Zaidi ya watu sabini hawajulikani waliko baada ya mashua kuzama katika bahari ya Mediterania

Chanzo cha picha, Reuters
Zaidi ya watu sabini hawajulikani waliko baada ya mashua walimokuwa wakisafiria kupinduka katikati mwa bahari ya Mediterania.
Makumi ya watu hawajulikani walipo baada ya boti iliyokuwa ikisafirisha wahamiaji kupinduka na kuzama katikati mwa bahari ya Mediterania, kwa mujibu wa shirika moja la kutetea haki za kibinadma la Mediterranea Saving Humans and Sea-Watch.
Kulingana na shirika hilo watu wawili walikufa na wengine 32 waliokolewa kutoka kwa boti hiyo, ambayo ilikuwa imeondoka nchini Libya siku ya Jumamosi alasiri ikiwa na karibu watu 105.
Kwenye mtandao wa kijamii wa X, shirika hilo limesema kuwa boti hiyo ilipinduka katika eneo la utafutaji na uokoaji linalosimamiwa na mamlaka ya Libya msimu huu wa pasaka na kuwa watu 32 walinusurika, miili miwili imepatikana na zaidi ya watu 70 hawajulikani walipo.
Shirika hilo la Sea-Watch lilisema meli mbili za kibiashara ziliokoa manusura na kuwapeleka kwenye kisiwa cha Italia cha Lampedusa.
Video iliyonaswa kutoka angani ilionyesha wanaume wawili wakiwa wameshikilia ubao wa meli iliyopinduka, na meli moja ya kibiashara ikielekea katika eneo la tukio.
Mediterranea Saving Humans and Sea-Watch ilisema ajali hiyo ni matokeo ya sera za serikali za Ulaya ambazo zinakataa kufungua njia salama na za kisheria kwa wahamiaji.
Lampedusa ni kituo muhimu cha kuingilia kwa wahamiaji wanaovuka bahari ya Mediterania kutoka Afrika Kaskazini kwenda Ulaya.
Kulingana na shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM, tangu kuanza kwa mwaka wa 2026, wahamiaji wasiopungua 683 wamepoteza maisha yao au kupotea katika majaribio ya kuvuka bahari ya mdeterenian.



