Zijue njia kuu nane za majini ambazo ni muhimu zaidi duniani

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mchoro wa tarehe 17 Novemba, 1869, wa sherehe ya ufunguzi wa Mfereji wa Suez huko Port Said.
    • Author, Walid Badran
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Milango na njia za bahari, ni miongoni mwa maeneo muhimu ya kijiografia ambayo huunda historia ya biashara ya kimataifa na kuchangia katika kuunda uhusiano wa kimataifa kwa karne nyingi. Njia hizi sio tu zinarahisisha kupita kwa meli, pia zinawakilisha udhibiti wa nishati na bidhaa kati ya mabara.

Kutokana naa utegemezi wa biashara ya baharini kama njia kuu ya kusafirisha bidhaa, umuhimu wa njia hizi za maji umeongezeka, na kuwa vitovu muhimu katika mfumo wa uchumi wa dunia.

Njia hizi za maji zina jukumu muhimu katika kuunganisha bahari na bahari, kupunguza umbali wa bahari na kufupisha muda na gharama. Badala ya kusafiri kwa meli kuzunguka mabara, mifereji na njia nyembamba za majini hupunguza bei za bidhaa na kurahisisha minyororo ya usambazaji wa kimataifa.

Kwa hivyo, usumbufu wowote katika mojawapo ya njia hizi za maji unaweza kusababisha usumbufu mkubwa katika masoko ya kimataifa.

Umuhimu wa mifereji na njia hizi hauishii tu katika uchumi, pia unaashiria nguvu za kisiasa na kijeshi, kwani vita na migogoro imetokea kutokana na njia hizi.

Mlango-Bahari wa Hormuz

Mlango-Bahari wa Hormuz upo kati ya Iran na Usultani wa Oman, ni mojawapo ya njia muhimu zaidi za baharini duniani kutokana na eneo lake la kijiografia linalounganisha Ghuba na Bahari ya Hindi. Eneo hili ni muhimu kwa usafiri kwa meli za mafuta zinazotoka nchi za Ghuba kuelekea masoko ya kimataifa.

Umuhimu wa njia hiyo unatokana na ukweli kwamba zaidi ya asilimia 20 ya usambazaji wa mafuta duniani hupitia hapo. Na usumbufu wowote unaotokea unaweza kusababisha shida katika bei za mafuta duniani.

Walinzi wa Mapinduzi ya Iran hivi karibuni walitangaza Mlango-Bahari umefungwa kwa meli, hasa zile zinazohusiana na Marekani na Israel, kujibu moja kwa moja mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran yaliyoanza Februari 2026.

Mfereji wa Suez

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mfereji wa Suez nchini Misri ni mojawapo ya njia muhimu ya maji duniani, kwani unaunganisha Bahari ya Shamu na Bahari ya Mediterania, na ndio njia ya mkato kati ya Ulaya na Asia bila kulazimika kuzunguka bara la Afrika.

Mfereji huo una jukumu muhimu katika biashara ya kimataifa, hasa meli za mafuta na gesi, na ni chanzo kikuu cha mapato ya taifa la Misri.

Kazi ya kuchimba Mfereji wa Suez ilianza mwaka 1859 wakati wa utawala wa gavana wa Misri, Said Pasha, ambaye alitoa kibali cha kuchimba, kwa kampuni ya Ufaransa iliyoongozwa na Ferdinand de Lesseps.

Mradi huo uliendelea kwa takriban miaka 10 hadi mfereji huo ulipofunguliwa rasmi Novemba 17, 1869, wakati wa utawala wa Khedive Ismail, katika sherehe kubwa ya kimataifa ya kuunganisha Bahari ya Shamu na Bahari ya Mediterania.

Uamuzi wa Rais wa Misri Gamal Abdel Nasser 1956 wa kutaifisha mfereji huo ulisababisha mashambulizi dhidi ya Misri 1956, ambapo Uingereza, Ufaransa na Israeli zilishiriki, katika jaribio la kudhibiti mfereji huo.

Mgogoro huo uliisha kwa kujiondoa kwa vikosi vya Israel, Uingereza na Ufaransa chini ya shinikizo la kimataifa, huku mfereji ukibaki chini ya mamlaka ya Misri.

Mfereji huo baadaye ulifungwa kutokana na vita vya Waarabu na Israel, wakati wa vita vya 1967 na kubaki umefungwa kwa miaka mingi, hasa baada ya kuwa eneo la mapambano ya moja kwa moja, kabla ya kufunguliwa tena mwaka 1975 baada ya kumalizika kwa Vita vya Oktoba vya 1973.

Mlango wa Bab el-Mandeb

Mlango-Bab el-Mandeb unaunganisha Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden, na uko kati ya Yemen, Djibouti na Eritrea. Ni lango la kusini kuelekea Mfereji wa Suez, una umuhimu wa kipekee katika biashara ya kimataifa.

Sehemu kubwa ya meli zinazosafiri kati ya Asia na Ulaya hupita, na kuifanya kuwa sehemu muhimu ya usafiri katika minyororo ya usambazaji wa kimataifa.

Hata hivyo, mlango bahari huo unakabiliwa na changamoto za kiusalama kutokana na mvutano katika Pembe ya Afrika na Yemen, na kuufanya uwe katika hatari. Kwa hivyo, mataifa yenye nguvu duniani yana nia ya kuhakikisha unabaki kuwa wazi.

Huko nyuma, vitisho vilivyotolewa na Wahouthi nchini Yemen, washirika wa Iran, vilisababisha usumbufu mkubwa katika usafirishaji wa meli na kuongezeka kwa gharama za bima ya baharini.

Kujibu vitisho hivyo, nchi kadhaa za Ulaya ziliunda kikosi cha kimataifa cha majini kinachojulikana kama Operesheni Aspidis, kwa lengo la kulinda meli za kibiashara na kuhakikisha uhuru wa katika Bahari Shamu na Bab al-Mandab.

Opresheni zao zinahusu kusindikiza meli, kufuatilia na kukabiliana na vitisho, na hivyo kuimarisha usalama wa ukanda huu muhimu na kupunguza athari za kuharibu biashara ya kimataifa.

Mlango-Bahari wa Gibraltar

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Picha ya setilaiti ya Mlango-Bahari wa Gibraltar, huku Uhispania ikiwa kaskazini na Morocco ikiwa kusini.

Mlango-Bahari wa Gibraltar uko kati ya kaskazini mwa Morocco na kusini mwa Uhispania, huku eneo la Gibraltar linalodhibitiwa na Uingereza likiwa upande wake wa Ulaya, na kuipa Uingereza uwepo wa kimkakati katika njia hii muhimu ya bahari inayounganisha Bahari ya Mediterania na Bahari ya Atlantiki.

Umuhimu wake unatokana na kuwa njia muhimu ya usafiri wa meli kati ya Ulaya, Afrika na Amerika, na kuifanya kuwa kitovu cha biashara ya kimataifa, na kuchangia kuunganisha masoko mengi kupitia njia moja ya baharini.

Mlango huo pia una umuhimu wa kijeshi na kisiasa, kutokana na ukaribu wake na bara la Ulaya. Miongoni mwa migogoro maarufu zaidi iliyoshuhudiwa ni ile iliyohusiana na uhasama wa kikoloni kwa karne nyingi kati ya mataifa makubwa ya Ulaya, hasa Uingereza na Hispania.

Migogoro ya mara kwa mara pia imeibuka kati ya Morocco na Uhispania kuhusu baadhi ya visiwa vidogo karibu na Mlango-Bahari, kama vile Kisiwa cha Leila (Tora). Ingawa migogoro hii haijageuka kuwa mapigano makubwa katika enzi ya sasa.

Mfereji wa Panama

Mfereji wa Panama upo Panama na unaunganisha Bahari ya Karibi (ambayo ni Bahari ya Atlantiki) na Bahari ya Pasifiki, na hivyo kufupisha njia ya bahari kati ya mashariki na magharibi mwa dunia.

Mfereji huo unachukuliwa kuwa mojawapo ya mafanikio makubwa zaidi ya uhandisi, kwani unategemea mfumo wa uhandisi wa kuinua na kushusha meli, kuruhusu meli kubwa kupita kati ya bahari hizo mbili kwa ufanisi mkubwa, na umechangia kupunguza kwa kiasi kikubwa muda wa safari za baharini na gharama za usafiri.

Mfereji huu una jukumu muhimu katika biashara ya kimataifa, hasa katika usafirishaji wa bidhaa kati ya Amerika na Asia, na umefanyiwa upanuzi wa hivi karibuni ili kuongeza uwezo wake wa kuendana na ukuaji wa kiasi cha biashara ya kimataifa.

Kazi ya kuchimba Mfereji wa Panama ilianza mwaka 1881 kupitia mpango wa Ufaransa ulioongozwa na Ferdinand de Lesseps, wakati ambapo Panama ilikuwa sehemu ya Colombia. Hata hivyo, mradi huo ulikwama na kusimama, kabla ya Marekani kuuanza tena baadaye baada ya kuunga mkono kujitenga kwa Panama na Colombia mwaka wa 1903.

Mfereji huo ulikamilishwa na kufunguliwa rasmi Agosti 15, 1914, wakati wa urais wa Woodrow Wilson. Rais wa Panama wakati huo alikuwa Belisario Porras Barahona, ambaye alichukua madaraka kati ya 1912 na 1916.

Baada ya kufunguliwa kwake, Mfereji wa Panama ulikuwa chini ya usimamizi na udhibiti wa Marekani kwa miongo kadhaa, jambo ambalo lilisababisha mvutano wa ndani na maandamano makubwa huko Panama, hasa matukio ya mwaka 1964, ambayo yalishuhudia mapigano ya umwagaji damu kati ya Wapanama na vikosi vya Marekani.

Katika miaka ya 1970, makubaliano yalifikiwa ya kuipa Panama umiliki, yalifikiwa rasmi mwaka 1999. Licha ya kumalizika kwa mzozo wa uhuru, mfereji bado unakabiliwa na changamoto za kisiasa na kiuchumi, ambazo wakati mwingine huathiri shughuli zake.

Rais wa Marekani Donald Trump alikosoa kuipa Panama udhibiti wa mfereji huo, akisema ni uamuzi mbaya kwa upande wa Marekani.

Mlango-Bahari wa Malacca

Chanzo cha picha, Getty Images

Mlango-Bahari wa Malacca, uliopo kati ya Malaysia na Indonesia, ni mojawapo ya njia za bahari zenye shughuli nyingi zaidi duniani, zinazounganisha Bahari ya Hindi na Bahari ya Kusini ya China. Mlango-bahari huu ndio njia kuu ya meli za kibiashara kati ya Mashariki ya Kati na Asia Mashariki.

Umuhimu wake unaonekana wazi kwani ni njia fupi zaidi ya kusafirisha mafuta na bidhaa kwenda nchi kubwa kama vile China na Japani, na kuifanya kuwa sehemu muhimu katika minyororo ya usambazaji duniani, na nchi nyingi huitegemea njia hii ili kuhakikisha mtiririko endelevu wa malighafi na nishati.

Licha ya umuhimu wake kiuchumi, Mlango-Bahari wa Malacca unakabiliwa na changamoto za kiusalama kama vile uharamia wa baharini na msongamano mkubwa.

Mojawapo ya changamoto kubwa zilizoshuhudiwa ilikuwa kuenea kwa uharamia wa baharini mwanzoni kati ya 2000 na 2005, wakati meli za kibiashara ziliposhambuliwa mara kwa mara katika baadhi ya maeneo nyeti ya mlango bahari, jambo ambalo lilizifanya nchi katika eneo hilo kama vile Malaysia, Indonesia na Singapore kuimarisha ushirikiano wa usalama na kufanya doria za pamoja.

Mlango wa Bosphorus na Dardanelles

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Picha ya setilaiti ya Bosphorus (kaskazini) na Dardanelles (kusini) huko Türkiye

Mlango-Bahari wa Bosphorus upo Istanbul, ndani ya Türkiye, na hutenganisha mabara ya Asia na Ulaya. Unaunganisha Bahari Nyeusi na Bahari ya Marmara.

Mlango huo una jukumu muhimu katika kusafirisha mafuta, gesi na bidhaa kutoka nchi za Bahari Nyeusi hadi masoko ya kimataifa. Pia ni njia kuu ya meli za kibiashara na kijeshi, na Uturuki ina udhibiti wa shughuli za hapa kulingana na makubaliano ya kimataifa.

Mlango-Bahari wa Dardanelles pia upo ndani ya Uturuki na unaunganisha Bahari ya Aegean (ambayo ni sehemu ya Bahari ya Mediterania) na Bahari ya Marmara nchini Uturuki.

Mlango bahari wa Uturuki ulishuhudia mgogoro wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia, wakati vikosi vya Washirika vilipojaribu kukamata mlango bahari ili kufungua njia ya baharini kuelekea Urusi ya Tsarist, lakini vikosi vya Ottoman viliweza kurudisha nyuma shambulio hilo katika moja ya vita vikali zaidi vya vita hivyo.

Mfereji wa Kil

Chanzo cha picha, Getty Images

Mfereji wa Kiel upo kaskazini mwa Ujerumani ndani ya jimbo la Schleswig-Holstein, na unaunganisha Bahari ya Baltiki na Bahari ya Kaskazini, na kutoa njia fupi ya baharini kwa meli za Ulaya.

Mfereji huo hutumika sana katika usafirishaji wa baharini ndani ya Ulaya, haswa kati ya bandari na viwanda, na kuufanya kuwa muhimu katika kusaidia uchumi wa Ulaya na kurahisisha biashara ya ndani.

Mradi wa uchimbaji wa Mfereji wa Kiel ulianza mwaka 1887 wakati wa utawala wa marehemu Kaiser Wilhelm I, na ulikamilishwa na kufunguliwa rasmi mwaka 1895 wakati wa utawala wa Kaiser Wilhelm II, ambaye alisimamia uzinduzi wake.

Mfereji huo ulipata umuhimu mkubwa wa kijeshi wakati wa vita viwili vya dunia kama njia muhimu kwa meli za majini za Ujerumani, na kuufanya kuwa shabaha ya vikosi vya adui vilivyotaka kuvuruga matumizi yake kupitia mabomu au vizuizi.

Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, mfereji huo uliwekwa chini ya vikwazo vya kimataifa chini ya Mkataba wa Versailles, ambao uliamuru ufunguliwe na hivyo kupunguza udhibiti wa Wajerumani.

Baadaye, mfereji huo ulirudi katika uhuru kamili wa Ujerumani, lakini ulibaki chini ya macho ya Ulaya kutokana na umuhimu wake katika mizani ya baharini, hasa wakati wa Vita Baridi.