Kwa nini saa ina dakika 60, na sio 100?

Muda wa kusoma: Dakika 6

Mnamo Oktoba 1793, Jamhuri mpya ya Ufaransa ilianza jaribio lililoshindwa. Iliamua kubadili namna muda unavyopimwa.

Wanamapinduzi waliamua kuwa siku igawanywe katika saa 10 badala ya 24. Kila saa ingekuwa na dakika 100 za desimali, na kila dakika ingegawanywa katika sekunde 100.

Mfumo huo ulikuwa sehemu ya kalenda mpya ya kimapinduzi iliyolenga kuleta mpangilio wa kimantiki na kuondoa athari za kidini katika mgawanyo wa mwaka, ikiwemo kuanzisha wiki ya siku 10.

Kazi ya kubadilisha saa zilizokuwepo ilianza mara moja. Majengo ya serikali yaliweka saa za desimali, na shughuli rasmi zikaanza kurekodiwa kwa kutumia mfumo huo mpya.

Hata hivyo, kulingana na Finn Burridge wa Royal Museums Greenwich nchini Uingereza, mfumo huo ulisababisha matatizo mengi. Ilikuwa vigumu sana kubadili saa zilizopo, na pia uliitenga Ufaransa na majirani zake.

Isitoshe, watu wa vijijini walipinga kupunguzwa kwa siku zao za mapumziko hadi kila siku ya kumi.

Hatimaye, mfumo wa desimali uliendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja tu kabla ya kuachwa.

Ili kuelewa kwa nini tunatumia mfumo wa sasa wa saa 24, dakika 60 kwa saa, na sekunde 60 kwa dakika, tunapaswa kurejea historia ya mwanzo kabisa wa kuhesabu muda.

Mfumo wa 60 ulianzia wapi?

Chanzo chake ni Mesopotamia, ambako waliishi Wasumeri moja wa wastaarabu wa kwanza duniani kati ya mwaka 5300 na 1940 KK.

Ubunifu wa uandishi wa nambari ulichochewa na uhitaji wa kuweka rekodi za mfumo wa kilimo unaozidi kuwa mkubwa na mgumu uliounga mkono miji yao inayokua, asema Martin Willis Monroe, mtaalamu wa tamaduni za kikabari (mifumo ya mapema zaidi ya uandishi ya Mashariki ya Kati ya kale) katika Chuo Kikuu cha New Brunswick huko Canada.

Walianza kutumia vibao vidogo vya udongo, mara nyingi vyenye ukubwa wa simu ya mkononi au hata vidogo zaidi, kuandika na kufuatilia namba, wakichora taarifa hizo kwenye udongo laini. Baadaye, alama za picha zilifuata, ambazo zilibadilika hatua kwa hatua na kuwa maandishi maarufu ya kikabari ya Wasumeri.

Haikuwa hadi katikati ya karne ya 19 ndipo vibao hivi vya udongo vilipogunduliwa na kuanza kufasiriwa.

Kwa mujibu wa Monroe, vinaonyesha kwamba Wasumeri walitumia mifumo mbalimbali ya namba, lakini mfumo muhimu zaidi kwa hisabati, na hivyo kwa unajimu na upimaji wa muda, ulikuwa ule unaoitwa mfumo wa msingi wa 60 (sexagesimal).

Kwa mujibu wa Martin Willis Monroe, walihitaji mfumo huo ili kuweka kumbukumbu za shughuli za kilimo zilizokuwa zikizidi kuwa kubwa na tata. Walitumia vibao vidogo vya udongo kuandika takwimu, ambavyo baadaye vilikuja kuwa maandishi ya kikabari.

"Kama unafanya hesabu za vitendo kama kodi au kugawa ardhi, mfumo huu ni msaada mkubwa," alisema Erica Meszaros.

Wasumeri walitumia 60 kwa namna inayofanana na jinsi sisi tunavyotumia 10 sasa. Walipofika kwenye namba tisa, walihamisha nafasi moja kuelekea kushoto, wakaandika moja, na kuongeza sifuri upande wa kulia, anaeleza Erica Meszaros, mwenye shahada ya uzamivu katika Historia ya Sayansi Sahihi na Enzi za Kale kutoka chuo kikuu cha Brown.

"Ni sawa na mfumo wa sexagesimal: wanahesabu hadi 59, na badala ya kutumia namba kubwa zaidi, hutumia tu moja, lakini katika nafasi ya chini zaidi."

Haijulikani kwa nini Wasumeri walichagua mfumo wa msingi wa 60. Baadhi ya watafiti wamependekeza kwamba mfumo huo unaweza kuwa ulitangulia hata Wasumeri wenyewe.

Hata hivyo, urahisi wake wa matumizi unaonekana wazi.

Mfumo wa 60 inaweza kugawanywa kwa 1, 2, 3, 4, 5, 6, 10, 12, 15, 20, 30 na 60 bila kuhitaji sehemu za desimali.

Kwa upande mwingine, namba 10 inaweza kugawanywa tu kwa 1, 2, 5 na 10; hivyo faida zake zinaanza kujidhihirisha.

Asili ya saa na muda

Hakuna ushahidi wazi kwamba Wasumeri walipima muda, lakini baadaye Babylon waliibua mfumo huo na kuutumia katika unajimu.

Ustaarabu wa kwanza tunaoujua uliogawa siku katika saa ulikuwa wa Wamisri wa kale, anasema Rita Gautschy wa Chuo kikuu cha Basel, na jambo hili linaonekana katika maandiko ya kidini ya karibu mwaka 2500 KK.

Vitu vya mwanzo vinavyohusiana na muda vilivyojulikana vilirejelea saa 12 za usiku: hizi zilikuwa saa za nyota zilizoegemea, zilizopatikana kwenye vifuniko vya ndani vya majeneza ya wakuu wa Misri kati ya mwaka 2100 na 1800 KK, anaeleza Gautschy.

Baadaye, Wababiloni waligawa saa katika vipande vidogo zaidi kwa ajili ya mahesabu ya anga, na hapo ndipo dhana ya dakika na sekunde ilipoanza kujitokeza.

Haijulikani kwa uhakika kwa nini Wamisri walichagua kugawa siku katika vipindi vya 12, ambavyo hatimaye vilisababisha kuwepo kwa saa 24 kwa siku.

Vifaa vya mwanzo kabisa vinavyojulikana vya kupimia muda saa za jua na saa za maji vilianza kuonekana nchini Misri karibu mwaka 1500 KK. Baadhi vilitumika katika shughuli za kila siku, lakini nyingi zilihusishwa zaidi na masuala ya kidini na ibada kuliko kupima muda, anasema Rita Gautschy.

"Kwa mtazamo wangu binafsi, naamini nyingi zilikuwa sadaka kwa miungu, zawadi za ibada," anaongeza. "Hatuna taarifa nyingi kuhusu upimaji wa muda kwa njia ya kisayansi [kutoka enzi hiyo]."

Awali, katika maandiko ya maisha ya kila siku, kipimo kidogo zaidi cha muda kilikuwa zamu ya kazi, anaeleza Gautschy, ambayo kwa kawaida ilichukuliwa kuwa ni asubuhi au mchana.

Hata hivyo, katika kipindi cha Waroma wa Misri ya kale (kuanzia mwaka 30 KK na kuendelea), saa zilianza kuwa kipimo cha kawaida, na hata vipindi vya nusu saa vikaanza kujitokeza, anaongeza.

Mfumo ulivyoendelea hadi leo

Baadaye, Wagiriki walirithi mfumo huo wa Wababiloni, na kupitia ustaarabu wa Kigiriki na baadaye Ulaya, dhana ya saa, dakika na sekunde ikaendelea hadi leo.

Ni katika karne chache zilizopita tu ndipo vifaa vya kupima muda vilipokuwa sahihi vya kutosha kufanya dakika na sekunde zitumike katika maisha ya kila siku.

Leo, saa za atomiki zimeufanya mfumo huu kuwa sahihi zaidi, na hutumika katika teknolojia kama intaneti, GPS na tafiti za kisayansi.

Kuzinduliwa kwa dakika

Wakati huo huo, Wababiloni pia walikuwa wakiendeleza matumizi yao ya saa. Hatimaye, wangekuwa wa kwanza kugawa saa katika vipimo vidogo zaidi, ingawa si kwa madhumuni ya kupima muda.

Wababiloni, waliostawi kati ya mwaka 2000 KK na 540 KK, walirithi maandishi ya kikabari pamoja na mfumo wa namba wa msingi wa 60 kutoka kwa Wasumeri. Kwa mujibu wa Erica Meszaros, kufikia mwaka 1000 KK walikuwa wamebuni kalenda iliyotegemea muda unaochukuliwa na jua kurudi katika nafasi ileile angani: zaidi kidogo ya siku 360.

Namba hii ilikuwa ya vitendo sana kwa ustaarabu uliokuwa tayari unatumia mfumo wa namba wa msingi wa 60.

"Unaona jinsi inavyolingana vizuri na mfumo wa 'sexagesimal!" anasema Meszaros. "Kwa kweli, ilielekea moja kwa moja kwenye miezi 12, kila mmoja ukiwa na siku 30," ambayo pia ililingana na mzunguko wa mwezi, anaongeza.

Wababiloni walibuni mfumo wa vitendo wa kupima muda kwa matumizi ya kila siku uliogawa mchana na usiku katika saa 12, sawa na Wamisri. Urefu wa hizi "saa za msimu" ulitofautiana kulingana na urefu wa mchana na usiku.

"Tunagawanya siku katika saa 12 kwa sababu tunagawanya anga ya usiku katika miezi 12 na ishara 12 za zodiaki," Meszaros anaeleza.

Ustaarabu mwingine mwingi wa kale ulitumia mifumo ya msimu, na ilikuwepo hadi katika Ulaya ya karne ya 15 na Japani ya karne ya 19.

Hata hivyo, Monroe anabainisha kuwa muda wa msimu haukugawanywa katika vipimo vidogo kwa matumizi ya kivitendo.

"Hili halikupata umaarufu hadi enzi za mapema za kisasa… halikuwepo Mesopotamia wala katika tamaduni nyingine za kale, kwa sababu hakukuwa na haja kubwa ya kufanya hivyo."

Kwa nini mfumo huu haukubadilika?

Ingawa mfumo wa desimali ulijaribiwa nchini France, haukufanikiwa. Uliendelea kwa miezi 17 tu kabla ya kuachwa.

Kwa mujibu wa Claude-Antoine Prieur, mfumo huo haukuwa na faida kubwa, na hata uliharibu taswira ya mifumo mingine ya vipimo vya desimali ambayo ilifanikiwa.

Kwa hiyo, mfumo wa saa 24, dakika 60 na sekunde 60 umeendelea kudumu kwa karne nyingi si kwa sababu ni kamilifu, bali kwa sababu umezoeleka sana na kubadilisha ungekuwa mgumu mno.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid