Watu kumi wauawa katika mapigano kati ya Hamas na wanamgambo Gaza
Vyanzo vya ndani vinasema kuwa takriban Wapalestina 10 wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israeli na mapigano kati ya Hamas na wanamgambo wa Palestina wanaoungwa mkono na Israeli katikati mwa Gaza.
Inasemekana mashambulizi hayo yaliwalenga maafisa wa usalama wa Hamas ambao walikuwa wamepambana na wanamgambo wa mashariki mwa kambi ya wakimbizi ya Maghazi. Haijulikani ni wangapi kati yao walikufa katika mashambulizi hayo au katika mapigano ya ardhini.
Msemaji wa hospitali ya al-Aqsa huko Deir al-Balah alisema walipokea miili ya watu 10 kutoka eneo la tukio. Watu wengine kadhaa walijeruhiwa na wengine walikuwa katika hali mbaya, waliongeza.
Hakukuwa na taarifa yoyote ya haraka kutoka kwa jeshi la Israel au Hamas.
Mashahidi walisema wanamgambo wanaoungwa mkono na Israeli waliweka kituo cha ukaguzi mashariki mwa Maghazi, ambapo walishambuliwa na maafisa wa usalama wa Hamas, na kusababisha mapigano.
Mashahidi hao waliongeza kuwa ndege zisizo na rubani za Israeli ziliingilia kati kuwasaidia wanamgambo, zikifanya mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa Hamas katika maeneo matatu.
Israel na Hamas wameshutumuana kwa kukiuka mara kwa mara makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo walikubaliana karibu miezi sita iliyopita.
Takriban Wapalestina 723 wameuawa huko Gaza katika mashambulizi ya Israeli tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoongozwa na Hamas.
Jeshi la Israel limesema wanajeshi wake watano wameuawa katika mashambulizi ya makundi ya Wapalestina katika kipindi hicho hicho.
Pia unaweza kusoma: