Moja kwa moja, Trump atishia kuiangamiza Iran ndani ya 'usiku mmoja'

Trump amesema anaamini viongozi "wenye busara" nchini Iran walikuwa wakijadiliana kwa "nia njema", lakini matokeo yake yamesalia kuwa yasio na uhakika.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Watu kumi wauawa katika mapigano kati ya Hamas na wanamgambo wa Gaza

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Vyanzo vya ndani vinasema kuwa takriban Wapalestina 10 wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israeli na mapigano kati ya Hamas na wanamgambo wa Palestina wanaoungwa mkono na Israeli katikati mwa Gaza.

    Inasemekana mashambulizi hayo yaliwalenga maafisa wa usalama wa Hamas ambao walikuwa wamepambana na wanamgambo wa mashariki mwa kambi ya wakimbizi ya Maghazi. Haijulikani ni wangapi kati yao walikufa katika mashambulizi hayo au katika mapigano ya ardhini.

    Msemaji wa hospitali ya al-Aqsa huko Deir al-Balah alisema walipokea miili ya watu 10 kutoka eneo la tukio. Watu wengine kadhaa walijeruhiwa na wengine walikuwa katika hali mbaya, waliongeza.

    Hakukuwa na taarifa yoyote ya haraka kutoka kwa jeshi la Israel au Hamas.

    Mashahidi walisema wanamgambo wanaoungwa mkono na Israeli waliweka kituo cha ukaguzi mashariki mwa Maghazi, ambapo walishambuliwa na maafisa wa usalama wa Hamas, na kusababisha mapigano.

    Mashahidi hao waliongeza kuwa ndege zisizo na rubani za Israeli ziliingilia kati kuwasaidia wanamgambo, zikifanya mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa Hamas katika maeneo matatu.

    Israel na Hamas wameshutumuana kwa kukiuka mara kwa mara makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo walikubaliana karibu miezi sita iliyopita.

    Takriban Wapalestina 723 wameuawa huko Gaza katika mashambulizi ya Israeli tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoongozwa na Hamas.

    Jeshi la Israel limesema wanajeshi wake watano wameuawa katika mashambulizi ya makundi ya Wapalestina katika kipindi hicho hicho.

  2. Wachezaji saba wa Eritrea waingia mitini baada ya mechi ya kimataifa

    .

    Chanzo cha picha, ENFF

    Wachezaji saba kutoka kikosi cha mpira wa miguu cha Eritrea waliopata ushindi wa kihistoria huko Eswatini wiki iliyopita hawajarudi nyumbani, chanzo cha karibu na timu hiyo kimeiambia BBC.

    Huku baadhi ya wachezaji wenzao wakirejea, inasemekana wote saba walitoroka.

    Kumekuwa na visa kadhaa ambapo Waeritrea wanaoshiriki katika michezo mbalimbali hawarudi nyumbani baada ya mechi za kimataifa katika miaka ya hivi karibuni.

    Makundi ya haki za binadamu yameelezea serikali ya Asmara kama ya ukandamizaji mkubwa - dai ambalo mamlaka inakataa. Licha ya idadi ndogo ya watu, mamia ya maelfu ya Waeritrea wametafuta hifadhi nje ya nchi.

    Habari za wachezaji hao kutoroka zitakuwa pigo kwa timu hiyo, ambayo, baada ya ushindi wake wa 2-1 dhidi ya Eswatini na ushindi wa jumla wa 4-1, ilikuwa ikisherehekea kurudi katika hatua za makundi za kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 19.

    Ni wachezaji 10 pekee kati ya 24 waliokuwa na makao yao nchini Eritrea na ni wachezaji watatu tu kati ya hao, akiwemo nahodha wa timu hiyo Ablelom Teklezghi, ambao sasa wamerejea, vyanzo kutoka Asmara viliiambia BBC Tigrinya.

    Ingawa haijulikani wazi wachezaji waliopotea wamekwenda wapi, ripoti zinasema baadhi yao wameonekana Afrika Kusini.

    Waliotoroka ni pamoja na kipa Kubrom Solomon na winga mkongwe Medhanie Redie.

    Vyombo vya habari vya serikali ya Eritrea vimekuwa kimya sana kuhusu kurejea kwa timu hiyo iliyoshinda, jambo ambalo kwa kawaida lingeambatana na shamrashamra za kuwakaribisha nyumbani.

    Vyanzo vinasema maandalizi yalifanywa kwa ajili ya mapokezi lakini yalifutwa kufuatia habari za kutoweka kwa wachezaji hao.

    Soma zaidi:

  3. Kanye West anachunguzwa iwapo anastahili kuingia Uingereza

    .

    Chanzo cha picha, PA Media

    Serikali inapitia upya iwapo Kanye West anapaswa kuruhusiwa kuingia Uingereza baada ya kuzua ghadhabu ilipotangazwa kuwa ndiye atakayeongoza tamasha la London ambalo rapa huyo alikuwa amepangiwa na kusababisha ukosoaji juu ya matamshi yake ya awali ya chuki dhidi ya Wayahudi.

    Nyota huyo, ambaye sasa anajulikana kama Ye, alitoa wimbo unaoitwa Heil Hitler na kuuza fulana za swastika mwaka jana. Baadaye aliomba msamaha na kutupia kidole cha lawana ugonjwa alionao wa hisia zinazobadilika-badilika.

    Waliokuwa wasimamizi wa tamasha hilo wamejiondoa, na wakosoaji wanatoa wito kwa waandaaji wake kumuondoa kwenye tamasha hilo na viza yake ya kuingia Uingereza ifutiliwe mbali.

    Mawaziri wana mamlaka ya kuwapiga marufuku raia wa kigeni kuingia au kuondoka Uingereza ikiwa uwepo wao hautachukuliwa kuwa "wenye manufaa kwa umma".

    Rapa huyo tayari amepigwa marufuku kuingia Australia, ambayo ilifuta viza yake baada ya kutoa wimbo wa Heil Hitler mwezi Mei mwaka jana.

    Soma zaidi:

  4. DR Congo yakubali kuwachukua wahamiaji kutoka Marekani

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imekubali kuwapokea wahamiaji waliohamishwa kutoka Marekani ambao wenyewe si WaCongo chini ya makubaliano yanayoanza kutekelezwa mwezi huu, maafisa walisema.

    Wizara ya Mawasiliano ilisema mfumo wa mapokezi wa muda umeanzishwa, huku vituo vya kuwahudumia wanaowasili vikitambuliwa katika mji mkuu, Kinshasa.

    "Msaada wa vifaa na kiufundi" utatolewa na Marekani, taarifa hiyo ilisema Jumapili, ikiongeza kuwa serikali ya Congo haitagharamia chochote kuhusiana na suala la kifedha kutekeleza mpango huo.

    Serikali haikusema ni wahamiaji wangapi watakaowakubali.

    Marekani tayari imewatuma wahamiaji katika nchi zingine kadhaa barani Afrika kama sehemu ya msako wao dhidi ya uhamiaji.

    Huku kukiwa na wasiwasi kwamba wahamiaji wanaweza kurejeshwa katika nchi zao za asili - ambapo baadhi wanaogopa mateso - maafisa wa Congo walisema hakuna uhamisho kama huo unaopangwa.

    Uamuzi wa kuwapokea wahamiaji kutoka nchi nyingine - yaani wale ambao hawatoki katika taifa linalowatuma wala kuwapokea - unaendana na dhamira ya DR Congo kwa utu wa binadamu, mshikamano wa kimataifa na kulinda haki za wahamiaji, taarifa hiyo ilisema.

    Mamlaka ya Congo pia ilisema kwamba mpango huo si "mfumo wa kudumu wa kuhama au utoaji wa sera za uhamiaji kwa watu wengine".

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema kwamba ingawa haikutoa maoni yoyote kuhusu "mawasiliano ya kidiplomasia na serikali zingine," serikali bado "imeshikilia msimamo wake" katika "ahadi yake ya kukomesha uhamiaji haramu na kuimarisha usalama wa mpaka wa Marekani".

    Soma zaidi:

  5. Trump atishia kuiangamiza Iran ndani ya 'usiku mmoja'

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kuiangamiza Iran "ndani ya usiku mmoja" ikiwa itashindwa kufikia makubaliano kabla ya tarehe ya mwisho aliyoiweka kwa Tehran kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji duniani.

    Tarehe ya mwisho ya Trump ya kufikiwa kwa "makubaliano" - ambayo yanajumuisha usafirishaji huru wa mafuta kupitia Ghuba - imewekwa saa 20:00, saa za Washington DC siku ya Jumanne (00:00 GMT Jumatano).

    Akizungumza katika Ikulu ya White House, Trump alisema kwamba anaamini viongozi "wenye busara" nchini Iran walikuwa wakijadiliana kwa "nia njema", lakini matokeo yake yamesalia kuwa yasio na uhakika.

    Iran imekataa mapendekezo ya kusitisha mapigano kwa muda, badala yake imetoa wito wa kukomeshwa kabisa kwa vita na kuondolewa kwa vikwazo.

    Mkutano wa Trump na waandishi wa habari uliofanyika pamoja na Jenerali Dan Caine, mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi na waziri wa ulinzi Pete Hegseth umefanyika siku chache baada ya vikosi vya Marekani kuwapata marubani wawili wa ndege ya kivita ya F-15 iliyodunguliwa kusini mwa Iran.

    Ingawa sehemu kubwa ya matamshi ya Trump yaliangazia kile alichokielezea kama uokoaji wa "kishujaa" wa marubani, alirudia tena onyo lake kwamba Marekani inaweza kuanzisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati na usafiri ya Iran ikiwa Mlango-Bahari wa Hormuz hautafunguliwa tena kufikia tarehe ya ukomo ya Jumanne.

    "Nchi nzima inaweza kuangamizwa kwa usiku mmoja - na usiku huo unaweza kuwa kesho usiku," alisema Jumatatu, akimaanisha leo usiku.

    Mara tu tarehe ya mwisho itakapopita, Trump aliongeza, Iran itarudishwa ksiku za "Enzi ya Mawe".

    "Hawatakuwa na madaraja," alisema. "Hawatakuwa na viwanda vya umeme."

    Licha ya Iran kukataa matakwa ya Marekani hapo awali, Trump aliendelea kuonyesha matumaini kwamba Iran ilikuwa ikijadiliana kwa nia njema baada ya safu ya mfululizo za uongozi wa Iran kuuawa katika mashambulizi ya Marekani na Israel.

    "Tutajua tu," alisema.

    Maendeleo yenye tija katika mazungumzo yoyote hayawezekani kufanyika bila kusitisha mapigano kwanza, kulingana na afisa wa kikanda anayefahamu majadiliano hayo.

    Afisa huyo - ambaye aliomba kutotajwa jina kutokana na jinsi mazungumzo yalivyo nyeti - alisema kwamba majadiliano yalikuwa magumu kwa sababu ya changamoto ya mawasiliano kutoka kwa maafisa wa Iran kutokana na hatua ya kuminywa kwa intaneti.

    "Ili kufikisha ujumbe kwa Iran, kupata jibu kwa wakati unaofaa ni jambo lisilowezekana," afisa huyo alisema. "Wastani wa muda wa kutoa majibu umekuwa siku moja hivi."

    Pakistani, Uturuki na Misri zote zinahusika katika juhudi za upatanishi.

    Soma zaidi:

  6. Hujambo. Karibu katika matangazo yetu mubashara ya tarehe 07/04/2026.