Israel yadai kushambulia 'miundombinu muhimu' ya Tehran
Jeshi la Israel (IDF) linasema limekamilisha "wimbi la mashambulizi dhidi ya maeneo ya miundombinu ya utawala wa kigaidi" mjini Tehran siku ya Ijumaa.
Taarifa mpya ya jeshi inasema ilishambulia eneo la ulinzi wa anga ambapo "makombora yaliyokusudiwa kulenga ndege yalihifadhiwa" pamoja na eneo la kijeshi "linalohusika na kuhifadhi taarifa za kitafiti za utawala".
"Mashambulizi haya yaliyokamilika ni sehemu ya awamu inayoendelea dhidi ya mifumo na misingi muhimu ya utawala wa kigaidi wa Iran," IDF inasema.
Awali iliarifiwa kwamba jeshi la Israel linasitisha kwa muda mashambulizi yake dhidi ya kusini mwa Iran, wakati juhudi za kumtafuta mwanajeshi wa ndege ya kivita ya Marekani aliyepotea zikiendelea.
Wakati huo huo, milipuko mikubwa imesikika mashariki mwa mji wa Tehran, kwa mujibu wa vyanzo viwili, alisema mwandishi mwandamizi wa BBC Persian.
Zaidi ya watu watatu pia wameiambia BBC kwamba wamesikia ndege za kivita zikiruka angani.
Vyombo vya habari vya Iran vimeripoti kuwa mifumo ya ulinzi wa anga imewashwa katika mji huo.