Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Trump aongeza muda wa kusitisha mashambulizi kwa siku 10 na kusema 'mazungumzo yanaendelea'
Rais wa Marekani amekuwa akisema kwa siku kadhaa kwamba mazungumzo kati ya Marekani na Iran yanaendelea, lakini Iran imekanusha kuendelea kwa hatua hiyo.
Muhtasari
- Mashambulizi yafanyika usiku kucha kote Mashariki ya Kati
- Marekani inajiandaa kwa 'shambulizi kubwa la mwisho' katika vita vya Iran
- Meli mbili za misaada zinazoelekea Cuba hazijulikani zilipo baada ya kuondoka Mexico
- Saini ya Trump kuonekana kwenye noti ya dola za Marekani
- Urusi na Ukraine zadai kuteka vijiji vilivyokumbwa na vita
- Zelensky yuko Saudi Arabia, Ukraine inawapa utaalamu wa droni
- IDF yasema imeshambulia miundombinu mjini Tehran
- Trump aongeza muda wa kusitisha mashambulizi kwa siku 10
Moja kwa moja
Na Asha Juma & Mariam Mjahid
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aishutumu Marekani na Israel kwa kulenga maeneo ya raia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, ameishutumu Marekani na Israel kwa “kuendelea na mashambulizi haramu” dhidi ya “malengo na maeneo ya raia,” ikiwemo shule, hospitali, majengo ya kihistoria na kitamaduni pamoja na makazi ya watu, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Iran.
Ameongeza kuwa nchi hiyo itaendelea kwa uthabiti “kuilinda taifa la Iran.”
Katika chapisho kwenye mtandao wa Telegram, shirika la habari la IRNA linalohusishwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran pia limesema Araghchi alijadili vita hivyo katika mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov.
Kwa mujibu wa IRNA, Araghchi alisema ukosefu wa usalama katika Mlango-Bahari wa Hormuz ni matokeo ya hatua za kijeshi za Marekani na Israel, na kwamba Iran ina haki ya kisheria kuzuia kupita kwa meli katika mlango huo.
pia unaweza kusoma:
Umoja wa taifa wasema shambulizi dhidi ya shule Iran ulisababisha ‘hofu kubwa’
Mkuu wa Shirika la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Volker Türk, ametaka uchunguzi kuhusu mashambulizi dhidi ya shule ya msingi katika mji wa Minab, kusini mwa Iran, uliofanyika mwanzoni mwa vita kukamilika “haraka iwezekanavyo,” akiongeza kuwa ulisababisha “hofu kubwa ya ndani.”
Mama wa watoto wawili waliouawa katika shambulizi hilo aliwaambia UN kuwa nyumba yake sasa iko, “kimya kuliko nyumba yoyote inavyopaswa kuwa.”
Pia alisema mashambulizi ya Marekani na Israel yamekuwa yakiharibu zaidi “miundombinu ya raia” kadri vita inavyoendelea, na akaita kulengwa kwa vituo vya nyuklia kuwa “hatari isiyoelezeka kwa uzito wake.”
Mamlaka za Iran zinasema watu 168 waliuawa, wengi wao wakiwa watoto.
Hatujasikia upande wa Marekani katika mjadala huo. Haijakubali kuwajibika kwa shambulizi hilo na imesema hailengi raia na hapo awali ilisema inachunguza tukio hilo.
Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa wachunguzi wa kijeshi wa Marekani wanaamini vikosi vya Marekani huenda vilihusika kwa bahati mbaya kupiga shule hiyo, lakini bado hawajafikia hitimisho la mwisho.
Watu 1,900 wameuawa nchini Iran tangu kuanza kwa vita
Afisa wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu alisema Ijumaa kuwa, kwa kuzingatia takwimu zilizotolewa na Hilali Nyekundu ya Iran, zaidi ya watu 1,900 wameuawa na takriban 20,000 wamejeruhiwa nchini Iran tangu kuanza kwa mashambulizi ya Marekani na Israel.
Kwa mujibu wa BBC Arabic, Maria Martinez anasema kuwa Shirika la Hilali Nyekundu la Iran ndilo shirika pekee la misaada la kitaifa ambalo linaendelea kufanya kazi kote nchini huku kukiwa na mzozo unaoongezeka.
pia unaweza kusoma:
Austria yapiga marufuku matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto chini ya miaka 14
Austria imekuwa nchi ya hivi karibuni katika Umoja wa Ulaya kupiga marufuku matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto walio chini ya miaka 14.
Hatua hiyo ilikuja baada ya mazungumzo ya muda mrefu ndani ya muungano wa serikali tawala.
Naibu kiongozi wa nchi hiyo, Andreas Babler, alisema ni vigumu kwa wazazi kuwalea watoto wao katika jamii hii, ambayo alisema imeundwa kwa makusudi kuwafanya wawe tegemezi.
Soma zaidi:
Kiongozi wa upinzani Israel atoa wito Wayahudi wa dhehebu la Orthodox wasajiliwe jeshini
Nchini Israel, kiongozi wa upinzani Yair Lapid ameishutumu serikali kwa kuwatuma wanajeshi wachache sana vitani bila kuwepo kwa mkakati wowote.
Katika taarifa yake ya video kwa lugha ya Kiebrania, Yair Lapid alidai kuwa “jeshi la Israel limefikia uwezo wake wa juu kabisa na serikali inaacha wanajeshi wakimwaga damu katika uwanja wa vita.”
Aliongeza kuwa serikali “inatuma wanajeshi wachache sana katika vita vikubwa bila mkakati na bila rasilimali za kutosha. Wanajeshi wa akiba wamechoka na hawawezi tena kukabiliana na changamoto za kiusalama.”
Yair Lapid alitoa wito kwa serikali pia kuwaandikisha jeshini Wayahudi wa dhehebu la Ultra-Orthodox (Haredi). Kundi hili la Wayahudi linajulikana kuwa la kidini zaidi na limekuwa likisamehewa kufanya huduma ya lazima ya kijeshi tangu mwaka 1948.
Kauli ya Yair Lapid imekuja wakati ambapo, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Israel, Mkuu wa Majeshi, Jenerali Eyal Zamir, alionya kuwa “jeshi la Israel liko karibu na kuporomoka.”
Soma zaidi:
Israel yadai kulenga mifumo ya ulinzi wa anga na mitambo ya makombora nchini Iran
Israel imedai kulenga mifumo ya ulinzi wa anga na mitambo ya makombora katika maeneo mbalimbali nchini Iran.
Kwa mujibu wa jeshi la Israel, maeneo yaliyopo Tehran yaliyokuwa kituo cha utengenezaji wa makombora ya masafa marefu (ballistic) na silaha nyingine yalilengwa kati ya Alhamisi na usiku wa Ijumaa.
Jeshi hilo pia linadai kuwa jeshi la anga la Israel lililenga vizindua makombora na maeneo ya kuhifadhi makombora katika magharibi ya Iran.
Kwa upande mwingine, Kuwait imesema bandari yake kuu ya kibiashara imeshambuliwa na droni za “adui.”
Katika taarifa, Mamlaka ya Bandari za Kuwait ilisema kuwa Bandari ya Shuwaikh iliharibiwa, lakini hakukuwa na taarifa za majeruhi.
Pia unaweza kusoma:
Marekani ilirusha mamia ya makombora ya Tomahawk dhidi ya Iran - Washington Post
Gazeti la Washington Post liliripoti siku ya Ijumaa, likinukuu vyanzo ambavyo havikutajwa jina, kwamba jeshi la Marekani limerusha zaidi ya makombora 850 ya kusafiri ya Tomahawk wakati wa vita vya wiki nne na Iran.
Ripoti hiyo ilisema kuwa utumiaji wa makombora hayo ambayo hulenga kwa usahihi shabaha zinazopigwa, ulikuwa wa kiwango cha juu, jambo ambalo lilizua wasiwasi miongoni mwa baadhi ya maafisa wa Pentagon na kusababisha mijadala ya ndani kuhusu jinsi ya kuongeza idadi ya silaha hizo.
Shirika la habari la Reuters lilisema bado halijaweza kuthibitisha ripoti ya gazeti hilo, huku Wizara ya Ulinzi ya Marekani na Ikulu ya Marekani hazikujibu ombi la Reuters la kutoa maoni yao.
Soma zaidi:
Je, ‘zawadi’ ya ‘meli 10 za mafuta’ zimepitia Mlango-Bahari wa Hormuz kama anavyodai Rais Trump?
Rais wa Marekani Donald Trump alidai katika kikao cha baraza la mawaziri Alhamisi kwamba Iran iliruhusu meli 10 za mafuta kupita katika Mlango-Bahari wa Hormuz kama ishara ya nia njema.
Rais Trump alisema kuwa Iran iliruhusu meli hizo 10 kupita katika Mlango-Bahari wa Hormuz kama “zawadi” kuonyesha kuwa inachukulia mazungumzo kwa uzito.
Rais huyo wa Marekani alisema kuwa “meli nane za mafuta zilizojaa mafuta zilipita (katika Mlango-Bahari wa Hormuz).”
“Niliwaza kwamba (meli hizi) zilikuwa zinabeba bendera za Pakistan. Nikasema tunazungumza na watu sahihi.”
Kisha rais wa Marekani alidai kuwa Iran iliomba radhi kwa jambo fulani ililosema hapo awali na kusema, “Tunatuma meli nyingine mbili (za mafuta) na hivyo jumla ya meli hizo imefikia 10.”
BBC Verify ilitumia data za umma za ufuatiliaji wa meli kujaribu kubaini ni meli zipi zilipita katika Mlango-Bahari huo zikiwa na vifaa vyao vya kutuma taarifa za mahali zilipo kati ya tarehe 23 na 25 Machi. Kwa mujibu wa Rais Trump, meli hizo zilipita katika kipindi hicho.
Meli tano zilizokuwa zikisafirisha mafuta kupitia Mlango-Bahari huo zilitambuliwa katika kipindi hicho, lakini hakuna iliyokuwa ikipeperusha bendera ya Pakistan. Hakuna hata moja ya meli nyingine tano zilizopita katika Mlango-Bahari wa Hormuz iliyoorodheshwa kama meli ya mafuta.
Wachunguzi wa ufuatiliaji wa meli huenda wasiwe na taarifa kuhusu meli zinazozima kwa muda mitambo yao ya GPS wakati zinapopita katika mlango huo.
Soma zaidi:
Iran yadai kuzirudisha nyuma meli tatu za mizigo zilizojaribu kupita Mlango-Bahari wa Hormuz
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) limeeleza kuwa limezirudisha nyuma meli tatu zilizokuwa zikijaribu kupita Mlango-Bahari wa Hormuz asubuhi ya leo.
IRGC ilisema katika taarifa kwamba meli tatu za mizigo kutoka nchi tofauti zilijaribu kuelekea kwenye korido hiyo. “Zilirudishwa nyuma baada ya kuonywa na Jeshi la Wanamaji la Walinzi wa Mapinduzi,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa “Mlango-Bahari wa Hormuz umefungwa na jaribio lolote la kupita litakabiliwa na jibu kali.”
“Chombo chochote kinachotoka au kuelekea katika bandari za washirika na wanaounga mkono Marekani na Israel hakiruhusiwi kupita kwenye korido hiyo.”
Siku mbili zilizopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, alisema katika televisheni ya taifa kuwa Iran hadi sasa imekubali maombi ya kupita kutoka kwa meli za nchi kama “China, Urusi, Pakistan, Iraq na India.” Alisema kuwa kwa mtazamo wa Iran, Mlango-Bahari wa Hormuz “haujafungwa kabisa, bali umefungwa kwa maadui pekee.”
Ikumbukwe kwamba jana, Rais wa Marekani Donald Trump alidai kuwa Iran iliruhusu meli 10 za mafuta kupita katika Mlango-Bahari wa Hormuz kama ishara ya nia njema.
Pia unaweza kusoma:
Iran yashauri watu wa Mashariki ya Kati kuondoka maeneo yaliyo karibu na vikosi vya Marekani
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) limewaonya watu katika eneo hilo kuondoka katika maeneo ambako kuna vikosi vya Marekani.
Katika taarifa iliyochapishwa na shirika la habari la Fars linalohusishwa na IRGC, walinzi hao wameishutumu Marekani na Israel kwa “kutumia maeneo ya raia na watu wasio na hatia kama ngao za binadamu.”
Taarifa hiyo pia imeishutumu Marekani kwa kuwaua raia na maafisa wa Iran.
Ikumbukwe kwamba IRGC imetoa onyo kadhaa kama hizi tangu kuanza kwa vita. Hapo awali, tarehe 14 Machi, IRGC iliwashauri wakazi wanaoishi karibu na maeneo ya viwanda vya Marekani katika Mashariki ya Kati kuhama.
Hata hivyo, katika onyo hili la hivi karibuni, mamlaka za Iran hazikutaja eneo maalum na inaonekana kuwa ni onyo la jumla.
Makamanda kadhaa wakuu wa IRGC wameuawa katika vita vinavyoendelea.
Iran haijatoa takwimu zozote za vifo katika siku za hivi karibuni.
Shirika la kutetea haki za kibinadamu Human Rights Watch (HRW) lililoko Marekani limesema kuwa raia 1,492 wa Iran, wakiwemo watoto 221, wameuawa katika mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, huku idadi ya wanajeshi wa Iran waliouawa ikifikia 1,167.
Pia unaweza kusoma:
Uingereza yaishutumu Iran kwa kuuteka uchumi wa dunia
Mawaziri wa mambo ya nje kutoka kwa mataifa saba tajiri zaidi duniani (G7), akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Yvette Cooper, wanakutana nchini Ufaransa. Mazungumzo yanatarajiwa kuangazia vita dhidi ya Iran.
Katika mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza alitoa wito wa “kupatikana kwa suluhu ya haraka” ya mgogoro wa Mashariki ya Kati, akiishutumu Iran kwa “kuushikilia uchumi wa dunia mateka” kwa kuzuia Mlango-Bahari wa Hormuz.
“Ni wazi kabisa kwamba tunahitaji kuona suluhu ya haraka ya mgogoro huu ili utulivu urejee katika eneo hilo,” alisema.
Akizungumzia hatua za Iran katika Mlango-Bahari wa Hormuz, alisema: “Iran haipaswi kuushika uchumi wa dunia mateka kwa kudhibiti tu mlango-bahari unaohusiana na njia za kimataifa za usafiri wa majini na uhuru wa usambazaji.”
Pia unaweza kusoma:
Oburu Oginga aidhinishwa rasmi kuwa kinara wa Chama kikuu cha Upinzani nchini Kenya ODM
Chama kikuu cha upinzani cha Orange Democratic Movement (ODM) kimeridhia rasmi kumteua Seneta wa Siaya, Dkt. Oburu Oginga, kuwa kiongozi mkuu wa chama kufuatia kifo cha kaka yake na kiongozi wa muda mrefu wa chama, Raila Odinga, kilichotokea tarehe 15 Oktoba 2025.
Dkt. Oburu, ambaye awali alikuwa akikaimu nafasi hiyo baada ya kuteuliwa na Baraza la Kitaifa la Uongozi wa chama (NGC), aliidhinishwa rasmi kushika wadhifa huo katika Mkutano Maalum wa Wajumbe (SDC) uliofanyika Jamhuri Grounds siku ya Ijumaa.
Alipendekezwa na Mbunge wa Mumias Magharibi, Johnson Manya Naicca, na kuungwa mkono na Mbunge wa Mathare, Anthony Oluoch, baada ya hoja hiyo kuwasilishwa mbele ya wajumbe na Mkurugenzi wa Uchaguzi na Kampeni wa ODM, Junet Mohamed.
Dkt. Oburu atasaidiwa na Gavana wa Mombasa, Abdulswamad Shariff Nassir, pamoja na mwenzake wa Kisii, Simba Arati, ambao pia walipendekezwa na kuungwa mkono rasmi kushika nyadhifa hizo.
Hata hivyo, Naibu Kiongozi wa chama aliyependekezwa wa tatu, Seneta wa Vihiga, Godfrey Osotsi, hakupata mpendekezaji wala muungaji mkono, na hivyo akaondolewa katika nafasi hiyo.
Hali hii imejiri wakati Osotsi na kundi linalodaiwa kuwa la waasi ndani ya ODM linaloitwa Linda Mwananchi waliposusia mkutano wa SDC na badala yake kuandaa mkutano wao sambamba wa “Kitaifa wa Wajumbe wa Wananchi” (NDC) katika Ufungamano House.
Wakati huo huo, Katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna ameshutumu polisi kwa kuwavurugia Kongamano la Wajumbe wa Kitaifa la Linda Mwananchi lililopangwa kufanyika katika jumba la ufangamano jijini Nairobi.
Sifuna alisema mrengo huo uliarifu rasmi mamlaka kuhusu mkutano huo, ambao alisisitiza ulinuiwa kuwa wa amani na sio maandamano.
Hata hivyo, wanachama waliofika katika ukumbi huo walikutana na malori yaliyokuwa yamejaa maafisa wa polisi, jambo ambalo SG alilitaja kuwa lisilo la lazima na la kutisha.
"Tulipeana ilani kwamba tutakuwa na mkutano hapa, lakini jambo la kusikitisha ni kwamba malori ya polisi yamejaa hapa nje," Sifuna alisema.
Soma zaidi:
Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki IEA laonya hatari ya mionzi iwapo mashambulizi yataendelea Iran
Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) limeonya uwezekano wa kuvuja kwa mionzi hatari iwapo mashambulizi yataendelea karibu na kituo cha nguvu za nyuklia cha Bushehr.
IAEA imetoa wito wa “kudumishwa kwa kiwango cha juu kabisa cha kujizuia” ili kuzuia uchafuzi wa mionzi nchini Iran, onyo lililotolewa kufuatia taarifa za shambulio karibu na kituo hicho kilichopo kusini mwa Iran zilizoripotiwa Jumanne.
“Kwa kuzingatia kwamba hili ni kinu hai cha nyuklia chenye kiwango kikubwa cha nyenzo za nyuklia, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Rafael Grossi, anaonya kuwa uharibifu wowote kwa kituo hiki unaweza kusababisha kuachiliwa kwa mionzi ya nyuklia itakayoweza kuathiri maeneo mapana ndani ya Iran na hata nje ya mipaka yake,” ilisema taarifa ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa.
Soma Pia:
Rais wa Korea Kaskazini Kim Jong Un azawadiwa bunduki
Rais wa Belarus, Alexander Lukashenko, amemkabidhi kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, bunduki kama zawadi, wakati walipotia saini mkataba wa urafiki mjini Pyongyang, vyombo vya habari vya serikali vimeripoti.
Viongozi hao wawili, ambao ni waungaji mkono muhimu wa vita vya Urusi nchini Ukraine, walikubaliana kuimarisha zaidi ushirikiano na kupinga shinikizo la mataifa ya Magharibi.
Lukashenko alitania akimwambia Kim kuwa amemletea bunduki ya kurusha risasi mfululizo “endapo adui atatokea,” kama inavyoonekana katika video iliyotolewa na vyombo vya habari vya Belarus.
Kwa upande wake, Kim alimkabidhi Lukashenko upanga na shoka vilivyochorwa picha yake.
“Ninakuambia kama rafiki yako, na kama mtu aliyeona sehemu nyingi za dunia: mustakabali mzuri sana unaisubiri nchi yako, kwa kuwa una watu wengi wanaofanya kazi kwa bidii na wenye nidhamu,” Lukashenko alimwambia Kim, kwa mujibu wa shirika la habari la Belarus, Belta.
Mashambulizi yafanyika usiku kucha kote Mashariki ya Kati
- Israel imeendelea kushambulia kote Iran usiku kucha, huku jeshi lake likisema asubuhi ya leo kwamba lilishambulia maeneo ya uzalishaji wa makombora huko Tehran na kituo cha kutengeneza vilipuzi vya baharini huko Yazd.
- Mashambulizi dhidi ya Israeli pia yaliendelea - picha zinaonyesha kile kinachoonekana kama njia za roketi angani juu ya mji wa pwani wa Netanya
- Wakati huo huo shambulizi la Israeli lilishambulia vitongoji vya kusini mwa Beirut mapema asubuhi ya leo, kulingana na vyombo vya habari vya Lebanon.
- Bandari kuu ya kibiashara ya Kuwait imeshambuliwa na ndege zisizo na rubani "za adui" - mamlaka ya bandari inasema kumekuwa na "uharibifu wa vifaa" lakini hakuna ripoti za majeruhi
- Na Saudi Arabia imeripoti kuwa ndege nyingi zisizo na rubani zimedunguliwa usiku kucha
- Pia, Wall Street Journal imeripoti kwamba Donald Trump anafikiria kutuma wanajeshi 10,000 wa ardhini Mashariki ya Kati.
Marekani inajiandaa kwa 'shambulizi kubwa la mwisho' katika vita vya Iran
Marekani inajiandaa kwa chaguzi za kijeshi kwa ajili ya "shambulizi kubwa la mwisho" katika vita vya Iran, lenye kujumuisha vikosi vya ardhini na mabomu makubwa, kulingana na ripoti ya Axios, ikinukuu maafisa wawili wa Marekani na vyanzo viwili vyenye ufahamu wa jambo hilo.
Kulingana na ripoti hiyo, "kuongezeka kwa wanajeshi kwa kasi" kunatarajiwa ikiwa hakutakuwa na hatua yoyote iliyopigwa katika mazungumzo kati ya Iran na Marekani.
Trump anaweza kuchagua mapendekezo manne, ikiwa ni pamoja na matumizi ya wanajeshi wa ardhini na uwezekano wa uvamizi wa Kisiwa cha Kharg, sehemu muhimu ya mafuta ya Iran, kulingana na Axios.
Chanzo kinachofahamu juhudi za mazungumzo kilisema kwamba Uturuki, Pakistan, na Misri zinaendelea na majaribio yao ya kupanga mazungumzo kati ya pande hizo mbili.
Chanzo hicho kilibainisha kuwa Iran imekataa madai ya awali ya Marekani lakini haijajiondoa kabisa uwezekano wa kufanya mazungumzo hayo.
Soma zaidi:
Meli mbili za misaada zinazoelekea Cuba hazijulikani zilipo baada ya kuondoka Mexico
Operesheni ya utafutaji na uokoaji inaendelea katika visiwa vya Caribbean kwa meli mbili zilizopotea zilizojaa vifaa vya kibinadamu vinavyosafiri kutoka Mexico hadi Cuba.
Mexico imetuma timu za wanamaji na ndege za utafutaji wa kijeshi ili kupata meli ya Friendship and Tigger Nondo, ambayo ilikuwa na wafanyakazi wasiopungua tisa, jeshi la wanamaji la Mexico lilisema katika taarifa.
Meli hizo zilitarajiwa kuwasili Havana Jumanne au Jumatano, lakini hakuna mawasiliano kutoka kwao na hakuna uthibitisho wa kuwasili kwao, jeshi la wanamaji lilisema.
Jeshi la wanamaji la Mexico lilisema limejitolea kutumia rasilimali zote zilizopo ili kupata meli hizo na kuhakikisha usalama wa wafanyakazi.
Meli mbili zilizopotea ziliondoka Isla Mujeres, katika jimbo la Quintana Roo la Mexico mnamo tarehe 20 Machi.
"Manahodha na wafanyakazi ni mabaharia wenye uzoefu, na meli zote mbili zina vifaa vya usalama vinavyofaa na vifaa vya kuashiria," msemaji wa msafara huo alisema katika taarifa kwa Reuters.
"Tunashirikiana kikamilifu na mamlaka na tunasalia na imani katika uwezo wa wafanyakazi kufika Havana salama."
Soma zaidi:
Saini ya Trump kuonekana kwenye noti ya dola za Marekani
Wizara ya Fedha ya Marekani imetangaza kuwa Donald Trump anatarajiwa kuwa rais wa kwanza wa Marekani aliye madarakani kutia sahihi yake kwenye noti za Marekani.
Saini ya Trump itaonekana pamoja na ile ya Waziri wa Fedha Scott Bessent, hatua ambayo haijawahi kutokea na idara hiyo ilisema itaadhimisha kumbukumbu ya miaka 250 ya Marekani.
"Hakuna njia yenye nguvu zaidi ya kutambua mafanikio ya kihistoria ya nchi yetu kubwa na Rais Donald J Trump zaidi ya noti za dola za Marekani kuwa na jina lake," Bessent alisema.
Noti za Marekani kwa kawaida zimekuwa na sahihi za maafisa wa wizara ya fedha.
Ni hatua ya hivi karibuni ya utawala kuhusisha jina la Trump na programu mbalimbali za serikali na majengo ya umma.
Noti za kwanza za $100 (£75) zenye sahihi za Trump na Bessent zitachapishwa mwezi Juni, na zingine zitafuata.
Noti zinazochapishwa kwa sasa zina sahihi za Waziri wa Fedha wa Rais wa zamani wa Joe Biden, Janet Yellen, na Mweka Hazina Lynn Malerba.
Imekuwa desturi tangu mwaka 1861 kwa sahihi ya mweka hazina wa Marekani kuonekana kwenye noti za benki, desturi ambayo itafikia ukomo wake chini ya mipango ya utawala wa Trump
pia unaweza kusoma:
Urusi na Ukraine zadai kuteka vijiji vilivyokumbwa na vita
Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema Alhamisi kwamba vikosi vyake vimechukua udhibiti wa kijiji kipya cha Sheviakivka katika eneo la kaskazini mashariki mwa Kharkiv la Ukraine, katika hatua yake ya taratibu ya kuteka maeneo.
Jeshi la Ukraine halijakiri kwamba kijiji kilichoko kwenye mpaka wa Urusi kilikuwa kimetekwa.
Kikosi cha wanajeshi wa parachuti cha Ukraine kilisema kimeteka kijiji kilichokuwa kusini katika eneo la Dnipropetrovsk ambacho hapo awali kilikuwa kimetawaliwa na Urusi.
Hata hivyo, Reuters haijaweza kuthibitisha ripoti za maeneo ya vita kwa uhuru.
Soma zaidi: