Waandishi wa habari watatu wauawa katika shambulio la Israel nchini Lebanon
Waandishi wa habari watatu wa Lebanon wameripotiwa kuuawa baada ya gari lao la kazi kushambuliwa na ndege ya Israel kusini mwa nchi hiyo, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani.
Waliofariki ni pamoja na mwandishi wa Al Manar TV, Ali Shoeib, pamoja na wanahabari wa Al Mayadin, Fatima na Mohamed Fetoni, ambao waliuawa katika shambulio la anga katika mji wa Jezzine.
Rais wa Lebanon, Joseph Aoun, amelilaani shambulio hilo akilitaja kuwa “uhalifu wa wazi” unaokiuka sheria za kimataifa, ambazo zinataka wanahabari kulindwa wakati wa vita.
Jeshi la Israel limethibitisha kumuua Ali Shoeib katika shambulio hilo, lakini limedai kuwa alikuwa mshirika wa Hezbollah akijifanya mwandishi wa habari.
Hili ni tukio la pili ndani ya muda mfupi ambapo Israel imetuhumiwa kulenga wanahabari nchini Lebanon tangu vita kuanza. Wiki iliyopita, mtangazaji maarufu wa Al Manar, Mohammad Sherri, na mkewe waliuawa katika shambulio lingine lililolengwa.
Tangu kuanza kwa mashambulizi hayo, zaidi ya raia 1,100 wameuawa nchini Lebanon, wakiwemo watoto 120 na wahudumu wa afya 42. Wengi nchini humo wanaeleza wasiwasi kuwa Israel inatumia mbinu zinazofanana na zile ilizotuhumiwa kutumia Gaza, ikiwa ni pamoja na kulenga raia, wanahabari na wahudumu wa afya, madai ambayo Israel imekuwa ikiyakanusha.