Vitisho vya Trump dhidi ya Iran, tafsiri na athari zake kwenye vita

Chanzo cha picha, Alex Brandon-Pool/Getty Images
- Author, Asha Juma
- Nafasi, BBC Nairobi
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Rais wa Marekani Donald Trump hivi karibuni aliandika ujumbe wa vitisho na maneno machafu kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, ambapo alitishia kuharibu viwanda vya nishati na madaraja ya Iran ikiwa itashindwa kufanya makubaliano kufikia tarehe yake ya mwisho aliyoitoa ya kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz.
Wakati anazungumza na wanaandishi wa habari siku ya Jumatatu ya Pasaka, Trump aliulizwa kwa nini alitumia "lugha chafu kama hiyo" katika ujumbe kwenye mtandao wa Truth Social – mwanahabari akirejelea matusi aliyotumia katika tishio lake la hivi karibuni kwa Iran kufungua Mlango-Bahari wa Hormuz.
Alisema "Ni kwa ajili tu ya kueleza hoja yangu".
"Nafkiri umewahi kusikia maneno kama hayo hapo awali."
Kama ulivyoone, Trump anadai kuwa hii ni njia moja ya kueleza hoja zake, lakini kwa mchambuzi wa masuala ya kisiasa Mubelwa Bandio aliyezungumza na BBC Swahili, ameashiria kuwa Trump ana tabia ya kwenda mbele na kurudi nyuma kumaanisha kuwa leo anasema hili, watu wakiwa bado wanalitafakari ameshazungumza jingine jipya.
"Alitoka kuambia watu kwamba yeye hana haja na wanaotaka mafuta wajifuatie wenyewe katika Mlango Bahari wa Hormuz lakini leo anaonekana kuhangaika huku na kule hasa baada ya ndege yake kudunguliwa Iran," Bandio alisema.
Kwa mtazamo wake, ilipofikia Trump hana jingine zaidi ya "kufanya mashambulizi".
Mkakati wa kuongeza shinikizo?

Chanzo cha picha, EPA
Kwa wengine vitisho hivi vya Rais Donald Trump dhidi ya Iran vinaeleweka kama njia ya kuongeza shinikizo na kulazimisha kufikiwa kwa makubaliano basi hata kama hayatukuwa ya muda mrefu angalau ya muda mfupi yapatikane.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Lakini kuna uwezekani kwa upande mwingine, Trump anatumia vitisho hivyo kama mkakati wa kifika kwenye meza ya mazungumzo ambayo amekuwa akionyesha dunia kuwa ni moja ya machaguo yake katika njia anazofikiria kuzitumia kumaliza mzozo huu.
Suali la kujiuliza ni je, mbinu hii ya kuongeza mashambulizi kisha kuomba kufanyika kwa mazungumzo ni kwamba anatafuta suluhu ya kudumu au njia nyingine ya kupoteza muda ili kupata fursa ya kutimiza lengo lake.
"Ikumbukwe kwamba Trump anachukia sana kushindwa na mpaka kufikia sasa ameshindwa kwa sababu Marekani anashinda kwa kutokushindwa na Iran anashinda kwa kutokushindwa. Mlima ni mkubwa kwa Mrekani kuliko Iran na nafkiri amegundua hilo na linamsumbua akili," alisema Bandio.
Marekani na Iran zimeweka mapendekezo ya kusitisha vita lakini tayari Iran imesema makubaliano ya kusitisha mapigano yataruhusu Marekani na Israel 'kujipanga upya ndani ya muda mfupi'
Iran ilishawasilisha matakwa yake ya hoja 10 kwa pendekezo la Marekani ikidai kuwa kuna haja ya kuwa na mwisho wa kudumu wa vita.
Pengine mzizi wa hili kama vile Bandio anavyosema ni kutokana na historia yake wakati wa vita kwa madai kuwa waingine kwenye meza ya mazungumzo.
"Trump ana historia fulani, ya kwanza ni kwamba katikati ya mazungumzo yenye mafanikio, tumeona mwaka jana na mwaka huu alipoishambulia Iran. Ni katikati ya mazungumzo wakati Iran inafuata walichokubaliana na kila mtu ametulia, yeye anageuka na kuanza kufanya mashambulizi," Bandio anasema.
Tuangazie kidogo mara ambazo Trump ameahirisha makataa aliyoweka mwenyewe dhidi ya Iran.
"Jumanne itakuwa Siku ya Viwanda vya Umeme, na Siku ya Madaraja, yote yakiwa yameunganishwa pamoja, nchini Iran," aliandika. "Itakuwa kitu ambacho hakijawahi kutokea!!!" - siku ya ukomo akisema ni "Jumanne, 8:00 P.M. Mashariki ya Kati!"
Hiki ndio kitisho cha hivi karibuni zaidi. Lakini tarehe ambazo amakuwa akizitoa kama makataa kwa Iran kufungua Mlango Bahari wa Hormuz ni pamoja na Machi 21 mwaka 2026.
Trump alitishia kushambuliwa viwanda vya nishati vya Iran ikiwa haitafungua Mlango Bahari ndani ya saa 48. Siku mbili baadaye, alisema majadiliano yanaendelea vizuri na kuahirisha mashambulizi katika miundombinu ya nishati kwa siku tano.
Machi 27, Trump alisema ataahirisha mashambulizi katika miundombinu ya nishati kwa siku 10, "kulingana na ombi la serikali ya Iran", na siku ya ukomo ikasongezwa mbele hadi 6 Aprili.
Huku tarehe hiyo ikiwa inakaribia, Trump alionya ikiwa Iran haitafungua Mlango Bahari ndani ya saa 48, atafanya mashambulizi aliyoyapa jina "mvua ya kuzimu"
Akizungumza na wanahabari, Trump amesema "Marekani inaendelea vizuri sana," akizungumzia vita vinavyoendelea dhidi ya Iran.
Kisha alirejelea tarehe ya mwisho aliyoweka ya mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati na usafiri ya Iran ikiwa haitafungua Mlango-Bahari wa Hormuz.
"Nchi nzima inaweza kumalizwa kwa usiku mmoja - na usiku huo unaweza kuwa kesho usiku," alisema akimaanisha leo usiku.
Akizungumza na BBC Swahili, Fernando Wolle mchambuzi wa masuala ya kisiasa alisema hatua hiyo "ni kitisho lakini kinaendana na diplomasia kwa sababu mara nyingi kauli zake zimekuwa hazifungii upande mwingine wa mazungumzo."
Lakini pia, Wolle amerejelea kuwa mara ambazo Trump amekuwa akisongeza mbele makataa aliyotoa, huenda ikawa ni ishara kuwa amefika mwisho na baada ya hapo kuna uwezekano akafanya lolote.
Ubabe wa Marekani au dalili za kukata tamaa?

Chanzo cha picha, Getty Images
Matamshi machafu na vitisho kutoka kwa Trump kama vile 'kutanyesha mvua wa kuzimu' na mengine mengi ambayo ameyatamka katika vita hivi, yanazua maswali mengi kama vile, je, bado Marekani inaamini ndiyo mbabe katika vita hivi au ni kuonyesha kukata tamaa?
Kuna uwezekano hata pengine walio karibu naye, nao wanatatizika na kauli zake hasa ukizingatia kwamba mara nyingi kinachojitokeza ni kama anachoandika huwa maamuzi yake binafsi tena anakiweka kwenye mtandao wake wa kijamii na sio kwamba semi zake hufuata itifaki kama ilivyozoeleka kwa tawala mbalimbali duniani.
Trump anaweza kulichukulia hili kama ushindi au namna ya kuonyesha kwamba bado makali yake yanapata, inaweza kuwa inaongeza hatari ya kuongezeka kwa vita hata kama pengine sio kusudi lake.
Makataa na maneno ya namna hii ni vigumu sana kuchukuliwa ya kawaida na upande ambao muko kwenye kipindi cha msuguano. Kuna uwezekano kwamba Iran inaendelea kujiweka sawa kwa namna moja au nyingine hata ingawa inaonekana kama iliyoshambuliwa sana kiasi cha kukaribia kusambaratika.
Dhihirisho ya hili ni pale ambapo Trump alisema Iran inakaribia kufanya makubaliano lakini ghafla dunia ikashuhudia ndege ya kivita ya Marekani ikidunguliwa kwenye anga la Iran.
Pia ikumbukwe kuwa Iran imesema mashambulizi katika miundombinu yake ya kiraia itakuwa ina halalisha kuongezeka kwa vita vya kikanda ikiwa ni pamoja na mashambulizi katika vituo vya nishati vya Ghuba.
Vitisho vya Trump ni mzaha au anamaanisha kweli?

Chanzo cha picha, EPA
Kama ilivyojitokeza mwanzoni mwa makala hii, halitakuwa jambo la busara kuchukuliwa vitisho vya Trump kama mzaha tu. Ikumbukwe kuwa yeye ni Amiri Mkuu wa Jeshi la Marekani na anaptoa amri zake, basi hakuna wa kumpinga.
"Athari zozote ni kheri zijitokeze sasa kuliko akaamua kufanya maamuzi. Rais anapofanya maamuzi yoyote hapa nchini Marekani hata kama nikutumia nyuklia, nafkiri wanakuwa na dakika kama nne tu za kutekeleza kwa sababu yeye ni amiri jeshi mkuu", alisema Bandio.
Ukosoaji umeanza kujitokeza dhidi ya Trump na pengine kuna wale wanaomuunga mkono.
Fungua Mlango-Bahari, nyinyi wanaharamu, la sivyo mtakuwa mnaishi Kuzimu - FUATILIA TU!" Trump aliandika, akisisitiza tena tishio lake la kufyatua mabomu kwenye viwanda vya nishati na madaraja ya Iran ikiwa Tehran itakataa kufungua Mlango-Mkuu wa Hormuz.
Ni ujumbe kama huo ambao umesababashi Trump kukosolea.
"Heri ya Pasaka, Marekani. Unapoelekea kanisani na kusherehekea na marafiki na familia, Rais wa Marekani amecharukwa kama mwendawazimu kwenye mitandao ya kijamii," Kiongozi wa Wachache wa Bunge la Seneti wa chama cha Democratic Chuck Schumer alisema kwenye mtandao wa X.
"Anatishia kutenda uhalifu wa kivita na kuwatenga washirika. Hivi ndivyo alivyo, lakini hivi sivyo tulivyo. Nchi yetu inastahili mtu bora zaidi."
Kwa Seneta wa Democratic Chris Murphy wa Connecticut, ambaye anapinga vita nchini Iran, mtazamo wa Trump ulikuwa "usio na msingi kabisa."
Hata hivyo, licha ya ukosoaji mkubwa wa vita, washirika wa rais wa Trump wa chama cha Republican wamemuunga mkono kwa kiasi kikubwa.
"Rais Trump ana haki ya kusisitiza kwamba makubaliano yoyote yaliyojadiliwa yanakidhi malengo yetu ya kijeshi na kimkakati. Ikiwa Iran itakataa, ana haki ya kulipua miundombinu yao muhimu ili wasiweze kurudi kwenye njia zao za zamani," Seneta wa Republican Lindsey Graham alisema.
"Huwezi kuruhusu nchi kuwalenga Wamarekani mara kwa mara na isijibu. Ayatollah na wasaidizi wake walifanya haya kwa muda mrefu," Bacon aliandika kwenye X, akimrejelea Kiongozi Mkuu Ali Khamenei, ambaye aliuawa siku ya kwanza ya vita.
Ukipima kwa mizani huenda anachosema Trump kipo na kama hakipo kinjiani chaja. Wewe tafakari hili, kama ni uwezo wa kijeshi Trump anao na kama ni usemi wa mwisho pia anao.
Bandio anasema hata kama kuna wale ambao watamchukulia kama ni 'mwoga' au 'aibu' kwa sababu ya kuahirisha makataa yake, hilo litakuwa vyema zaidi badala ya kufuata kile ambacho ametishia kufanya kwa sababu madhara yake ni makubwa.
Vile vile, usisahau kuwa hadi kufikia sasa, Trump hajatangaza vita kamili na Iran na uwezekano mkubwa ni kwamba, vitisho na maneno machafu, ni mkakati wa kushinikiza Iran kuridhia anachotaka hasa katika kipindi hiki ambapo hakuna uhakika wa kitakachotokea dakika inayofuata.















