Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ifahamu hali ya kukaza misuli inayomkumba Celine Dion
Celine Dion amefichua kuwa amegunduliwa na hali inayoitwa Stiff Person Syndrome (SPS), hali adimu wa neva wenye sifa za ugonjwa wa autoimmune.
Mwimbaji huyo wa Kifaransa wa Canada aliwaambia wafuasi wake milioni 5.2 wa Instagram hali hiyo inamfanya misuli yake ikaze bila kudhibitiwa. Pia imemfanya kuwa na ugumu wa kutembea na kuimba, alisema, akimaanisha kuwa hataweza kushiriki maonesho yaliyopangwa nchini Uingereza na Ulaya mwaka ujao.
"Nimekuwa nikikabiliana na matatizo ya afya yangu kwa muda mrefu," Dion alisema. "Na imekuwa vigumu kwangu kukabiliana na changamoto hizi na kuzungumza kuhusu kila kitu ambacho nimekuwa nikipitia," mwanamama huyo mwenye umri wa miaka 54 aliendelea kueleza katika video iliyojaa hisia.
"Hivi karibuni nimegunduliwa kuwa na ugonjwa wa nadra sana wa neva unaoitwa stiff person syndrome ambao huathiri mtu mmoja kati ya milioni.
"Wakati bado tunajifunza kuhusu hali hii adimu, sasa tunajua hii ndiyo imekuwa ikisababisha mifadhaiko yote ambayo nimekuwa nayo." Aliongeza: "Kwa bahati mbaya, kukaza huku kunaathiri kila nyanja ya maisha yangu ya kila siku, wakati mwingine husababisha ugumu ninapotembea na kutoniruhusu kutumia sauti zangu kuimba jinsi nilivyozoea.
"Inaniuma kukwambia leo kwamba hii inamaanisha kuwa sitakuwa tayari kuanza tena ziara yangu huko Ulaya mwezi Februari."
Mnamo mwaka wa 2014, diva - ambaye wimbo wake wa "My Heart Will Go On", kutoka kwa wimbo wa filamu ya Titanic, alishinda Oscar ya wimbo bora - alisema alikuwa akiweka kazi yake "kwa muda usiojulikana" huku mumewe René Angélil akipambana na saratani.
Ingawa maonesho yake yalianza tena mwaka mmoja baadaye, aliondoka kwenye jukwaa tena mapema 2016, kufuatia kifo cha Angélil na kaka yake, Daniel Dion. Hatimaye alirudi na albamu ya studio ya 2019 Courage, ambayo ilikuwa na ushirikiano na Sia, Sam Smith na David Guetta.
'Imekuwa mapambano'
Nyota huyo aliunga mkono rekodi hiyo kwa ziara ya ulimwengu, ambayo sehemu kubwa ililazimika kuahirishwa kwa sababu ya janga la Covid.
Alilazimika kupanga tarehe tena mwaka huu baada ya "misuli kukaza na kuwa katika hali inayoendelea"; ambayo pia ilichelewesha kurudi kwenye makazi yake Las Vegas. "timu kubwa ya madaktari wanaofanya kazi pamoja nami ili kunisaidia kupata nafuu" huku "watoto "wakiniunga mkono na kunipa msaada".
Alifafanua: "Ninafanya kazi kwa bidii na mtaalamu wangu wa dawa za michezo kila siku ili kunijengea nguvu na uwezo wangu wa kufanya tena, lakini lazima nikubali kuwa imekuwa ngumu. "Ninachojua ni kuimba. Ni kile ambacho nimefanya maisha yangu yote na ndicho ninachopenda kufanya zaidi.
"Ninawakumbuka sana. Ninakosa kuwaona nyote [na] mkiwa jukwaani, mkitumbuiza. "Huwa natoa asilimia 100 ninapofanya onyesho langu lakini hali yangu hainiruhusu kukupa hiyo sasa hivi." Bila kuzuia machozi tena, mwimbaji huyo alitia sahihi kwa kuwashukuru mashabiki kwa usaidizi wao, akisisitiza kwamba hakuwa na chaguo ila kuzingatia afya yake hivi sasa, na anatumai yuko kwenye "njia ya kupona".
Stiff Person Syndrome ni nini na kuna tiba?
SPS ni hali adimu sana na haieleweki vyema. Kulingana na Taasisi ya Kitaifa ya Matatizo ya Neva, ina sifa ya "kubadilika badilika ikikamata misuli kwenye miguu na mikono na vichocheo kama vile kelele, mguso, na mfadhaiko wa kihemko, ambao unaweza kuanzisha mkazo wa misuli."
"Mkao usio wa kawaida, ambao mara nyingi huinama na kuwa mgumu, ni tabia ya ugonjwa huo," wanabainisha pia. "Watu walio na SPS wanaweza kuwa walemavu sana kuweza kutembea au kuhama, au wanaogopa kuondoka nyumbani kwa sababu ya kelele za mitaani, kama vile honi, zinaweza kusababisha mshtuko na kuanguka.
"Watu wengi walio na SPS huanguka mara kwa mara na kwa sababu hawana uwezo wa kawaida wa kujihami; majeraha yanaweza kuwa makubwa." Ingawa hakuna tiba ya SPS, kuna matibabu ikiwa ni pamoja na dawa za kupunguza wasiwasi na dawa za kutuliza misuli ambazo zinaweza kupunguza kasi ya kuendelea kwake.