Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mzozo wa Ukraine: Jiji ambapo Makaburi ya halaiki yaligunduliwa, kuna nini nyuma yake?
Kwa mujibu wa Ukraine, siku chache baada ya mji wa Izyum uliokombolewa kutoka kwa uvamizi wa Urusi makaburi ya halaiki yaligunduliwa nje kidogo ya jiji hilo.
Misalaba iliyoandikwa namba ilipatikana msituni nje ya jiji hilo huku vikosi vya Ukraine vikiendelea kusonga mbele. Kwa mujibu wa viongozi wa Ukraine, litafanyika zoezi la kufukua miili iliyokutwa makaburini kuanzia Ijumaa na kuanza utaratibu wa kuchunguza chanzo cha vifo vyao.
Bado haijabainika nini kimewaua watu hao, lakini uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa huenda wengine walifariki kutokana na shambulio la bomu na ukosefu wa huduma za afya.
Siku ya Ijumaa, mkuu wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi ya Ukraine alisema kuwa miili hii mingi ilikuwa ya raia wa kawaida.
Mamlaka zinasemaje?
Ihor Klimenko aliuambia mkutano na waandishi wa habari kwamba hapo awali ilishukiwa kuwa miili ya baadhi ya wanajeshi huenda ilizikwa hapa, lakini hakuna mwili wa mwanajeshi ambao umepatikana mpaka sasa.
Maafisa waliambia BBC kuwa zaidi ya miili 400 huenda ilizikwa katika eneo hilo. Umoja wa Mataifa ulitarajia kutuma timu ya ufuatiliaji mjini humo katika siku chache zijazo.
Msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu amesema watajaribu kubaini iwapo miili hiyo ni ya raia au wanajeshi. Mbali na hili, watachunguza kubaini sababu za vifo vyao. Jiji la Izume lilishambuliwa katika siku za mwanzo za vita ya Ukraine. Jiji hilo lilitumika kama kituo cha usambazaji cha jeshi la Urusi katika eneo la mashariki mwa Ukraine.
EU yataka Urusi iwajibishwe kwa uhalifu
Ofisi ya rais wa Umoja wa Ulaya imetoa wito wa kuundwa kwa mahakama ya kimataifa kuhusu uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.
Wito huo kutoka Jamhuri ya Czech ambayo kwa sasa inashikilia urais wa zamu wa umoja huo, umekuja baada ya kugunduliwa kwa mamia ya makaburi hayo huko Izyum, mji uliokombolewa hivi karibuni na wanajeshi wa Ukraine.
Wengi wanasemekana kuwa raia, wanawake na watoto miongoni mwao.
"Tunasimamia adhabu ya wahalifu wote wa vita," Waziri wa Mambo ya Nje wa Czech Jan Lipavsky alisema.
Hotuba ya Rais Zalenskyi wa Ukraine
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyi alisema katika hotuba yake ya usiku kwamba "hatua za lazima za kiutaratibu" zimeanza kuchukuliwa katika eneo hilo.
Alisema, "Tunataka kuuambia ulimwengu kile kinachotokea na pia kuhusu hali ambayo uvamizi wa Urusi umesababisha.
Bucha, Mariupol na sasa Izume... Urusi imeacha njia ya vifo vingi." "Na inapaswa kuwajibika kwa hili." Katika hotuba hii, alikumbuka makaburi ya halaiki yaliyopatikana hapo awali huko Bucha na Mariupol karibu na Kiev, mji mkuu wa Ukraine.
Andriy Yermak, mkuu wa ofisi ya Rais Zelensky, aliandika katika mtandao wa twitter na kuchapisha picha za madai ya makaburi ya halaiki.
Jambo la kushangaza vikosi vya Urusi vililazimika kurudi nyuma mapema mwezi huu baada ya shambulio la kivita la jeshi la Ukraine lililopelekea ukombozi wa baadhi ya miji katika mikoa ya Izum na Kharkiv.
Kulingana na Ukraine, Jeshi la Urusi limetekeleza uhalifu wa kivita karibu 21,000, ikiwa ni pamoja na vifo na ubakaji wa raia. Yote ilianza wakati Rais wa Urusi Vladimir Putin alipoamuru uvamizi kamili wa Ukraine mnamo Februari 24.