Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waasi wa Houthi kujiunga vita ya Iran ina maana gani kwa dunia?
Kujiunga kwa waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran katika vita vinavyoendelea kati ya Iran, Israel na Marekani kunaashiria hatua mpya hatari katika mzozo wa Mashariki ya Kati, huku vita hivyo vilivyoanza Februari 28 sasa vikiingia mwezi wa pili.
Hatua hiyo inaongeza hofu ya vita kupanuka zaidi, wakati tayari madhara makubwa yameripotiwa, ikiwemo vifo vya viongozi wa ngazi za juu na kuongezeka kwa mashambulizi katika nchi kadhaa za ukanda huo.
Houthi wamethibitisha kurusha makombora ya masafa marefu ya balistiki kulenga maeneo ya kijeshi ya Israel, ikiwa ni mara yao ya kwanza kushiriki moja kwa moja katika vita hii mpya. Wamesema mashambulizi hayo ni sehemu ya kujibu hatua dhidi ya Iran na washirika wake, na kuonya kuwa wataendelea hadi kile wanachokiita "uchokozi" kitakapotamatika.
Kujiunga kwao kunakuja wakati Iran yenyewe imepata pigo kubwa kufuatia vifo vya baadhi ya viongozi wake wakuu katika mashambulizi ya hivi karibuni, hali inayoongeza uwezekano wa hatua za kulipiza kisasi na kuifanya vita kuwa ngumu zaidi kuidhibiti.
Mashambulizi yaongezeka zaidi Mashariki ya Kati
Katika siku za karibuni, mashambulizi yameripotiwa katika maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati, ikiwemo Iran, Israel na nchi za Ghuba, hali inayoonyesha wazi kuwa vita hii haiko tena katika mipaka ya nchi chache bali imeanza kuwa ya kikanda.
Wachambuzi wanaonya kuwa hatua ya Houthi inaweza kuwa mwanzo wa ushiriki mkubwa zaidi wa makundi mengine yanayoungwa mkono na Iran katika eneo hilo.
Athari za vita hii tayari zinaonekana katika uchumi wa dunia, hasa katika sekta ya nishati.
Wasiwasi umeongezeka juu ya usalama wa njia muhimu za usafirishaji wa mafuta, huku nchi zikianza kuchukua tahadhari dhidi ya uwezekano wa kuvurugika kwa usambazaji wa mafuta katika masoko ya kimataifa.
Marekani inayoshirikiana na Israel kuendesha operesheni za kijeshi eneo hilo, inaeleza kuwa operesheni hizo zinaweza kumalizika ndani ya wiki chache zijazo.
Houthi ni kina nani na kwa nini hatua yao ni muhimu?
Waasi wa Houthi kutoka Yemen ni miongoni mwa washirika wakuu wa Iran katika ukanda wa Mashariki ya Kati, na kwa muda mrefu wamekuwa wakijihusisha na mashambulizi ya hapa na pale dhidi ya Israel tangu vita vya Gaza vilipoanza Oktoba 2023.
Hata hivyo, mashambulizi hayo yalikuwa ya nadra na kwa kiasi kikubwa hayakusababisha madhara makubwa. Tukio la Julai 2024, ambapo raia mmoja wa Israel aliuawa baada ya kushambuliwa na drone lilionyesha uwezo wao lakini halikubadilisha mwelekeo wa mzozo kwa kiasi kikubwa.
Tofauti na hapo awali, kujiunga kwao katika vita hii mpya kunakuja katika mazingira ya mvutano mkubwa zaidi kati ya Iran, Israel na Marekani, jambo linaloongeza uzito wa hatua yao.
Kati ya Novemba 2023 hadi mapema 2025, Houthi walifanya karibu mashambulizi 200 dhidi ya meli katika Bahari ya Shamu, wakaharibu zaidi ya meli 30 na kupunguza kwa kiasi kikubwa usafiri kupitia njia muhimu kama Bab al-Mandab na Mfereji wa Suez.
Ikiwa hali hiyo itajirudia, athari zake kwa biashara ya dunia zinaweza kuwa kubwa zaidi, hasa endapo pia njia ya Hormuz itaathirika.
Kwa ujumla, kujiunga kwa Houthi katika vita hii ya sasa kunaongeza hatari ya mgogoro mpana zaidi wa kikanda, huku dunia ikifuatilia kwa karibu iwapo hali hiyo itazidi kuwa mbaya katika wiki zijazo.
Imeandaliwa kwa msaada wa taarifa kutoka kwa Paul Adams, Mwandishi wa Diplomasia