Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita dhidi ya Iran vinawezaje kubadilisha sera za mataifa ya Kiarabu?
- Author, Luis Barucho
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Nchi zinazounda Baraza la Ushirikiano la Ghuba (GCC) - Saudi Arabia, UAE, Kuwait, Qatar, Oman, na Bahrain - kwa muda mrefu zimetazamwa kama nchi tulivu, zinazovutia wawekezaji, makampuni makubwa, na wafanyakazi wenye ujuzi. Viwanja vyao vya ndege ni kitovu cha shughuli za kimataifa, na miji yao imekuwa vituo vikuu vya kifedha na utalii.
Hata hivyo, vita ambavyo Marekani na Israel zinapigana dhidi ya Iran vimetikisa taswira hii, ni baada ya makombora na ndege zisizo na rubani za Iran, ambazo zinalenga kambi za kijeshi za Marekani katika eneo hilo, pia kushambulia miundombinu ya kiraia na sekta ya nishati ya eneo hilo.
Wataalamu wanaamini, licha ya uwezo wa mataifa ya Ghuba kuvumilia mashambulizi hayo, vita hivi vitaleta mabadiliko ya kimkakati.
Alex Vatanka, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati katika Taasisi ya fikra tunduizi ya Middle East Institute huko Washington, anasema: "Nchi hizi zimejikuta katika mstari wa mbele katika vita ambavyo hawakuvianzisha, lakini zinabeba gharama kubwa ya kiuchumi."
Vatanka anasema mashambulizi haya husababisha gharama kubwa za bima, ugumu wa usambazaji wa bidhaa, na yanaweza kuchochea makampuni kutathmini upya kiwango chao cha uwekezaji katika eneo la Ghuba.
Huku mataifa ya Ghuba yakitafuta kusitisha vita kati ya Marekani na Iran, moja ya matokeo ya haraka ni "marekebisho ya ushirikiano wao wa usalama na Washington," kulingana na Ebtisam Al-Ketbi, rais wa Kituo cha Sera cha Emirates.
Anasema mataifa ya Ghuba "yanasukumwa kuelekea kuwa uhusiano mkubwa zaidi na Marekani, na Israel," lakini anasisitiza kwamba ushirikiano huo utakuwa ni wa vitendo, si wa kiitikadi.”
Vatanka anasema: "Trump ameingia vitani kwa kiasi kikubwa kwa ajili ya Netanyahu, akipuuza mataifa ya Ghuba, ambayo yanatambua kuwa hayatawahi kusikilizwa sawa na Israel."
Suluhisho ni diplomasia?
Iran, kwa upande wake, inaweka shinikizo kwa mataifa ya Ghuba ili kutangaza kutoegemea upande wowote, kulingana na Vatanka.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi, alionyesha kutofurahishwa kwake na kushindwa kwa mataifa yoyote ya Ghuba kulaani mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, akiongeza kwamba Tehran inatuma ujumbe unaosema: "Lazima mjiepushe na mzozo huu."
Ingawa serikali za mataifa ya Ghuba, kulingana na Vatanka, "zina hasira sana na Iran," wakati huo huo zinajaribu kuepuka kuwa shabaha za moja kwa moja. Anasema mkakati wao unategemea kuimarisha uwezo wa kuzuia mshambulizi, huku wakiepuka kuhusika waziwazi katika vita vya Marekani na Israel.
Anaonya: "Iran inaweza kuzidisha matatizo katika nchi hizi, na hivyo kuharibu utulivu wao kwa vizazi vingi," akimaanisha hatari zinazohusiana na kulenga vifaa vya kuondoa chumvi kwenye maji na umeme.
Badr Moussa Al-Saif, afisa wa zamani wa serikali ya Kuwait, profesa msaidizi katika Chuo Kikuu cha Kuwait, na mtafiti katika kituo cha utafiti cha Uingereza, anaamini suluhisho la muda mrefu liko katika njia ya kidiplomasia.
Anasema: "Lazima tufikie uelewano na majirani zetu, tufungue njia za moja kwa moja za mazungumzo na Iran, na tubuni maono wazi ya jinsi tunavyoweza kuishi maisha yetu pamoja katika eneo hili."
Mtihani wa Kiuchumi
Mabadiliko ya mataifa ya Ghuba kutoka uchumi unaotegemea mafuta hadi huduma ni mojawapo ya mabadiliko makubwa ya kiuchumi ambayo nchi hizi zimeyashuhudia katika muongo mmoja uliopita, na wataalamu wanaonya, ingawa vita havijabadilisha mwelekeo huu, lakini vimefichua udhaifu.
Al-Kutbi anaamini mataifa ya Ghuba "yatabaki kuwa vituo vikuu vya kiuchumi, lakini chini ya masharti magumu zaidi," ikiwa ni pamoja na gharama kubwa, kuongezeka kwa bima, na ufahamu juu ya hatari iliopo.
Inaonyesha kwamba njia ya mabadiliko itategemea zaidi serikali kuliko makampuni binafsi, huku makampuni yakianza kutumia mikakati mbadala, kama vile kupeleka shughuli zao katika vituo vingine.
Al-Kutbi anatarajia kwamba, baada ya muda mrefu, nchi hizi zitajaribu kuwa na washirika wengi wa biashara, na labda kupanua uhusiano wao na China na washirika wa kikanda, ili "kuepuka kuitegemea sana" Marekani.
Badr Musa Al-Saif anakubaliana na mtazamo huu, akisisitiza kwamba nguvu ya kifedha ya eneo hilo itapunguza athari kutokana na mzozo huu, lakini bado athari zitakuwepo.
Anasema: "Uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya makombora kwenye kituo cha gesi cha Ras Laffan huko Qatar unaweza kuchukua "miaka kadhaa kutengenezwa," huku hasara ya kila mwaka ikifikia dola bilioni ishirini wakati wa kipindi cha ukarabati.
Anaongeza: "Licha kuwa tuna uwezo wa kifedha wa kukarabati. Huenda ikahitajika kupanga upya baadhi ya miradi na kupanga upya vipaumbele vya uwekezaji."
Anaamini "kwa kuzingatia hali ya sasa, kwa upande wa mfumo wa kisiasa, wingi wa fedha, wingi wa mtaji, idadi ndogo ya watu, fursa za uwekezaji bado zinapatikana kwa wingi."
Badr Moussa Al-Saif anasema kujikuta katikati ya vita si jambo jipya, akitoa mfano uvamizi wa Iraq dhidi ya Kuwait na Vita vya Ghuba mwanzoni mwa miaka ya 1990. Pia tulikuwa na matukio ya ugaidi mwanzoni mwa karne ya 21, na tulifanikiwa kushinda changamoto hii."
Anaongeza kwamba "mapema mwaka 2010 na 2011, ukikumbuka maandamano ya Waarabu katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na Ghuba, pia tuliweza kuyashinda vyema."
Kuelekea ulinzi jumuishi
Wataalamu wanaamini moja ya matokeo endelevu ya mgogoro huu ni kuwepo kwa mfumo wa ulinzi wa Ghuba uliounganishwa na ulioendelea kiteknolojia.
Al-Kutbi anatarajia uwekezaji mkubwa kufanywa katika mifumo ya ulinzi yenye tabaka nyingi, ikitegemea mitandao ya tahadhari ya mapema, ndege zisizo na rubani, na uwezo wa kimtandao.
Badr Musa Al-Saif anasema kiwango kinachohitajika cha ujumuishaji kinazidi hayo, akiongeza: "Lazima turatibu michakato ya ununuzi, kuanzisha mfumo mkuu wa usambazaji wa mifumo ya ulinzi katika nchi za Ghuba, na pia uzalishaji wa ulinzi wa ndani, hatua itayoongeza uwezo wetu wa kufanya maamuzi yetu wenyewe."
Hata hivyo, ushindani kati ya nchi unazuia kufikiwa kwa azma hii.
Fatanka anasema "baadhi ya mataifa ya Ghuba yanashindana kama vile Iran ilivyo adui kwao," jambo ambalo hufanya suala la uratibu wa ulinzi kuwa suala nyeti sana la kisiasa.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi