Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Pakistan imewezaje kuwa mpatanishi wa vita vya Trump na Iran?
- Author, Caroline Davies
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Jukumu la Pakistan kama mpatanishi katika mzozo huu liliwashangaza wengi.
Mkuu wa majeshi wa Pakistani, Field Marshal Asim Munir, ana usuhuba na Rais wa Marekani Donald Trump. Kiongozi huyo wa Marekani mara nyingi humtaja kama Field Marshal "anayempenda" na hapo awali amezungumzia Munir anavyoijua Iran "vizuri zaidi kuliko wengi."
Iran si tu kwamba ni jirani wa Pakistan, ambayo inapakana nayo katika mpaka wa kilomita 900 (maili 559) au zaidi, lakini pia ina uhusiano wa "kindugu" na uhusiano wa kitamaduni na kidini.
Pia haina kambi za anga za Marekani. Na tofauti na wapatanishi wengi wa Ghuba bado Pakistan haijaingizwa kwenye mzozo huo. Muhimu zaidi, iko tayari kuingilia kati - amani kati ya Marekani na Iran itakuwa na manufaa yake.
Hata hivyo, kumekuwa na maswali kuhusu jinsi nchi iliyoingia katika mgogoro na majirani zake wawili - Afghanistan na India - imejiweka kama mleta amani.
Kwa sasa nchi hiyo inaishambulia Afghanistan kwa mabomu na mvutano na India ulisababisha hofu ya matumizi ya silaha za nyuklia mwaka jana pekee.
Hadi sasa Pakistan imejiweka katikati kati ya Iran na Marekani, ikipeleka ujumbe kati ya pande hizo mbili, ikiwakaribisha mawaziri wa mambo ya nje kutoka mataifa mengine ya Kiislamu na kupiga simu za kidiplomasia.
Pakistan ina ya kupoteza
Pakistan inategemea sana mafuta yanayoagizwa kutoka nje, mengi yakipitia Mlango-Bahari wa Hormuz.
Serikali ya Pakistani iliongeza bei ya petroli na dizeli kwa karibu 20% mwanzoni mwa Machi na tayari imeanzisha hatua ikiwemo wiki ya kazi ya siku nne kwa wafanyakazi wa serikali ili kujaribu kuokoa mafuta.
"Ikiwa vita vitaendelea, shinikizo la kiuchumi nchini Pakistani litaongezeka sana," anasema Farhan Siddiqi, Profesa wa Sayansi ya Siasa katika Taasisi ya Utawala na Biashara, Karachi.
Pia kuna hofu nyingine: Septemba mwaka jana, Pakistan ilisaini mkataba wa ulinzi na Saudi Arabia, kwamba "uchokozi wowote dhidi ya nchi kati ya hizo, utachukuliwa kama uchokozi dhidi ya zote mbili".
Kuna maswali kuhusu kile ambacho Pakistan itakifanya ikiwa Saudi Arabia itajiunga na vita na kuidhinisha makubaliano hayo.
"Shida kwetu ni kwamba tukiombwa kujiunga na vita upande wa Saudi Arabia, mpaka wetu wote wa Magharibi utakuwa hauna usalama kwa kiasi kikubwa," anasema Siddiqi.
Pakistan tayari iko katika na Afghanistan; inawashutumu Taliban wa Afghanistan kwa kuwa na makundi ya kigaidi ndani ya mipaka yake, jambo ambalo serikali ya Taliban inakanusha.
Siddiqi anasema kufungua uwanja mwingine wa vita sio wasiwasi pekee ambao Pakistan inao, pia kuna "gharama ya sifa yake ya ndani."
Katika siku chache baada ya Kiongozi Mkuu wa Iran kuuawa katika shambulio la anga la Marekani na Israel, waandamanaji wanaounga mkono Iran waliandamana mitaani kote Pakistan - kadhaa waliuawa wakiwemo wale waliojaribu kuvamia ubalozi mdogo wa Marekani huko Karachi.
"Hisia za umma nchini Pakistan zinaunga mkono Iran kwa kiasi kikubwa," anasema Maleeha Lodhi, balozi wa zamani wa Pakistan nchini Marekani, Uingereza na Umoja wa Mataifa.
"Nina uhakika kwamba watunga maamuzi wa Pakistan wanaelewa hilo vyema."
Je, ikishindwa?
Na kisha kuna suala la hadhi ya Pakistan duniani.
"Hii ni diplomasia yenye umuhimu mkubwa," anasema Lodhi. "Ina hatari kubwa na ina thawabu kubwa. Ikiwa itafanikiwa, itaipeleka Pakistan kileleni mwa mchezo wa kidiplomasia duniani."
Lakini ikishindwa "Pakistan bado itaonekana kuwa imefanya juhudi nzuri.”
Haijulikani jinsi mambo yatakavyokuwa, lakini kilicho wazi ni kwamba Pakistan imekuwa na haraka ya kutumia uhusiano wake na Trump.
Lodhi anasema Pakistan imewahi kumpendekeza Trump apewe Tuzo ya Amani ya Nobel "kwa kutambua uingiliaji wake wa kidiplomasia" wakati wa mzozo wa Pakistan na India mwaka 2025.
Pia Kabul imempeleka Marekani mwanaume aliyeshitakiwa kwa kupanga shambulio la bomu katika uwanja wa ndege wa Kabul wakati wa kujiondoa kwa Marekani nchini Afghanistan.
"Pakistan ilimpongeza Trump mapema katika ushindi mara mbili wa kiti cha urais, jambo ambalo ni muhimu sana kwake. Hilo liliimarisha uhusiano," anasema Lodhi.
"Ukweli kwamba viongozi wakuu wa Pakistan wamejitahidi sana kumsifu rais, hilo limesaidia sana huko Washington na limeifanya Pakistan kuwa mpatanishi anayevutia zaidi machoni pa utawala."
Kuna zaidi ya hilo
"Nadhani sababu ya Pakistan kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuzungumza na Iran ni kwa sababu haina mtazamo mzuri juu ya Israel au hata kuwa upande wa Marekani kupita kiasi."
Wakati mikutano ya kidiplomasia inaendelea, Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan Ishaq Dar anasafiri kwenda China Jumanne kwa mwaliko wa mwenzake wa China, Wang Yi.
"Tuwe wa kweli, uwezekano wa makubaliano si mkubwa sana kutokana na hali ya kutoaminiana kati ya Wamarekani na Wairani na jinsi matakwa yalivyo makubwa kwa upande wa Marekani na Iran," anasema Michael Kugelman, mtafiti wa masuala ya Kusini mwa Asia katika Taasisi ya Atlantic Council.
"Nadhani hilo ndio jambo gumu zaidi, na Pakistan italazimika kuufikiria upya ikiwa mipango yake haitafanikiwa."