Mvulana wa Kipalestina asimulia jinsi familia yake ilivyouawa na vikosi vya Israel

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Wazazi wa Khaled Bani Odeh na ndugu zake wawili walipigwa risasi ndani ya gari akitazama.
Muda wa kusoma: Dakika 5

Onyo - Makala haya yana maelezo kuhusu ufyatulianaji risasi.

Baada ya kimya cha muda mfupi kufuatia tukio la ufyatuaji risasi, Khaled Bani Odeh mwenye umri wa miaka 12 alidhani yeye pekee ndiye aliyebaki hai katika familia yake kabla ya kutoka kwenye gari.

Sekunde chache kabla, wazazi wake na wadogo zake wawili wa kiume walipigwa risasi na kuuawa kupitia kioo cha mbele na wanajeshi wa Israel, walipokuwa wakiendesha gari kurudi nyumbani baada ya kwenda kununua mahitaji ya familia katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel.

Miongoni mwa waliokufa ni Othman mwenye umri wa miaka saba - kipofu na mlemavu - aliyeuawa akiwa ameketi kwenye mapaja ya mama yake.

"Mama yangu alilia mara ya mwisho kabla ya kunyamaza," Khaled alisema. "Baba yangu alisoma Shahada [tamko la imani la Kiislamu] alipokufa."

Wakati vikosi vya Israel vilipomtoa kaka yake aliyesalia, Mustafa, kutoka kwenye gari, Khaled alisema alijaribu kuingilia kati.

"Walinivuta nje," anasema. "Kisha walinipeleka kwenye kona na kuniuliza kuhusu ni nani aliyekuwa ndani ya gari. Niliwaambia ni mama na baba yangu. Walinituhumu kwa kusema uongo na wakaanza kunipiga."

.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Mkewe Ali Khaled Bani Odeh, na ndugu zake wawili walizikwa siku ya Jumapili.

Familia ya Ali Khaled Bani Odeh mwenye umri wa miaka 37 na mkewe Waad mwenye umri wa miaka 35 waliuawa karibu na kwao katika kijiji chao Tammun, karibu na Tubas, saa sita usiku.

Jamaa wanasema Ali alirudi nyumbani hivi karibuni huko Tammun baada ya wiki sita kufanya kazi katika eneo la ujenzi nchini Israel, na wavulana hao walimtaka awapeleke kufanya manunuzi huko Nablus, kabla ya likizo ya Eid al-Fitr.

Usiku huo, walipokuwa wakirudi kutoka kufanya ununuzi na chakula cha jioni huko Nablus, jeshi la Israel linasema wanajeshi wake na Polisi wa Mpakani walikuwa wakifanya operesheni huko Tammun kuwakamata watu wanaoshukiwa kufanya shughuli za kigaidi dhidi ya vikosi vya usalama vya Israel.

Wanasema gari la familia ya Bani Odeh "lilielekea kwa kasi kuelekea vikosi, ambavyo vilihisi hatari na kujibu kwa risasi."

Maelezo ya shuhuda

.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lakini mkazi aliyekuwa karibu, anayeishi karibu na barabara, alituambia alikuwa akichungulia nje ya dirisha lake wakati tukio hilo lilipotokea, baada ya kusikia ufyatuaji risasi wa hapa na pale. Hatutamtaja jina lake, ili kulinda utambulisho wake.

Anasema gari la familia lilikuwa limegeuka kushoto kuelekea mtaani kwake, likielekea juu, na lilikuwa limesimama kabisa kabla ya risasi zozote kufyatuliwa, kinyume na maelezo ya jeshi la Israel.

Nilimuuliza kama alisikia maonyo yoyote yaliyotolewa na vikosi vya Israei, au risasi zozote za onyo zilizopigwa.

"Hapana, hakuna kitu," anasema. "Milio ya risasi ililenga gari moja kwa moja. Nilimsikia tu mwanamke aliyekuwa ndani ya gari akipiga kelele. Watoto wadogo walikuwa wakilia kabla hawajauawa."

Taarifa ya gazeti la New York Times la Marekani, inaelezea Waad alimwomba mumewe asimame barabarani ili aweze kutafuta kitu kwenye begi lake.

Jeshi la Israel linasema tukio hilo linachunguzwa na mamlaka husika.

Tuliomba majibu kuhusu ripoti kwamba gari lilikuwa limesimama na lilishambuliwa bila onyo, na tukaambiwa tuelekeze maswali yetu kwa polisi. Tunasubiri majibu yao.

.

Katika nyumba ya familia, bibi yake Khaled, Najah Bani Odeh, aliketi akiwa amezungukwa na waombolezaji. Kando yake anabembelezwa na wanawake mara kwa mara, na Mustafa mwenye umri wa miaka minane akiwa ameketi mbele yake.

Bibi yake alituonyesha bandeji usoni mwake.

"Ni vipande vya kioo kutoka dirishani mwa gari walipofyatua risasi," anasema. "Anahitaji upasuaji ili kuviondoa."

Anasema familia haina taarifa zozote kuhusu operesheni yoyote ya kijeshi katika kijiji hicho walipokuwa wakielekea nyumbani.

"Walikuwa wakiendesha gari karibu na eneo la shule ambapo vikosi maalum vilikuwa vimejificha. Watoto walikuwa wakiimba na kufurahi. Mohammed, ambaye alikuwa katika shule ya chekechea, alikuwa ameketi kati ya mama na baba yake walipopigwa risasi."

Anasema Mohammed alianguka kwenye mapaja ya Mustafa wakati ufyatuaji risasi ulipoanza, na nguo za Mustafa zikajaa damu.

.
Maelezo ya picha, Mustafa Bani Odeh, mwenye umri wa miaka nane, alijeruhiwa.

Hassan Fuqoha, mmoja wa wafanyakazi wa gari la wagonjwa la Hilali Nyekundu la Palestina aliyeitwa kwenye eneo la tukio, alituambia eneo hilo lilikuwa tofauti kabisa na matukio mengine aliyohudhuria, na wazazi wote wawili na mmoja wa watoto wamepasuka vichwa kwa risasi.

"Niliona maganda mengi ya risasi, kila mahali karibu na gari," anasema. "Risasi zilifyatuliwa nyingi mno, moja kwa moja kwenye gari, si kawaida."

Wakazi walituambia walipata zaidi ya maganda 50 ya risasi, zenye ukubwa unaotumiwa na vikosi vya jeshi la Israel, na kuzikabidhi kwa mamlaka.

.
Maelezo ya picha, Najah Bani Odeh, nyanyake Mustafa

Yair Lapid, mkuu wa chama cha upinzani cha Israeli Yesh Atid, ameikosoa serikali ya Israel kwa kutoomba msamaha kwa familia hiyo kwa vifo vya watoto.

"Mvulana wa miaka saba mwenye mahitaji maalum hapaswi kufa katika vita vya watu wazima," amesema.

Matumizi ya nguvu kubwa dhidi ya gari la raia lililokuwa limebeba watoto wanne wadogo yameibua tena mjadala jinsi wanajeshi wa Israel wanavyo washughulikia Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi.

Najah Bani Odeh aliniambia mauaji ya mwanawe, mkwewe na wajukuu wawili ni sehemu ya vurugu zinazoongezeka dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi, na wanajeshi wa Israel na walowezi, tangu mashambulizi ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba 2023 dhidi ya Israeli.

"Mlowezi mmoja huko anaendelea na ghasia akiwadhuru wanaume, wanawake na watoto, nasi tunajilinda kwa kurusha mawe tu," alisema.

"Wanataka kutunyang'anya ardhi zetu. Sasa wanajenga kuta kuzunguka ardhi walizochukua na kufyatua risasi wapendavyo kwa yeyote anayekaribia."

Kati ya tarehe 7 Oktoba 2023 na 15 Machi 2026, ofisi ya masuala ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, OCHA, inasema Wapalestina 1,071 wameuawa katika Ukingo wa Magharibi, wakiwemo watoto wasiopungua 233.

Inasema raia 19 wa Israel na maafisa wa usalama 23 wa Israela wameuawa hapo kuanzia Oktoba 2023 hadi katikati ya Oktoba 2025.

Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula na kuhaririwa na Ambia Hirsi