Je, vita dhidi ya Iran vinamnyima usingizi Kim Jong-un?

    • Author, Sangmi Han
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Kim Jong-un ni lazima amepata mawazo tata baada ya Marekani na Israel kuanzisha vita dhidi ya Iran. Korea Kaskazini ililaani mashambulizi hayo, ikiyaita "vita vya uchokozi visivyo na msingi."

Nchi hizo mbili Iran na Korea Kasakazini, zina uadui na Marekani tangu 1979 na baadaye wakaanzisha ushirikiano katika utengenezaji wa makombora.

Iran pia ndio sehemu kuu ya mauzo ya silaha za Korea, kulingana na mwanadiplomasia wa zamani wa Korea Kaskazini ambaye alizungumza na BBC kwa sharti la kutotajwa jina.

Hata hivyo, mambo mawili yanaiweka Korea Kaskazini katika nafasi nzuri zaidi kuliko Iran, kulingana na wachambuzi: silaha za nyuklia na China.

Wakati wa Vita vya Iraq vya 2003, kiongozi marehemu Kim Jong-il alitoweka kwa siku 50. Kulingana na idara ya ujasusi ya Korea Kusini, alitumia muda mwingi akijificha kwenye handaki katika eneo la Samjiyon, takriban kilomita 600 kutoka mji mkuu, Pyongyang.

Kinyume chake, mwanawe, Kim Jong-un, hakuogopa kuonekana hadharani, hata baada ya kuuawa kwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ali Khamenei.

“Hilo linaonyesha imani ya Korea Kaskazini katika nguvu zake,” anaelezea Jang Yong-seok, mkurugenzi wa zamani wa timu ya uchambuzi juu ya Korea Kaskazini katika Shirika la Kitaifa la Ujasusi la Korea Kusini.

Silaha za nyuklia

Korea Kaskazini kwa hakika ni taifa lenye silaha za nyuklia - na hata Rais wa Marekani Donald Trump alisema mwaka 2025 kwamba nchi hiyo ina "namna fulani ya nguvu za nyuklia" na "ghala kubwa la nyuklia".

Kulingana na ripoti ya 2025 ya Taasisi ya Utafiti wa Amani ya Kimataifa ya Stockholm (SIPRI), Korea Kaskazini ina takriban vichwa 50 vya nyuklia na nyenzo za kutosha kutengeneza vingine 40.

Julai 2024, Korea Kusini ilionya kwamba Korea Kaskazini ilikuwa katika "hatua za mwisho" za kutengeneza silaha za nyuklia za masafa mafupi zinazokusudiwa kutumika katika uwanja wa vita.

Mwaka jana, Rais wa Korea Kusini Lee Jae-myung pia alisema Kaskazini iko karibu kutengeneza kombora la masafa marefu linaloweza kufikia eneo la Marekani kwa kutumia kichwa cha nyuklia. Lakini madai hayo yanatiliwa shaka.

Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki la Umoja wa Mataifa (IAEA) limesema Iran ina "mitambo ya nyuklia lakini haijapata ushahidi wowote kwamba ina panga kutengeneza silaha za nyuklia."

Kufuatia makubaliano muhimu ya nyuklia ya 2015, Iran ilikubali kupunguza kurutubisha urani. Ukaguzi wa IAEA pia ilipanuliwa, jambo ambalo lilisaidia kupunguza kasi ya mpango wa nyuklia wa Iran, anaelezea Jang Ji-hyang, mtaalamu wa Mashariki ya Kati katika Taasisi ya Asan ya Uchunguzi wa Sera.

Lakini kufuatia kujiondoa kwa Marekani kutoka makubaliano ya nyuklia mwaka 2018, Iran ilianza kuizuia IAEA kufikia vituo vyake vya nyuklia. Shirika hilo lilionyesha katika ripoti yake kwamba Iran iliacha ushirikiano wote na IAEA baada ya vita na Israeli Juni 2025, Associated Press iliripoti mwezi uliopita.

Kwa upande wa Korea Kaskazini ilifanya jaribio lake la kwanza la nyuklia mwaka 2006 na, miaka mitatu baadaye, iliwafukuza wakaguzi wote wa IAEA. Imefanya majaribio mengine matano ya nyuklia tangu wakati huo, la mwisho mwaka 2017.

Wakati huo Korea Kaskazini ilikuwa na hamu ya kufanya mazungumzo na Marekani, jambo lililosababisha mikutano miwili ya kihistoria kati ya viongozi wa nchi hizo mbili mwaka 2018 na 2019. Kim Jong Un alitaka kuondolewa kwa vikwazo vya kimataifa na akakubali kubomolewa kwa mtambo wa nyuklia wa Yongbyon. Lakini Trump alitaka zaidi, na mazungumzo hayo hatimaye yalishindwa.

Korea Kaskazini sasa inaonekana kuwa na ujasiri kwa sababu vita nchini Ukraine vimeileta karibu na Urusi, ambayo inaipa ushirikiano muhimu wa kiuchumi na kijeshi, anaelezea Jenny Town, mkurugenzi wa Taasisi ya fikra tunduizi ya Stimson, huko Marekani.

Bado Trump na Kim wanaonekana kuwa na uhusiano mzuri, rais wa Marekani alimsifu mwenzake wa Korea Kaskazini mwaka jana.

Korea Kaskazini haikumkosoa Trump waziwazi ilipolaani vita dhidi ya Iran. Na katika mkutano wa chama mwezi uliopita, ilisema itadumisha uhusiano mzuri na Marekani ikiwa nchi yake itaheshimiwa, na hivyo kuacha mlango wazi kwa mazungumzo.

China, Japan na Korea Kusini

Jiografia pia inaipa unafuu Korea Kusini: Inapakana na China. Ikiwa utawala wa Korea Kaskazini utaanguka, China inaweza kukabiliwa na wimbi kubwa la wakimbizi.

Hii ndiyo sababu uhusiano kati ya nchi hizo mbili za kikomunisti ni wa karibu. Tangu 1961, China imeahidi kuilinda Korea Kaskazini iwapo kutatokea uvamizi, kupitia mkataba wa ulinzi wa pande zote mbili - mkataba pekee wa aina hiyo uliosainiwa na Beijing.

Jang Yong-seok, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Seoul, anasema: "Korea Kaskazini ina maslahi ya kimkakati kwa China ... Na China iko imara sana katika maslahi yake ya kimkakati, ambayo Kim Jong-un anayajua vyema."

Korea Kaskazini pia inazishikilia Korea Kusini na Japani kama "mateka wa nyuklia" kwa sababu ya ukaribu wao wa kijiografia, anaelezea Jang wa Taasisi ya Asan.

Korea hizo mbili zimetenganishwa tu na eneo lenye urefu wa takriban kilomita 250 na upana wa kilomita 4, huku miji yao mikuu ikiwa umbali wa takriban kilomita 200 pekee.

Hii ina maana kwamba eneo la mji mkuu wa Seoul, ambalo pia linajumuisha Incheon na Mkoa wa Gyeonggi, linaweza kufikiwa na mashambulizi ya moja kwa moja la Korea Kaskazini, anasema Jang, afisa wa zaman wa shirika la Kijasusi la Korea Kusini.

"Mtu anaweza kujiuliza: Je, Korea Kusini inaweza kuzuia makombora kama vile Israeli, Marekani au nchi nyingine za Mashariki ya Kati zinavyoweza," anaongeza.

Japani pia iko katika eneo la mashambulizi ya moja kwa moja la Korea Kaskazini, na Korea Kaskazini imekuwa ikirusha makombora mara kwa mara kwenye Bahari ya Japani wakati wa majaribio yake ya nyuklia.

Nchi hizi mbili za Asia zinahifadhi takriban wanajeshi 80,000 wa Marekani, huku takriban wanajeshi 50,000 wa Marekani wakiwa katika eneo la Mashariki ya Kati.

Vita dhidi ya Iran huenda vinaimarisha imani ya Kim Jong-un kwamba Ali Khamenei "hakuwa na nguvu kwa sababu hakuwa na silaha za nyuklia" na mazungumzo na Marekani yasingehakikisha uhai wa utawala huo, anaelezea Ellen Kim wa Taasisi ya masuala ya Uchumi ya Korea na Marekani yenye makao yake Washington.

Town anasema: "Korea Kaskazini imehangaika sana kwa miaka mingi katika harakati zake za kutafuta silaha za nyuklia, lakini katika nyakati kama hizi, Kim Jong-un ana hakika kabisa kwamba amefanya uamuzi sahihi, akijua kwamba chagua la kufanya shambulio dhidi ya nchi yenye silaha za nyuklia ni la hatari sana."

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi