Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Trump aipa Iran saa 48 kufikia makubaliano au kukabiliana na adhabu kali

Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Trump kutoa muda wa aina hiyo wakati wa mvutano unaoendelea. Ametoa matamko kadhaa katika siku za hivi karibuni, yakihusiana na mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati ya Iran.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Martha Saranga

  1. Wabunge wa Cameroon waidhinisha kuundwa kwa nafasi ya makamu wa rais

    Bunge la Cameroon limeidhinisha muswada wa kurejesha wadhifa wa Makamu wa rais, ambao ulifutwa zaidi ya miaka 50 iliyopita, huku seneta mmoja wa chama tawala akielezea mchakato huo kama "wa haraka" na "wa kutiliwa shaka."

    Wakati wa kikao cha leo, wajumbe 200 wa bunge la juu na la chini vilivyotawaliwa na chama tawala cha CPDM cha Biya walipiga kura kuunga mkono marekebisho ya katiba, 18 walipiga kura ya Hapana, wanne hawakupiga kura.

    Kwa mujibu wa muswada huo ambao BBC imeuona, nafasi hiyo ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa uendeshaji wa shughuli za serikali, kuboresha uwakilishi pale ambapo kiongozi anahitajika kumwakilisha Rais nje ya nchi, na pia kupunguza mzigo wa urithi wa uongozi kutoka kwa Seneti ili iweze kuzingatia majukumu yake ya kutunga sheria.

    Kabla ya marekebisho hayo, katiba ilimtaja kiongozi wa Seneti kuwa ndiye anayechukua madaraka kwa muda mfupi iwapo Rais atafariki, ataacha madaraka, au atashindwa kuyatekeleza.

    Muswada uliopitishwa sasa unaeleza kuwa makamu wa rais atateuliwa na kuondolewa na rais, na ndiye atakayemrithi mkuu wa nchi.

    Hata hivyo, akiwa rais wa mpito, hataruhusiwa kurekebisha katiba wala kugombea urais.

    “Katika kusubiri kutiwa saini na rais wa Jamhuri, nafasi ya makamu wa rais sasa imeanzishwa rasmi nchini Cameroon,” alisema Spika wa Bunge la Taifa, Théodore Datouo, baada ya kura hiyo.

    Upinzani umeukosoa muswada huo, ukisema uliwasilishwa bila mashauriano ya kutosha.

    Wabunge wa chama cha Social Democratic Front (SDF) walisusia upigaji kura huo. Walikuwa wamependekeza marekebisho yawe kwa mfumo wa makamu wa rais kuchaguliwa pamoja na rais, badala ya kuteuliwa.

    Unaweza kusoma pia:

  2. Trump aipa Iran saa 48 kufikia makubaliano au kukabiliana na adhabu kali

    Rais wa Marekani, Donald Trump, ameipa Iran muda wa saa 48 kufikia makubaliano au kufungua Mlango wa Bahari wa Hormuz, akionya kuwa “adhabu kali itawakumba” endapo haitafanya hivyo.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa Truth Social, Trump alisema muda unaisha na ndani ya saa 48 hatua kali zitachukuliwa dhidi ya Iran.

    Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Trump kutoa muda wa aina hiyo wakati wa mvutano unaoendelea. Ametoa matamko kadhaa katika siku za hivi karibuni, yakihusiana na mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati ya Iran.

    Mtiririko wa matukio:

    21 Machi 2026: Trump alitishia kushambulia na kuharibu mitambo ya umeme ya Iran iwapo haitafungua Mlango wa Hormuz ndani ya saa 48

    23 Machi 2026: Alisema mazungumzo kati ya pande hizo mbili yalikuwa mazuri, na akaahirisha mashambulizi kwa siku tano

    27 Machi 2026: Alitangaza kusitisha mashambulizi kwa siku 10 kufuatia kile alichosema ni ombi kutoka Iran, na hivyo kusogeza mwisho wa muda hadi Aprili 6

    Leo amerudia msimamo wake wa Machi 27, akisema Iran ina saa 48 kabla ya “kuwashushia adhabu kubwa”

    Katika ujumbe mwingine, Trump pia alisisitiza kuwa Marekani inalenga kuhakikisha Iran haitakuwa na silaha za nyuklia.

  3. Baraza la usalama halitapiga kura leo kuhusu Mlango Bahari wa Hormuz: UN

    Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa halitapiga kura leo kuhusu azimio la Mlango Bahari wa Hormuz kama ilivyotarajiwa afisa wa Umoja wa Mataifa ameithibitishia BBC kwamba haitafanyika kama ilivyopangwa.

    Hakuna tarehe iliyopangwa rasmi kwa ajili ya kura hiyo, kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric.

    Bahrain, ambayo kwa sasa inashikilia urais wa baraza hilo, iliwasilisha azimio hilo.

    Lingeidhinisha nchi wanachama "kutumia njia zote za kujilinda zinazohitajika na zinazolingana na hali" ili kupata njia ya usafiri katika Mlango wa Hormuz kwa angalau miezi sita.

    Jana, msemaji wa Umoja wa Mataifa aliiambia BBC kwamba kura iliyopangwa kufanyika Aprili 3 imeahirishwa hadi leo, Aprili 4, baada ya wanachama kuamua kuahirisha.

    Unaweza kusoma pia:

  4. Mlipuko wa mionzi 'utasababisha maafa' katika nchi za Ghuba, asema waziri wa mambo ya nje wa Iran

    Waziri wa Mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi ametoa maoni kuhusu shambulio lililoripotiwa karibu na kiwanda cha nyuklia cha Bushehr.

    Anaandika kwenye mitandao ya kijamii: "Unakumbuka hasira za Magharibi kuhusu uhasama karibu na Kiwanda cha Nyuklia cha Zaporizhzhia nchini Ukraine? Israel-Marekani wameshambulia kiwanda chetu cha Bushehr mara nne sasa.

    "Mlipuko wa mionzi utakomesha uhai katika miji mikuu ya GCC [Baraza la Ushirikiano la Ghuba], sio Tehran.

    Mashambulizi dhidi ya kemikali zetu za petroli pia yanawasilisha malengo halisi."

    Marekani na Israeli bado hazijathibitisha kwamba zilihusika katika shambulio hilo.

  5. Iran yakanusha ripoti za kukamatwa mwanajeshi wa pili aliyekuwa katika ndege ya Marekani

    Iran imekanusha taarifa zinazoenea kuwa rubani wa pili wa Marekani aliyekuwa kwenye ndege ya kivita aina ya F-15 amekamatwa.

    Maafisa wa jeshi la Iran (IRGC) katika jimbo la kusini la Kohgiluyeh na Boyerahmad, pamoja na gavana wa eneo hilo, wamesema wazi kuwa hakuna tukio la aina hiyo lililotokea.

    Kwa upande mwingine, gavana huyo pia amepinga madai kwamba rubani wa kwanza aliokolewa na majeshi ya Marekani.

    Amesisitiza kuwa taarifa hizo ni sehemu ya propaganda za adui zinazolenga kupotosha umma na kuleta mkanganyiko.

    Licha ya kauli hizo rasmi, baadhi ya vyombo vya habari vinavyohusishwa na serikali ya Iran vimeanza kuhamasisha wananchi kushiriki katika juhudi za kumkamata rubani huyo.

    Vimeripotiwa kutoa wito kwa wananchi kuhakikisha rubani huyo anakamatwa akiwa hai.

    Katika hatua inayozua mjadala, taarifa zimeenea zikieleza kuwepo kwa zawadi nono kwa yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa rubani huyo.

    Kiasi kinachotajwa ni takriban pauni 50,000, sawa na dola 66,100 za Marekani.

    Kiasi hicho cha fedha kimeonekana kuwa kikubwa sana ukilinganisha na wastani wa mishahara ya kila mwezi nchini Iran, ambao unakadiriwa kuwa kati ya pauni 150 hadi 230.

    Hali hii imeibua hisia mseto miongoni mwa wananchi na wachambuzi wa masuala ya kisiasa.

    Unaweza kusoma pia:

  6. Kufuatia kupanda kwa bei ya mafuta, Senegal yapiga marufuku safari za mawaziri

    Serikali ya Senegal imepiga marufuku mawaziri wake kufanya safari za nje ya nchi zisizo za lazima kufuatia kupanda kwa bei ya mafuta duniani kunakosababishwa na mzozo wa Iran, waziri mkuu ametangaza.

    Akizungumza katika mkutano wa vijana siku ya Ijumaa, Ousmane Sonko alisema kuwa gharama ya sasa ya pipa la mafuta inakaribia kuwa mara mbili ya kiwango kilichokuwa kimepangwa kwenye bajeti.

    Sonko ameahirisha pia safari zake binafsi kwenda Niger na Hispania kama sehemu ya hatua hizo za kubana matumizi.

    Aliongeza kuwa waziri wa madini atatangaza hatua zaidi za kupunguza matumizi ya serikali katika wiki ijayo.

    Hatua ya Senegal ni miongoni mwa hatua za hivi karibuni barani Afrika dhidi ya kupanda kwa bei ya mafuta, hali ambayo imesababisha baadhi ya nchi kupunguza tozo za mafuta na kuweka mgao wa umeme.

    Katika hotuba yake kwa vijana, waziri mkuu alisema hataki kuwatisha wala kuwawekea shinikizo, bali anataka kuwapa uelewa kuhusu hali halisi ya dunia ilivyo ngumu kwa sasa.

    Hata hivyo, alisisitiza kuwa licha ya changamoto, wananchi wa Senegal wameendelea kuwa na ustahimilivu mkubwa.

    Licha ya kuwa na sekta changa ya mafuta na gesi, Senegal bado inategemea kwa kiasi kikubwa uagizaji wa mafuta kutoka nje.

    Mwaka uliopita, IMF iliielezea uchumi wa Senegal kuwa imara, ikiwa na ukuaji wa karibu asilimia 8 na mfumuko mdogo wa bei.

    Unaweza kusoma pia:

  7. Shirika la kimataifa la kudhibiti nyuklia latoa wito wa 'kujizuia kijeshi' baada ya shambulio dhidi ya kiwanda cha nyuklia

    Shirika la kimataifa la kudhibiti nishati ya nyuklia linasema limearifiwa kuhusu shambulio hilo karibu na kiwanda cha nyuklia cha Bushehr na limeelezea "wasiwasi mkubwa".

    "Hakuna ongezeko la viwango vya mionzi lililoripotiwa," linaandika kwenye X.

    Shirika hilo pia limesisitiza kuwa maeneo ya vituo vya nyuklia na maeneo ya jirani “hayapaswi kamwe kushambuliwa,” na limetoa wito wa “kiasi cha juu cha kujizuia kijeshi” ili kuepusha ajali ya nyuklia.

    Bushehr ni kiwanda pekee cha nguvu za nyuklia kinachofanya kazi nchini Iran na kilijengwa kwa msaada wa Urusi.

    Naye mkuu wa shirika la nyuklia la Urusi (Rosatom), Alexei Likhachev, alisema siku mbili zilizopita kuwa awamu ya mwisho ya uhamishaji wa takribani watu 200 unapangwa kufanyika wiki ijayo.

  8. Iran: Kiwanda cha nyuklia chashambuliwa mara nne, mmoja auawa

    Taarifa ya Iran inasema kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha tukio hilo "halikusababisha uharibifu" kwa sehemu kuu za kiwanda wala kuathiri uendeshaji wake.

    Hata hivyo, inaonya kuwa kutokana na uwepo wa kiasi kikubwa cha nyenzo za mionzi, uharibifu mkubwa unaweza kusababisha ajali kubwa ya nyuklia.

    Bushehr ni kiwanda pekee cha nguvu za nyuklia kinachofanya kazi nchini Iran na kilijengwa kwa msaada wa Urusi.

    Moscow imewahamisha wafanyakazi wake wengi kutoka kiwandani.

    Mkuu wa shirika la nyuklia la Urusi (Rosatom), Alexei Likhachev, alisema siku mbili zilizopita kuwa awamu ya mwisho ya uhamishaji wa takribani watu 200 unapangwa kufanyika wiki ijayo.

    Mpango wa nyuklia wa Iran kwa muda mrefu umekuwa chanzo cha mvutano wa kimataifa na kusababisha vikwazo vikali.

    Vita kati ya Marekani, Israel na Iran vilianza tarehe 28 Februari, siku mbili baada ya duru ya tatu ya mazungumzo ya nyuklia kati ya Marekani na Iran mjini Geneva.

    Unaweza pia kusoma:

  9. Zelensky: Urusi imechagua 'kuzidisha mashambulizi msimu wa pasaka' badala ya kusitisha mapigano

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameishutumu Moscow kwa kuchagua "kuongeza kasi ya mashambulizi katika msimu wa sikukuu ya pasaka" badala ya kusitisha mapigano baada ya Urusi kutekeleza shambulio jingine kubwa la ndege zisizo na rubani na kombora dhidi ya Ukraine.

    Raia sita waliuawa na wengine 40 kujeruhiwa huku Urusi ikirusha mamia ya ndege zisizo na rubani na makombora kote nchini Ukraine.

    Mashambulizi makubwa ya mchana, ambayo hapo awali yalikuwa nadra, yamekuwa yakiongezeka.

    Hayo yanajiri huku juhudi za kukomesha vita, zikiongozwa na Marekani, zikisimama tangu Rais wa Marekani Donald Trump na timu yake walipoelekeza nguvu zao kwenye mzozo wa Mashariki ya Kati.

    Wakati huo huo, Zelensky alikubaliana na tathmini ya ujasusi ya Uingereza kwamba hali katika mstari wa mbele mashariki ilikuwa "nzuri zaidi" kwa Ukraine katika miezi 10, huku kusonga mbele kwa wanajeshi wa Urusi kukipungua.

    Lakini hakujashuhudiwa usitishaji wa mashambulizi ya anga.

    Katika eneo la Zhytomyr, magharibi mwa mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, waokoaji walilazimika kutafuta manusura chini ya vifusi vya nyumba zao huku safu nzima ya nyumba ikiharibiwa.

    Katika eneo la Kyiv, ndege isiyo na rubani ilirekodiwa ikielekea kwenye jengo la ghorofa, kisha ikagonga ubavu wake, na kusababisha moto.

    Unaweza pia kusoma:

  10. Kikosi cha uokozi nchini Iran chakabiliwa na msako hatari kinapomtafuta mwanajeshi wa Marekani

    Ripoti za awali zinaonyesha kuwa rubani wa ndege ya kivita ya Marekani aina ya F-15 iliyodunguliwa na Iran ameokolewa ikiwa itathibitishwa, tukio hili litaongeza kwenye historia ndefu ya operesheni za uokoaji wa kijeshi za Marekani (combat search and rescue - CSAR) zilizofanywa kwa miongo kadhaa.

    Operesheni ya kumtafuta rubani ambaye ni mwanajeshi wa pili bado inaendelea nchini Iran, kwa mujibu wa shirika la habari CBS, mshirika wa BBC nchini Marekani.

    Operesheni za uokoaji wa kivita (CSAR) huchukuliwa kuwa miongoni mwa shughuli ngumu zaidi na zinazohitaji uharaka mkubwa ambazo majeshi ya Marekani na washirika wake hujiandaa kuzitekeleza.

    Nchini Marekani, vikosi maalum vya jeshi la anga hupatiwa mafunzo ya hali ya juu kwa ajili ya operesheni hizi za CSAR, na mara nyingi hupelekwa mapema karibu na maeneo ya migogoro ambapo kuna uwezekano wa ndege kupotea au kudunguliwa.

  11. Artemis II: Wanaanga waelekea mwezini huku wakipiga picha ya 'kushangaza' ya dunia

    NASA imechapisha picha za kwanza zenye ubora wa hali ya juu za dunia zilizopigwa na wafanyakazi wa misheni ya Artemis II walipofika katikati ya safari kati ya dunia na Mwezi.

    Mkuu wa misheni hiyo, Reid Wiseman, ndiye aliyepiga picha hizo ambazo zimetajwa kuwa za kuvutia sana.

    Picha hizo zilichukuliwa baada ya wafanyakazi kukamilisha mwendo wa mwisho wa injini ulioweka chombo chao kwenye njia sahihi kuelekea Mwezi.

    Kwa mujibu wa taarifa za NASA, chombo cha Orion spacecraft kilikuwa umbali wa maili 142,000 kutoka Dunia na maili 132,000 kutoka mwezini wakati huo.

    Mwanaanga Christina Koch alisema wana anga wote walijawa na furaha kubwa walipojulishwa kufikia hatua hiyo muhimu.

    Hatua hiyo ilifikiwa takriban siku mbili, saa tano na dakika 24 tangu walipoondoka Duniani.

    Picha ya kwanza, iliyopewa jina la “Hello, World,” inaonesha mandhari pana ya bahari ya Atlantiki ikiwa imezungukwa na mwanga wa anga huku dunia ikifunika mwanga wa Jua.

    Pia kuna miale ya kijani inayoonekana katika ncha zote mbili za sayari.

    Unaweza kusoma pia:

  12. Israel yadai kushambulia 'miundombinu muhimu' ya Tehran

    Jeshi la Israel (IDF) linasema limekamilisha "wimbi la mashambulizi dhidi ya maeneo ya miundombinu ya utawala wa kigaidi" mjini Tehran siku ya Ijumaa.

    Taarifa mpya ya jeshi inasema ilishambulia eneo la ulinzi wa anga ambapo "makombora yaliyokusudiwa kulenga ndege yalihifadhiwa" pamoja na eneo la kijeshi "linalohusika na kuhifadhi taarifa za kitafiti za utawala".

    "Mashambulizi haya yaliyokamilika ni sehemu ya awamu inayoendelea dhidi ya mifumo na misingi muhimu ya utawala wa kigaidi wa Iran," IDF inasema.

    Awali iliarifiwa kwamba jeshi la Israel linasitisha kwa muda mashambulizi yake dhidi ya kusini mwa Iran, wakati juhudi za kumtafuta mwanajeshi wa ndege ya kivita ya Marekani aliyepotea zikiendelea.

    Wakati huo huo, milipuko mikubwa imesikika mashariki mwa mji wa Tehran, kwa mujibu wa vyanzo viwili, alisema mwandishi mwandamizi wa BBC Persian.

    Zaidi ya watu watatu pia wameiambia BBC kwamba wamesikia ndege za kivita zikiruka angani.

    Vyombo vya habari vya Iran vimeripoti kuwa mifumo ya ulinzi wa anga imewashwa katika mji huo.

  13. Iran imeangusha ndege vita ya pili ya Marekani

    Iran imethibitisha kuiangusha ndege ya pili ya kivita ya Marekani katika Ghuba ya Uajemi.

    Hata hivyo, vyombo vya habari vya Marekani vinaripoti kuwa ndege ya kivita aina ya A-10 Warthog ililengwa ilipokuwa katika operesheni ya uokoaji wa ndege ya kwanza iliyokuwa imeangushwa.

    Mmoja wa wahudumu wa ndege ya kivita aina ya F-15 iliyodunguliwa ameokolewa, lakini rubani bado hajulikani alipo.

    Ikiwa rubani huyo ambaye ni mwanajeshi atakamatwa na Iran, hali hiyo itaongeza mvutano mkubwa kati ya nchi hizo mbili.

    Vita hii pia imekuwa na ukosoaji mkubwa, ndani ya Marekani na kimataifa, kwamba rais wa Marekani Donald Trump hajatoa sababu thabiti ya kuanzisha vita hiyo, wala hajafanikiwa kufikia lengo lake la kubadilisha uongozi wa Iran.

    Trump amesema kuwa tukio la ndege hiyo kuangushwa halitaathiri mazungumzo na Iran.

    Hata hivyo, hali inaweza kubadilika haraka ikiwa mwanajeshi huyo atakamatwa.

  14. Marekani yamsaka rubani wake baada ya ndege kudunguliwa, Iran yatangaza dau nono

    Ripoti zinaonyesha kuwa Marekani na Iran zinashindana kwa kasi kumtafuta rubani wa pili wa ndege ya kivita ya Marekani iliyodunguliwa katika eneo la kusini mwa Iran.

    Operesheni hiyo imekuwa ya dharura huku pande zote zikijaribu kumfikia mhudumu huyo kabla ya mwingine.

    Hapo awali, uchunguzi wa BBC Verify ulithibitisha video iliyokuwa ikisambaa mtandaoni ikionyesha kile kinachoonekana kuwa ndege ya Marekani ikifuatana na helikopta mbili, zikifanya operesheni ya utafutaji na uokoaji.

    Video hiyo ilithibitishwa kushambuliwa katika jimbo la Khuzestan, karibu na daraja juu ya mto Karun.

    Video hiyo imechunguzwa ili kuthibitisha kuwa ni ya hivi karibuni na pia kuangaliwa kama ina dalili zozote za kutengenezwa kwa teknolojia ya AI, lakini hakuna ushahidi uliopatikana unaoonyesha udanganyifu.

    Hii inaongeza uzito wa taarifa kuwa operesheni hiyo ni halisi.

    Kwa mujibu wa ripoti kutoka Marekani, zikimnukuu maafisa wasiotambulishwa majina, operesheni hiyo imefanikiwa kumwokoa mmoja wa wahudumu wa ndege hiyo, lakini juhudi bado zinaendelea kumtafuta rubani wa pili ambaye hajapatikana.

    Wataalamu wa masuala ya kijeshi wanaeleza kuwa operesheni kama hizi ni hatari sana na zinahitaji kufanyika kwa haraka zaidi.

    James Jeffrey, mwanadiplomasia wa zamani wa Marekani, amesema kuwa hii ni miongoni mwa oparesheni hatari zaidi za kijeshi, kwani hujumuisha helikopta, ndege za kuongeza mafuta angani, na ndege za kulinda eneo hilo.

    Kwa upande mwingine, mhudumu na rubani wa ndege walioanguka huwa wamefunzwa kukabiliana na hali kama hizi.

    Kipaumbele chao kikuu ni kubaki hai na kuepuka kukamatwa, ikiwa ni pamoja na kujificha na kuondoka haraka katika eneo walipoangukia.

    Aidha, hupatiwa mafunzo ya mbinu za kuishi mazingira magumu, ikiwa ni pamoja na jinsi ya kupata chakula na maji au kuhimili bila hivyo kwa muda.

    Hii huwasaidia kuongeza nafasi ya kuokolewa kabla hawajapatikana na maadui.

    Unaweza kusoma pia:

  15. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu za leo.