Slowjamastan: Taifa jipya nchini Marekani

Chanzo cha picha, Slowjamastan Ministry of Propaganda
Zaidi ya watu elfu 25,000, wamejitangaza kuwa raia na kumfuata kiongozi bandia wa kiimla wa eneo ambalo limepiga marufuku kuvaa viatu aina ya "crocs" na kutuma barua pepe na kubofya "reply all".
Kati ya mashamba za tende katika bonde la Coachella, California hadi mpaka wa Mexico, kuna eneo kavu la jangwa lenye rangi ya kahawia lenya upana mrefu, eneo hili kame halina makazi ya watu, na limejaa vichaka.
Hii ni Jamhuri ya Slowjamastan, taifa bandia lililo changa zaidi duniani ukubwa wake ukiwa takriban ekari 11.
Katika "nchi" hii, viatu aina ya "Crocs" zimepigwa marufuku kikatiba. Barua pepe za "reply-all" zimeharamishwa kisheria. Kuendesha gari kwa kasi kunaruhusiwa, lakini tu ikiwa unakimbia kurudi nyumbani kula chakula aina ya "tacos".
Kiongozi wa eneo hili ni Randy Williams anayejulikana pia kama "Sultan wa Slowjamastan". Kando na raia elfu 25,000 anaowatala, pia ni mkurugenzi wa programu katika kituo cha redio cha Z90 na Magic 92.5 mjini San Diego, na anajulikana kwenye redio kama "R Dub".
Tangu mwaka 1994, pia amekuwa akiendesha kipindi cha redio kinachoitwa Sunday Night Slow Jams, ambacho husambazwa katika zaidi ya vituo 250 kote duniani.

Chanzo cha picha, Slowjamastan Ministry of Propaganda
Williams ametumia miaka mingi kuzuru mataifa yanayotambuliwa na Umoja wa Mataifa.Mwanzoni mwa mwaka wa 2020, alikuwa amebakisha safari moja tu ya mwisho. Kisha dunia ikakumbwa na janga la dunia la Covid 19.
Akiwa amekwama nyumbani kama watu wengine wote wakati wa janga la COVID-19, Williams alijikuta hana pa kwenda huku akiwa na muda mwingi wa ziada. Hapo ndipo wazo likamjia, "Ikiwa siwezi kutembelea nchi nyingine, kwa nini nisiunde yangu?"
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Jinsi ya kuwa dikteta bandia.
"Nilipokuwa mtoto, nilipenda kufanya vitu vya ubunifu, iwe ni uandishi wa hadithi, kuchora, kutengeneza picha au miradi ya shule. Hivyo hili lilionekana kama mradi wa mwisho kabisa wa ubunifu," Sultan alisema wakati wa ziara katika "balozi" yake ambapo huhifadhi propaganda kutoka kwa madikteta halisi wa duniani kote.
Alipomuelezea rafiki yake, Mark Corona, alichokuwa nacho akilini,Corona alicheka. "Kitu pekee nilichofikiria kilikuwa sehemu ya filamu ya Family Guy ambapo Peter alianzisha nchi yake, Petoria," Corona alisema.
Williams hakukata tamaa. Aliendelea kutafuta, akipitia tovuti tofauti akitafuta eneo lenye sifa maalum. Alihitaji ardhi zaidi ya ekari tano, karibu na barabara na iwe eneo ambalo anaweza kufika na gari kutoka San Diego.
Hatimaye, alikuta kipande kimoja cha ardhi kilichokidhi vigezo vyake. Kilikuwa kipande cha ardhi ambacho hakijaendelezwa, kilichojaa mchanga, vichaka na mawe, na kilichokuwa kikiuzwa kwa dola 19,500.
"Nilipapenda kwa mara ya kwanza," Alisema Williams. Aliinunua ardhi hiyo mwaka 2021.

Chanzo cha picha, Slowjamastan Ministry of Propaganda
Williams alimwomba Corona asafirishe dawati linalofanana na la rais kutoka Phoenix na kukileta Kusini mwa California. Walipolishusha katikati ya ardhi hiyo iliopo jangwani, walianza "kuweka mipaka la eneo lao," wakasimamisha mabango kando ya barabara ya jimbo la California 78 yaliyotangaza taifa lao jipya: "Jamhuri ya Slowjamastan" jina ambalo awali Williams alikuwa amelitoa kama mzaha, lakini likabaki rasmi.
Haikuchukua muda mrefu kwa mamlaka za eneo hilo kuligundua. Mabango hayo yalipewa onyo kwa kuwekwa karibu na barabara. Williams akayahamisha kidogo ili yaendane na sheria za kaunti, huku bado yakitangaza kwa fahari taifa lake jipya
"Watu walikuwa wakipita na kujiuliza ni nini kinaendelea hapa," Corona alisema. "Labda walidhani sisi ni magaidi, na hilo lilichochea hamasa ya kutaka kujua zaidi."
Lakini lile bango la kando ya barabara lilikuwa mwanzo tu. Kwanza ikaja kituo cha ukaguzi wa mpaka kilichotengenezwa kwa muda. Kisha zikafuata bendera na pasi za kusafiria kisha Jamhuri ya Slowjamastan ikaanza kufanana na nchi halisi.
"Ghafla nilijikuta nikinunua magari ya polisi, sarafu za nchi na vibanda vya uhamiaji," alisema Williams.

Chanzo cha picha, Slowjamastan Ministry of Propaganda
Williams alijitangaza kama Sultan na akaanza kuvaa hivyo, pamoja na miwani na mapambo ya kifahari ambayo yeye mwenyewe anakiri yanamkumbusha mtindo wa kijeshi wa kiongozi wa kidikteta wa Libya, Muammar Gaddafi.
Miaka mitano baadaye, Slowjamastan sasa inatoa pasi za kusafiria kwa wageni wanaotaka kuwa "raia wasio rasmi," inatengeneza sarafu yake, na kufanya sherehe za kupandisha bendera. Ardhi hiyo imegawanywa katika majimbo, ikiwa ni pamoja na Dublândia, Bucksylvania na Queendom ya Hotdamnastan.
Sultan hata aliandika wimbo wa taifa unaoitwa Slowjamastan (I Think It's Going to Be an Awesome Place) uliotungwa kwa tuni ya wimbo wa Elton John Rocket Man.
Kwa wale wanaotaka kuhalalisha kushiriki kwao, wanaweza kupewa vyeo kwa kulipia ada.

Chanzo cha picha, Slowjamastan Ministry of Propaganda
Raia wa Slowjastaman pia hukutana ana kwa ana. Sherehe mbalimbali, kama uzinduzi wa "meli ya kwanza ya jeshi la majini" ya taifa hilo iitwayo SS Badassin iliyoundwa "kulinda ardhi dhidi ya uhalifu wowote"
Hata hivyo, uraia kamili unapatikana kupitia fomu ya mtandaoni.
Kwa mujibu wa Sultan, watu huenda Slowjamastan kwa sababu tofauti tofauti. Wengine wana hamu ya kujua, wengine wanaburudika tu, na wengine wanatafuta tu kupumzika kutoka kwa dunia ya kawaida.

Chanzo cha picha, Slowjamastan Ministry of Propaganda
Katika kipindi ambapo idadi inayoongezeka ya Wamarekani wanazidi kuchoshwa na siasa za nchi yao na kuanza kutafuta pasipoti za nchi nyingine, Williams anasema raia wa Marekani wanaunda takriban asilimia 50 ya raia wa Slowjamastan. Sultan alieleza kuwa ukuaji wa nchi hiyo si wa kisiasa bali ni wa kimataifa; ongezeko la hivi karibuni la waombaji kutoka Bangladesh ni ushahidi kwamba mvuto wa Slowjamastan "hauna mipaka," alisema.
Stephanie Heddon alisikia kuhusu Slowjamastan kwa mara ya kwanza wakati mshiriki mmoja alitaja nchi hiyo kwenye kipindi cha Jeopardy!. Baadaye, alimtafuta Williams kwenye Maonesho ya Usafiri na Vituko ya Long Beach.
"Ninataka kumshukuru Sultan kwa furaha aliyoileta katika maisha yangu," alisema Heddon, ambaye sasa ni raia. Kwa upande wake, furaha hiyo huja kupitia kushiriki na machapisho ya mara kwa mara ya micronation hiyo kwenye mitandao ya kijamii, ambayo yanajumuisha kila kitu kuanzia maonyo ya kuchekesha kuhusu sheria za kipekee za nchi hiyo hadi raia wapya wakijivunia pasi zao za Slowjamastan. "Kila kitu kuhusu hii hunifanya niwe na furaha. Na nadhani maelfu na maelfu ya raia wengine wa Slowjamastan wangekubaliana nami. Huu ni wakati mgumu sana kwa sisi sote [nchini Marekani], lakini hapa kuna kitu cha kufurahisha."
Kutoka jangwa hadi jukwaa la dunia
Inakadiriwa kuwa kuna mamia ya micronations duniani kote. Baadhi ziko katikati ya maji ya kimataifa, nyingine zipo katika vitongoji tulivu vya miji. Mwaka ujao, Slowjamastan itakuwa mwenyeji wa MicroCon 2027, mkutano wa micronations. Wajumbe kutoka zaidi ya majimbo 43 ya kujitangaza, kuanzia Jamhuri ya Bomber hadi Dragon Isle, watakutana kujadili masuala kuanzia uhuru wa kisiasa hadi kubuni nembo za taifa.
Kama tovuti ya tukio hilo inavyosema: "Hii ni cosplay ikichanganyika na uundaji wa dola."

Chanzo cha picha, Slowjamastan Ministry of Propaganda
Ingawa Sultan anasema wageni wanakaribishwa katika eneo hilo la jangwa la Slowjamastan, kwa sasa hakuna sehemu ya kulala kwa wageni wanaotaka kukaa usiku.














