Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wanaanga wa Artemis II wavunja rekodi kwa safari ya kihistoria mwezini
Hakuna mtu ambaye ameenda mbali sana na dunia, isipokuwa wanaanga wa Artemis II.
Kikosi hicho kimeandika historia ya kipekee ya kufika kwenye mwezi.
Historia ya awali ilishikiliwa na Appolo 13 ambapo walisafiri zaidi ya kilomita 400,171 kutoka duniani mwaka wa 1970.
Wanaanga wa Artemis II wamezidisha kiwango hicho na kufika kilele cha kilomita 406,000.
"Wanaanga hao walisema kizazi kijacho kinafaa kuvunja rekodi hiyo"
Kamanda Reis Wiseman ambaye anasimamia misheni ya Artemis II anaelezea alichokiona kupitia dirisha la chombo chao
"Dunia inakaa kama mwezi mwandamo, inakaa vizuri kabisa, nilichukua picha," alisema
NASA imetoa picha za kwanza zenye ubora wa juu zaidi zilizotumwa duniani, zilizopigwa na kikosi cha Artemis II walipokuwa wakipita kati ya dunia na mwezi.
Kipindi cha kutazama mwezi kilidumu saa saba
Wanaanga walishuhudia kupatwa kwa Jua
Wanaanga hao pia walichunguza "miale hatari" wakati wakirejea.
Hii ni mlipuko wa mwanga wa papo hapo na wa muda mfupi sana inayotokea wakati mawe madogo ya angani yanapogonga mwezi kwa kasi kubwa na kuyeyuka yenyewe.
Kikosi hicho, kilichukua mapumziko ya saa moja kwa ajili ya uchunguzi, walishuhudia kupatwa kwa jua saa moja baadaye.
Dakika 40 za kukatika kwa mawasiliano
Tangu kuenda angani, kikosi hicho kimedumisha mawasiliano ya mara kwa mara na kituo kinachoendesha misheni hiyo mjini Houston, Texas.
Timu ya Nasa imekuwa ikiwapa motisha wanaanga wao kwa kuhakikisha wanawasiliana na watu walioko duniani.
Lakini mawasiliano hayo yalikatika kwa muda mfupi siku ya Jumatatu.
Wanaanga hao walipopita nyuma ya mwezi, mawimbi ya redio ya mawasiliano yalizuiwa na mwezi na kukatisha mawasiliano kati ya chombo hicho na dunia,
Kwa takriban dakika 40, wanaanga hao walikuwa pekee yao, wakijawa na hisia tofauti, upweke na ukimya wakisafiri katika giza la anga.
Baada ya muda mfupi, chombo hicho cha Orion kilitokea nyuma ya mwezi na kurejesha mawasiliano na dunia tena.
Baada ya mawasiliano kurejea, kiasi kikubwa cha data iliyokuwa imekusanywa ilianza kutumwa.
Zaidi ya miaka 50 iliyopita, wanaanga wa Apollo pia walipitia hali ya upweke iliyosababishwa na kupotea kwa mawasiliano wakati wa safari yao ya mwezini. Chombo chao kilipita nyuma ya mwezi na mawasilaino yao kukatika kwa dakika 48.
Kikosi cha Artemis II
Rais wa Marekani Donald Trump alifanya mazungumzo na wanaanga hao wanne walioko kwenye chombo cha anga cha Orion wakiwa angani wakirejea duniani.
Wanaanga hao walikuwa wakizungumza kupitia kipaza sauti ambacho kilikuwa kinaelea. Trump aliwapongeza wanaanga hao kwa kuandikisha historia ya kipekee ya kuenda mbali zaidi na dunia, na kuwaalika kwenye ikulu ya white house wakisharejea ardhini.
Kikosi kilichoangani cha Artemis II kina wanaanga wanne kwenye ndani ya chombo cha Orion. Kikosi hicho kinajumuisha wanaanga watatu wa Nasa, Kamanda Reid Wiseman, Victor Glover, Christina Koch Pamoja na Jeremy Hansen wa shirika la anga la Canada.
Kikosi hicho kinatarajiwa kurejea duniani Ijumaa tarehe 10 mwezi huu wa Aprili na kutua katika bahari ya Pacific, katika pwani ya San Diego, Carlifornia, baada ya kumaliza takriban siku kumi angani.
Misheni ya Artemis II
Chombo cha anga cha Orion, kilichobeba wanaanga katika misheni ya Artemis II, kilipaa tarehe 2 mwezi Aprili.
Roketi hiyo ilirushwa kutoka Kennedy Space Center nchini Marekani.
Kila kitu kilienda kulingana na mpango wakati wa uzinduzi wa kifaa hicho.
Artemis II ilibaki katika mzunguko wa dunia kwa takriban saa 24, ambapo wanaanga walifanya ukaguzi muhimu wa chombo hicho.
Baada ya kuthibitishwa kuwa kila kitu kiko sawa, chombo hicho kilianza safari yake kuelekea mwezini.
Kutua mwezini
Artemis II haikutua kwenye mwezi.
Lengo la misheni hii ilikuwa kuweka msingi kwa ajili ya kutua mwezini katika misheni ijayo ya Artemis III.
NASA inasema kuwa uzinduzi wa Artemis III utafanyika "mapema zaidi" mwaka 2027.
Hata hivyo, wataalamu wanaamini kuwa tarehe ya mapema zaidi inayowezekana ni mwaka 2028.
Hadi sasa bado hakuna uamuzi wa mwisho umefanywa kuhusu chombo cha anga kitakachowashusha wanaanga mwezini.
Je, nchi nyingine zina mpango wa kutuma wanaanga mwezini?
Nchi nyingi pia zina malengo ya kutuma wanaanga wao kwa mwezi ifikiapo 2030. Wanaanga wa Ulaya wanatarajiwa kushiriki katika misheni ya baadaye ya Artemis, huku Japan nayo ikiwasilisha nia ya kushiriki katika misheni hiyo
China inaunda chombo chake cha anga chenye lengo la kutua kwa mara ya kwanza karibu na mwezi ifikapo mwaka wa 2030.
Urusi na India pia zimeonyesha nia ya kuwatuma wanaanga wake kwenye mwezi ifikiapo 2030.
Hata hivyo, kutokana na vikwazo vya kiuchumi, changamoto za ufadhili na changamoto za kiufundi, ratiba yao ya kuenda kwenye mwezi huenda ikapata changamoto.