Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mzozo wa Ukraine: Majeshi ya Urusi kurudi nyuma ni ishara ya udhaifu?
Kuondoka kwa majeshi ya Urusi kutoka Kharkiv, kaskazini-mashariki mwa Ukraine, kunadaiwa kumefichua udhaifu mkubwa katika mgawanyo na utumishi wa wanajeshi wa taifa hilo, maveterani wa Urusi na wanamtandao wa kijeshi wanasema.
"Hujui jinsi ninavyochoka kumsalimia mtu asubuhi na kisha kutambua mabaki yake baadaye siku hiyo hiyo," afisa mmoja wa Urusi anayehudumu kama askari wa majini huko Ukraine aliripotiwa kumwambia mfanyakazi mwenzake wa zamani kwa njia ya simu, ambaye alituma kwenye wake wa Telegram.
"Juzi tu vikosi vyangu viwili vya walenga shabaha ama wadunguaji vilishambuliwa vibaya na vifaru. Watu watatu walikufa papo hapo, wa nne alipigania maisha yake kwa muda wa saa moja na nusu, mwingine akiwa katika hali mbaya alipelekwa hospitalini.
Wakati maofisa wa Urusi na vyombo vya habari vya serikali vinajaribu kuzizima taarifa kuwa vikosi vya Urusi vimeondoka huko Kharkiv, waandishi wa habari za vita, maveterani na wanamtandao wa kijeshi wenye ushawishi wanakubaliana na taarifa za kuondoka kwa vikosi licha ya changamoto nyingi za kuzuia usambazaji wa taarifa za aina hiyo.
Mitandao kadhaa inaeleza Jeshi la Urusi linakabiliwa na uhaba wa vifaa na wafanyakazi, vinavyochangia kuwepo kwa utendaji mgumu vitani. Muda mfupi baada ya kurudishwa kutoka vitani Ukraine, baadhi ya wanajeshi wa taifa hilo wanadaiwa kueleza namna ambavyo hata kupeleka ndege ndogo isiyo na rubani kunahitaji kuidhinishwa na afisa mkuu au jenerali, na hivyo kupunguza kasi ya uelewa wa nafasi za adui.
Kupitia akaunti moja ya Telegram, inayodaiwa kuendeshwa na mkongwe wa kikosi maalum cha Urusi, kimeweka picha ya mwanajeshi wa Urusi akiwa amevalia kitambaa cha mkono kilichonakshiwa kwa maneno: "Hakuna mpinzani mbaya zaidi kuliko kamanda wako mwenyewe ambaye ni ..." akitumia maneno ya dharau kumuelezea.
Hofu si tu kuhusu uongozi mbaya. Vifaa vya kimsingi bya vita vinaonekana kuwa na uhaba mkubwa kiasi kwamba imebidi watu wengi kujitokeza kusaidia kufadhili. Makundi mengi ya mitandao ya kijamii yanakusanya pesa kununua vifaa- kuanzia ndege zisizo na rubani hadi soksi na chupi.
Kundi moja wapo linaloitwa "The People's Front", linasema limechangisha takriban ruble 1.5bn (£15m, $17m) katika kipindi cha miezi mitatu tu iliyopita, na tayari imetumika kununua sare, helmeti na jaketi za kubana, vifaa vya huduma ya kwanza kwanza pamoja na darubini.
Lakini suala si tu ukosefu wa vifaa, pia ukosefu wa askari. Ingawa hakuna dalili za kukaribia kuajiriwa kwa lazima, kumekuwa na msukumo wa kuajiriwa - unaoelezewa na serikali kama "uhamasishaji usio rasmi" - tangu baada ya uvamizi wa nchi hiyo nchini Ukraine.
Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilianza kuweka matangazo kwenye tovuti maarufu za kazi mapema mwezi Machi, jambo ambalo lilifanywa mara chache kabla ya vita. Kwenye tovuti moja kuna nafasi zaidi ya 7,000 za kijeshi zilizoorodheshwa - kwa wapiganaji wa kutumia bunduki na wafanyakazi wengine wenye majukumu mengine yanayolenga mapigano. Hakuna matangazo yanayotaja "operesheni maalum ya kijeshi" nchini Ukraine.
Vipeperushi vya ajira pia vimebandikwa kwenye milango ya nyumba, kwenye usafiri wa umma na nje ya vyumba vya makazi na hata hospitali za magonjwa ya akili.
Pengine katika namna ya kuwavutia watu zaidi, urefu wa mkataba umepunguzwa kutoka miaka mitatu hadi miezi mitatu, na kikomo cha umri wa juu kwa mkataba wa kwanza umeongezwa kutoka miaka 40 hadi 60.
Mishahara ya kila mwezi inayotangazwa ni kati ya rubles 100,000-450,000 (£1,000-£4,500, $1,139-$5,125) - licha ya hatari ya kazi yenyewe vitani, pendekezo hili la mishahara mikubwa ni kuwavutia zaidii wale wasio na kazi ama kutarajia kupata kazi katika maeneo duni ya kiuchumi nchini.
Urusi inaaminika kutuma Ukraine vikosi vikivyoundwa kwa namna hii kila baada ya siku 10, kufuatia mafunzo ya wiki moja au chini ya hapo.
Kuna ripoti kwamba wale wanaosaini mikataba ya kwenda vitani sio wote wanafanya hivyo kwa hiari. Wanaharakati wa haki za binadamu wa Urusi wanadai kumekuwa na visa vya wanaume nchini Chechnya kushinikizwa kujiunga na jeshi kwa nguvu na mamlaka.
Waandishi wa habari huru wa Urusi wameripoti kuwa hadi wafungwa 500 pia wameandikishwa kwenda vitani. Mfungwa mmoja, Konstantin Tulinov, alisifiwa katika vyombo vya habari vya serikali baada ya kuuawa wakati wa vita mwezi Julai. Tulinov alikuwa ametumikia vifungo vingi kwa kuwatesa wafungwa katika magereza ya Urusi.
Wakati changamoto hizi zinajadiliwa ndani ya makundi ya mtandao, hakujawa na uthibitisho rasmi kwamba ni kweli majeshi ya Urusi yamerudi nyuma.