Katibu wa Jeshi la Wanamaji la
Marekani John Phelan anaondoka katika utawala wa Trump, imetangaza Pentagon siku
ya Jumatano.
Kuondoka kwake "ni mara moja," msemaji wa Pentagon Sean
Parnell alisema katika chapisho la mitandao ya kijamii.
Parnell aliongeza kuwa, Naibu Katibu Mkuu wa Jeshi la Wanamaji Hung Cao
atahudumu kama kaimu katibu.
Phelan ndiye kiongozi wa hivi karibuni wa ngazi ya juu wa kijeshi
kuondoka katika utawala huo katika miezi ya hivi karibuni.
Kuondoka kwake
kunakuja wakati wa vita kati ya Marekani, Israeli na Iran na kuendelea kwa
vizuizi vya Marekani kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz.
"Kwa niaba ya Waziri wa Vita na Naibu Waziri wa Vita, tunamshukuru
Katibu Phelan kwa utumishi wake katika Jeshi la Wanamaji la Marekani,"
Parnell aliandika. "Tunamtakia kila la kheri katika maisha yake ya
baadaye."
Jeshi la Wanamaji halijatoa sababu ya kuondoka kwa Phelan.
Hii inakuja wiki chache tu baada ya Waziri wa Vita/Ulinzi wa Marekani
Pete Hegseth kumtaka Mkuu wa Majeshi Randy George ajiuzulu kutoka
wadhifa wake.
Maafisa wengine wawili wa Jeshi, Jenerali David Hodne na Meja Jenerali
William Green, pia wameondolewa katika nyadhifa zao hivi karibuni.
Tangu aingie Pentagon, Hegseth amewafukuza kazi dazeni ya maafisa wakuu
wa jeshi, akiwemo mkuu wa operesheni za majini na naibu mkuu wa wafanyakazi wa
Jeshi la Anga.
Jukumu la Katibu wa Jeshi la Wanamaji la Marekani kwa kiasi kikubwa ni
la kiutawala na linajumuisha kuunda sera, kuajiri, kutoa mafunzo na kuwapa
vifaa Jeshi la Wanamaji, pamoja na kusimamia bajeti na vifaa kama vile ujenzi,
na ukarabati wa meli na vifaa vya majini.
Phelan, ambaye hakuwahi kuhudumu jeshini hapo awali, aliapishwa kama
Katibu wa Jeshi la Wanamaji Machi 2025 baada ya kuteuliwa na Rais Donald Trump 2024.
Mfanyabiashara huyo alikuwa mfadhili mkubwa wa kampeni ya Trump.