakati huo ilikuwa biashara kubwa na yenye faida zaidi duniani.
Simin Fadaee alisema "Hasa baada ya Uingereza kupoteza India, ilijaribu kupinga utaifa wa mafuta, ambao ulikuwa tishio kwa ushawishi wake wa kiuchumi na kimkakati nchini Iran."
Marekani ilihofia kwamba Mossadegh angefungua mlango kwa ushawishi mkubwa wa Kisovyeti nchini kuingia Iran, kwani kulikuwa na harakati kali za kikomunisti katika nchi hiyo.
Uingereza ilijaribu kufanya mazungumzo na Mossadegh, lakini waziri huyo mkuu alikataa nchi za kigeni kuendesha sekta ya mafuta ya Iran.
Baadaye, Uingereza iliomba msaada kutoka Marekani, ikidai kwamba Mossadegh alikuwa tishio kwa vita dhidi ya ukomunisti
Hivyo ndivyo njama ya kumuangusha Waziri huyo mkuu ilianza.
Mpango wa Uingereza ulikuwa kumuondoa Mossadegh na kumweka Fazlullah Zahedi, ambaye walimwona kama mshirika mwenye urahisi wa kufanya naye kazi.
Walitaka Zahedi afanye kazi chini ya Shah au mfalme wa taifa hilo, ambaye alikuwa na msimamo wa ulioegemea maslahi ya Magharibi.
Hati zilizofichuliwa zinaonyesha kwamba Kermit Roosevelt Jr. alitembelea Iran mnamo Julai 1953.
Roosevelt alikutana na wawakilishi wa Iran, akakusanya msaada kutoka kwa maafisa wa kijeshi, na kutafuta wafuasi miongoni mwa viongozi wa kidini.
Pia aliwasiliana na mfalme Mohammad Reza Pahlavi, ambaye alikuwa ameikimbia nchi hiyo baada ya jaribio la awali la kumuangusha Mossadegh kutofaulu.
Simin Fadaee alisema "Walipanga njama za kisiasa, vita vya kisaikolojia, na maandamano mitaani. Walifadhili na kuandaa watu na makundi ya upinzani, wakiwemo wanasiasa wenye ushawishi, maafisa wa kijeshi, na viongozi wa kidini, na pia walitekeleza kampeni kubwa katika vyombo vya habari kuonyesha Mossadegh kama tishio kwa utulivu wa nchi hiyo."
Waliaandaa pia maandamano na vurugu mitaani, ambayo ilisababisha machafuko nchini humo.
Baada ya machafuko hayo, Fazlullah Zahedi alitumia jeshi kurejesha utulivu, akaiangusha serikali, na kumfungia gerezani waziri mkuu.
Hati zilizofichuliwa zinaonyesha kwamba waislamu wengi, wakiwemo Abolqasim Kashani, pia alihusika pakubwa katika mapinduzi hayo.
Mossadegh alikabiliwa na mashtaka ya uhaini na kuadhibiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani. Baadaye alipewa kifungo cha nyumbani, ambapo alitumikia maisha yake yote hadi alipoaga dunia mnamo 1967.
Mohammad Reza Pahlavi alirejea madarakani kama mfalme wa Iran mnamo 1953 na kutekeleza ukandamizaji na ukiuakaji wa haki za kibinadamu.
Simin Fadaee alisema: "Mapinduzi hayo yaliweka msingi wa kipindi kirefu cha udikteta, na athari zake bado zinashuhudiwa hadi leo."
"Kuangushwa kwa Mossadegh na kuimarishwa kwa utawala wa kifalme kulikuwa muhimu kwa utaifishaji wa Iran, ambao mwishowe ulisababisha mapinduzi ya mwaka 1979 yaliyoanzisha Jamhuri ya Kiislamu."
Baada ya mapinduzi ya 1979, , uhusiano kati ya Marekani na Iran uligeuka kuwa wa adui.