Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mbegu za kiume zisizo sahihi zilitolewa kwa familia za Uingereza na kliniki za IVF
"Baada ya James kuzaliwa ndipo nilijua kuna tatizo" anasema Laura
Yeye na mpenziwe Beth wana watoto wawili, James akiwa kifungua mimba na kate mdogo wake ambao wote walizaliwa kwa njia ya kupandikiza yai IVF, katika kliniki moja ya Kituruki kaskazini mwa Cyprus.
Wanawake hao wawili walitumia mayai yao na kuchagua mbegu za kiume zenye afya nzuri. Waliiambia Kiliniki hiyo kuwa ni muhimu kuwa mbegu za kiume aina moja itumike kwa watoto hao wawili ili watoto hao wakuwe na ukoo mmoja.
Ila James alipozaliwa wote waliweza kugundua kuwa ana macho mazuri yenye rangi ya kahawia ambayo ni tofauti sana na macho ya mama yao mzazi,Beth na mfadhili aliyetoa mbegu za kiume. Hii ilizua shaka miongoni mwa wazazi hao, "Je kliniki ilifanya makosa?"
Beth na Laura waliamua kuwafanyia watoto wao vipimo vya DNA. Matokeo yalionyesha kuwa hakuna hata mmoja wa watoto hao alikuwa na uhusiano wa damu na mfadhili wa mbegu za kiume waliokuwa wamemchagua . Zaidi ya hayo, ushahidi ulionyesha kuwa watoto hao hawakuwa hata na uhusiano wa damu kati yao.
"Hofu ilikuwa kudhibitisha kwamba kulikuwa na kitu ambacho si sawa, na hilo lingemaanisha nini kwa watoto" anasema Beth.
BBC News imezungumza na familia za watoto saba kwa jumla ambao wanaamini kuwa mbegu za wafadhili wasio sahihi zilitumika katika kurutubisha mayai yao ya uzazi.
Familia nyingi zimefanya vipimo vya DNA ambavyo vimedhibitisha hofu yao.
Kesi zote zinahusisha kliniki ambazo zipo kaskazini mwa Cyprus eneo ambalo sheria za Umoja wa Ulaya hazitumiki na ambalo linatambuliwa kisheria na Uturuki pekee.
Kaskazini mwa Cyprus ni mojawapo ya maeneo maarufu zaidi kwa Waingereza wanaotafuta matibabu ya uzazi nje ya nchi. Kliniki za eneo hilo zinasimamiwa kwa uangalizi hafifu na hutoa matibabu ya gharama nafuu.
Eneo la Cyprus linajivunia kuwa na wigo mpana wa wafadhili wa mayai na mbegu za kiume wasiojulikana kutoka kote duniani, jambo linalowavutia zaidi watu wenye changamoto za uzazi, wale kutoka jamii ya LGBTQ au watu wazima wasio na wenza ambao huenda wasiweze kupata matibabu kama hayo katika nchi zao.
Kliniki za kaskazini mwa Cyprus pia hutoa taratibu ambazo ni kinyume cha sheria nchini Uingereza, kama vile kuchagua jinsia ya mtoto. Wizara ya Afya ya eneo hilo ndiyo inayosimamia kliniki za uzazi, lakini haijajibu maswali yetu licha ya kutuma maombi mara kadhaa.
"Tulidhani tulikuwa tumeagiza mbegu za kiume kutoka Denmark"
Kujenga uaminifu na familia zote katika uchunguzi huu kulichukua miezi kadhaa.
Tulifanya kazi kwa karibu na Beth, Laura, Kate na James ili kuhakikisha walikuwa tayari kutupa simulizi zao.
Beth na Laura walituambia kuwa waliamua kuanza familia mwaka 2011.
Walichagua kituo cha Dogus IVF kilichopo kaskazini mwa Cyprus. Mratibu wa wagonjwa wa kituo hicho wakati huo, Julie Hodson, aliwaambia kuwa kliniki hiyo ingeweza kuagiza mbegu za kiume zilizogandishwa kutoka benki kubwa zaidi ya mbegu za kiume duniani, Cryos International, iliyoko Denmark.
Wawili hao wanasema walivutiwa na wigo wa wafadhili wasiojulikana ambao walikuwa wamefanyiwa "uchunguzi wa kina wa afya" pamoja na tathmini za kisaikolojia.
Walivutiwa na wasifu wa mfadhili aliyejulikana kama "Finn" raia wa Denmark ambaye alijieleza kuwa mtu mwenye afya njema na anayefanya mazoezi, na hunywa pombe mara chache tu na havuti sigara kabisa.
Finn aliwaambia kuwa motisha yake ya kutoa mbegu za kiume ilikuwa "kuleta maisha na furaha kwa wengine".
Beth na Laura walitumai kuwa wasifu huo ungewapa watoto wao wa baadaye faraja wakikuwa wakubwa. "Tulihisi ilikuwa muhimu sana kwa watoto wetu kuwa na angalau ufahamu fulani kuhusu mfadhili wao" alisema Beth.
Finn na jamaa zake walikuwa na sifa za kimwili zinazofanana na wanandoa hao wa Uingereza macho "mepesi" na nywele za kahawia, ambayo ipo kwenye ukoo wao.
"Tulimuuliza mratibu wetu, Julie, ni nini tulihitaji kufanya ili kuagiza mbegu za kiume za Finn," anakumbuka Laura. "Naye akasema: 'Dkt. Firdevs ataagiza kwa niaba yenu.' Hapo ndipo mazungumzo hayo yaliishia."
wawili hao wanasema matibabu yao ya IVF katika kituo cha Dogus yalifanywa na Dkt. Firdevs Uguz Tip , ambaye wanamwelezea yeye na timu yake kuwa "watu wazuri."
Miezi tisa baadaye, Laura alijifungua mtoto wao wa kwanza, Kate.
Wakati wapenzi hao walipotaka mtoto wa pili, walirudi kwa kliniki ile ile ya IVF na kuuliza kama wangeweza kutumia tena mfadhili Finn kupata mtoto wa pili.
Hodson alithibitisha kupitia barua pepe kwamba Firdevs angeagiza tena mbegu za kiume.
Safari hii, Beth ndiye aliye jifungua mtoto wao, James.
Matibabu yao ya uzazi kaskazini mwa Cyprus ikiwa ni pamoja na dawa, hoteli na safari za ndege yaligharimu takriban pauni 16,000 kwa jumla, huku mbegu za kiume za Finn zikigharimu pauni 2,000.
Beth na Laura wanasema walikuwa wazi kwa watoto wao kuhusu mwanaume waliyedhani ndiye alikuwa mfadhili wa mbegu za kiume. "Wote wawili walikuwa wakijieleza kama 'wana vinasaba vya Denmark'," anasema Laura.
Lakini macho ya rangi ya kahawia, nywele nyeusi na rangi ya ngozi ya James yaliwafanya wazazi wake kutilia shaka kwamba mfadhili wao hakuwa Finn na baada ya miaka ya kutafakari, Beth na Laura waliamua watoto wote wawili wafanyiwe vipimo vya DNA.
Matokeo yalionyesha kuwa hakuna hata mmoja wa watoto hao aliyekuwa na jeni za mbegu za kiume za Finn. Pia matokeo yalionyesha kuwa watoto hao walitokana na wafadhili tofauti wa mbegu za kiume na hawakuwa na uhusiano wa damu kati yao.
Matokeo hayo yaliwaacha wazazi hao wakiwa "wameghadhabishwa sana" wakibaki na maswali mengi yasiyo na majibu. Wafadhili hao walikuwa kina nani, na je, kulikuwa na uchunguzi wowote wa afya uliofanywa?
Beth na Laura walijaribu kuwasiliana na Firdevs na Hodson lakini hakuna hata mmoja wao aliyejibu.
BBC imechukua miezi kadhaa kujaribu kubaini kilichotokea kwa Beth na Laura.
Katika harakati za uchunguzi wetu, tulipata familia nyingine mbili za Waingereza ambazo pia zilitibiwa na Firdevs na zilikuwa na shaka kwamba wafadhili wasio sahihi walitumika wakati wa matibabu yao ya IVF.
Wao pia wamekamilisha vipimo vya DNA ambavyo vilidhibitisha shaka yao.
Beth na Laura wanashauku iwapo kliniki yao iliagiza mbegu za kiume za mfadhili Finn.
Wakati tulipo wasiliana na Firdevs, alisema kuwa hakuwa na haja ya kuagiza mbegu za kiume kutoka Dogus na kwamba hakuna taarifa yoyote kuhusu ombi la mfadhili Finn .
Daktari huyo pia alitilia shaka juu ya uhalali wa vipimo vya DNA vya Beth na Laura. Anasema haiwezekani kujua "kwa hakika" kuwa mfadhili aliyetumiwa si sahihi.
Firdevs pia ameiambia BBC kuwa "hakufanya matibabu ya IVF" kati ya mwaka 2011 na 2014, wakati Beth na Laura walikuwa wanapokea matibabu hayo, licha ya kwamba ya kuwepo na maelezo ya kina kwenye tovuti ya Dogus kuhusu taratibu alizotoa wakati huo.
Kliniki ya Dogus, ambayo Firdevs anasema ilikuwa inajukumika na matibabu ya Beth na Laura, haijajibu ombi letu la kutaka majibu kuhusu madai haya dhidi yao.
Ifikiapo mwaka 2015, Firdevs na Hodson walikuwa wameondoka Dogus na walikuwa wakifanya kazi pamoja katika kliniki nyingine kaskazini mwa Cyprus.
Beth, Laura na watoto wao sasa wamefanya vipimo zaidi vya DNA vinavyotambulika na vinavyoweza kutumika katika mahakama za Uingereza. Vipimo hivi vimethibitisha kuwa James na Kate hawana uhusiano wa damu na hawakuzaliwa na mfadhili mmoja wa mbegu za kiume.
Mtaalamu maarufu wa jenetiki ya kisheria, ambaye amechambua vipimo vyote vya familia hiyo, alituambia kuwa ni jambo lisilo la kawaida mtoto yeyote asiwe na uhusiano wa damu na mfadhili wa mbegu za kiume, kwa muktdha huu Finn.
Tulizungumza na Cryos International, benki ya mbegu za kiume iliyoko Denmark, ambapo Beth na Laura, pamoja na familia nyingine katika uchunguzi wetu, walidhani mbegu za kiume zilikuwa zimeagizwa kutoka huko.
"Tuna taratibu nyingi za usalama, lakini haziwezi kukupa 100%." anasema Ole Schou, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo. Hata hivyo, alisema kwamba kosa kama hili halijawahi kutokea katika historia ya Cryos ya miaka 45.
Wataalamu mbalimbali wa uzazi kutoka Ulaya wote waliiambia BBC kuwa uwezekano wa mfadhili asiye sahihi kutumika kwa bahati mbaya wakati wa taratibu ya IVF ni nadra.
Hata hivyo, kwa kosa lenye ukubwa huu kutokea mara zaidi ya moja likihusisha timu hiyo hiyo ya matibabu, linaweza kuashiria "kutokujali" au hata "udanganyifu," wataalamu walisema.
"Ni hali mbaya kabisa kwa wagonjwa kujipata ndani yake," anasema Dkt. Ippokratis Sarris kutoka British Fertility Society . "Sijawahi kusikia tukio kama hili nchini Uingereza. Ni hatari kubwa zaidi kwa kituo chochote cha IVF kuchanganya mayai, mbegu za kiume au viini."
Cyprus ina sheria zake za uzazi, lakini, tofauti na Uingereza, haina mdhibiti huru wa kliniki za uzazi, kudumisha viwango na, ikiwa ni lazima, kunyanganya leseni.
"Bado sisi ni familia"
Imekuwa miaka miwili tangu Beth na Laura wazungumze na watoto wao kuhusu jinsi Finn huenda asikuwa mfadhili wao.
Watoto sasa wanajua hawana uhusiano wa damu, lakini jambo hilo halijabadilisha upendo waliokuwa nao kwa kila mmoja.
"Tumewalea wote pamoja jinsi mamangu alitulea," anasema Kate. "Bado sisi ni familia hata kama si kwa damu."