Iran yakataa mpango wa amani wa Marekani huku ikitoa masharti matano ya kumaliza vita

Maafisa wa Iran wamekuwa wakisema mara kwa mara wanataka kukomeshwa kabisa kwa vita, na sio tu kusitishwa kwa mapigano.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma & Mariam Mjahid

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo yetu ya moja kwa moja.Kuwa na usiku mwema.

  2. AU yamteua Jakaya Kikwete kuwa Mwakilishi wake upembe wa Afrika

    J
    Maelezo ya picha, Ni picha ya aliyekuwa rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete

    Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, ametangaza uteuzi wa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa zamani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa Mwakilishi Mkuu wa Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu.

    Katika jukumu lake Rais Kikwete ataunga mkono juhudi za Umoja wa Afrika kushughulikia mienendo tata ya kisiasa, amani na usalama katika kanda nzima.

    Mamlaka yake yatajumuisha kuendeleza diplomasia, kuwezesha mazungumzo ya kisiasa jumuishi, kukuza kujenga imani miongoni mwa wadau, na kuimarisha mifumo ya ushirikiano wa kikanda inayolenga kustawisha amani na utulivu endelevu.

    Aidha, Kikwete katika wadhifa wake atafanya kazi kwa uratibu wa karibu na washirika husika wa kikanda na kimataifa, ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo (IGAD), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Umoja wa Mataifa ya Kiarabu, Umoja wa Mataifa, na washirika wengine, kwa nia ya kuhakikisha uwiano, ulinganifu na ufanisi katika juhudi za pamoja za kukuza amani, utulivu na usalama.

    Kiongozi huyo anatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika kuzisaidia nchi za eneo hili, pamoja na mifumo husika ya kikanda na kimataifa, katika kutatua changamoto zilizopo na kuendeleza amani, utulivu na ustawi wa kudumu.

    Soma zaidi:

  3. Iran yakataa mpango wa amani wa Marekani huku ikitoa masharti matano ya kumaliza vita

    dhd

    Chanzo cha picha, Reuters

    Shirika la utangazaji la taifa la Iran Press TV linasema, likimnukuu "afisa mkuu wa usalama wa kisiasa", kwamba Iran imekataa pendekezo la Marekani linalolenga kumaliza vita vya sasa.

    Press TV haijamtaja afisa huyo, wala cheo au cheo chake, lakini ripoti afisa huyo anasema: "Iran itamaliza vita itakapoamua kufanya hivyo na wakati masharti yake yenyewe yatatimizwa."

    Maafisa wa Iran wamekuwa wakisema mara kwa mara wanataka kukomeshwa kabisa kwa vita, na sio tu kusitishwa kwa mapigano.

    Kulingana na Press TV, afisa huyo alielezea masharti matano, hayo ni pamoja na:

    • Kusimamishwa kabisa kwa "uchokozi na mauaji" na adui
    • Kuanzishwa kwa mifumo madhubuti ya kuhakikisha kwamba vita havirejei tena kwa Jamhuri ya Kiislamu
    • Malipo yaliyothibitishwa na yaliyofafanuliwa wazi ya uharibifu wa vita na fidia
    • Hitimisho la vita katika nyanja zote na kwa vikundi vyote vya upinzani vinavyohusika katika eneo lote
    • Utambuzi wa kimataifa na dhamana kuhusu haki ya kujitawala ya Iran ya kutumia mamlaka juu ya Mlango-Bahari wa Hormuz.

    Press TV inasema Washington imekuwa ikifuatilia mazungumzo kupitia njia mbalimbali za kidiplomasia, lakini Tehran inaona mapendekezo hayo kuwa "ya kupita kiasi".

  4. Jeshi la Iran ladai kuishambulia meli ya kubeba ndege ya USS Abraham Lincoln kwa makombora

    Kundi la wanamaji linaloongozwa na shehena ya ndege ya USS Abraham Lincoln limeripotiwa kuwa tayari limewasili Mashariki ya Kati.

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Kundi la wanamaji linaloongozwa na shehena ya ndege ya USS Abraham Lincoln limeripotiwa kuwa tayari limewasili Mashariki ya Kati.

    Jeshi la Iran limesema kuwa limeishambulia meli ya USS Abraham Lincoln kwa kombora la kuzuia meli aina ya Qadeer.

    Marekani haijatoa maoni yoyote.

    Jeshi la Irani lilisema katika taarifa kwamba Jeshi la Wanamaji lilirusha "kombora kutoka pwani hadi baharini" kwa kikosi cha meli ya kubeba ndege cha Abraham Lincoln "kwa mara ya kumi na moja," na kulazimisha meli hiyo kubadilisha mkondo.

    Kabla ya shambulio hilo, Shahram Irani, kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Iran, alikuwa amesema kwamba "shughuli na mienendo" ya meli ya kubeba Abraham Lincoln ilikuwa ikifuatiliwa na kwamba "mara tu meli ya kundi hili hasimu inapokuwa ndani ya safu ya mifumo ya makombora, italengwa na Jeshi la Wanamaji la Irani." Marekani haijatoa maoni yoyote

    Wakati huo huo, mashambulizi ya Marekani na Israel katika maeneo ya kijeshi na viwanda ya Iran yanaendelea.

    Huku uvumi kuhusu kutumwa kwa wanajeshi wa nchi kavu wa Marekani ukiendelea, Mohammad Baqer Qalibaf alionya kwamba Iran inafuatilia hatua zote za Marekani za "kupeleka wanajeshi wake katika eneo hilo."

    Maafisa wa Iran wanasisitiza kuwa hawafanyi mazungumzo na Marekani wala kutafuta usitishaji mapigano.

  5. Jinsi baadhi ya Wairani wanavyokabiliana na vita vinavyoendelea nchini mwao

    Watu wanafanya mazoezi kwenye bustani ya Pardisan mjini Tehran wakati wa vita vya Marekani na Israel na Iran

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Watu wanafanya mazoezi kwenye bustani ya Pardisan mjini Tehran wakati wa vita vya Marekani na Israel na Iran

    Hakuna kitu "cha kawaida" kuhusu vita.

    Baadhi ya watu wanalipa pesa nyingi ili kuunganisha kwenye mtandao, kwani serikali imeminya mtandao.

    Kutokana na kile ninachosikia kutoka kwa vijana ndani ya nchi, wanajaribu kurejea kwenye shughuli zao za kawaida kabla ya vita na wanatoka nje zaidi wakati wowote wakijiskia.

    "Ninajisikia nafuu. Nilienda kwenye duka la kahawa kwa mara ya kwanza tangu vita kuanza! Lakini mitaa ilikuwa tupu kuliko kawaida," alisema mwanamke aliye na umri wa miaka 20 huko Tehran.

    "Nilitoka kukimbia asubuhi. Nilikuwa na mwanzo mzuri wa siku yangu," alisema mwanamke mwingine mwenye umri wa miaka 20 ambaye alihama kutoka Tehran hadi jimbo la kaskazini analoliona kama "salama".

    Tehran imeshuhudia mashambulizi makali zaidi tangu vita kuanza.

    Wengine wanajaribu kutembelea jamaa na marafiki wakati wa likizo ya sasa ya Mwaka Mpya wa Kiajemi.

    Mwanamke mwingine katika miaka yake ya 20 ambaye amehama Tehran alisema, "Nilienda kuwaona kwa siku moja au mbili. Naam, ilikuwa wakati mzuri kwa mabadiliko angalau. Lakini ninaikumbuka sana Tehran."

    Soma zaidi:

  6. Iraq kuwasilisha malalamiko kwa Umoja wa Mataifa baada ya kushambuliwa

    Iraq itawasilisha malalamiko rasmi kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya mashambulizi dhidi ya vitengo vyake vya kijeshi, msemaji wa Iraq alisema katika taarifa kutoka ofisi ya waziri mkuu ya vyombo vya habari.

    Waziri Mkuu pia ameiambia wizara ya mambo ya nje kuwaita watendaji wakuu wa Ubalozi wa Marekani kufuatia mashambulizi hayo.

    Wizara ya ulinzi ya Iraq imesema wapiganaji saba waliuawa na 13 kujeruhiwa katika kambi moja magharibi mwa Iraq siku ya Jumatano.

    Shambulio hilo linakuja baada ya shambulio baya zaidi dhidi ya Iraq tangu vita vilipoanza Mashariki ya Kati na kusababisha vifo vya wapiganaji 15 wa Iraq siku ya Jumanne.

    Kundi la Hashed al-Shaabi linalotawaliwa na Washia (Popular Mobilization Forces, PMF) lilisema waliuawa katika shambulio la Marekani.

    Marekani haijatoa maoni yoyote.

    Soma Pia:

  7. Rais wa Uganda aelezea chakula kilichomsaidia kupunguza uzito wa mwili wa kilo 30

    g

    Chanzo cha picha, social

    Lishe ya mihogo, viazi vitamu na mboga za asili imemsaidia Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, kupunguza kilo 30, ameiambia BBC.

    “Afya yangu imekuwa nzuri kila wakati, lakini madaktari walifanya makosa na kisha nikaamua kupunguza uzito,” alisema Bw. Museveni.

    Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 75 awali hakuwa na ufahamu wa uzito wake, ambao ulikuwa ni kilo 106.

    Alikanusha maoni kwenye mitandao ya kijamii kwamba “anaonekana mchovu,” akisema amepunguza uzito kidogo tu.

    Alisema kwenye blogu yake ya kibinafsi mwezi uliopita: “Nimekwepa kuwa na mwili mnene, kwa sababu madaktari hawakunielezea kuwa hii inasababisha matatizo au kwamba ni lazima kukabiliana na unene kupita kiasi.”

    Aliongeza kuwa uzito wake wa sasa ni kilo 76, unaolingana na urefu wake wa futi 5 na inchi 7 (170cm).

    Hata hivyo, Bw. Museveni hakueleza ni muda gani uliochukua kupunguza kilo 30.

    “Ninakula mihogo kwa sababu sili chakula chenu cha Ulaya au Asia. Ninakula chakula chetu kama; mihogo, ndizi, viazi na mboga zetu za asili,” alisema Bw. Museveni kwa BBC.

    Soma Pia:

  8. Miili 32 imefukuliwa katika kaburi la pamoja Kericho nchini Kenya

    Baadhi ya miili inaonekana kutoka hospitali katika kaunti jirani
    Maelezo ya picha, Baadhi ya miili inaonekana kutoka hospitali katika kaunti jirani

    Takriban miili 32, mingi yao ikiwa ya watoto wachanga, imefukuliwa kutoka kaburi la pamoja katika mji wa magharibi mwa Kenya, Kericho, huku uchunguzi ukiendelea kuhusu ugunduzi huu wa kushangaza.

    Ufukuaji huo ulifanyika baada ya polisi kupata amri ya mahakama ya kufukua miili 14, ambayo awali iliaminika kuzikwa katika eneo hilo.

    Mchunguzi wa maiti wa serikali, Richard Njoroge, aliwaambia waandishi wa habari Jumanne jioni kwamba kile walichokigundua kilikuwa “cha ajabu”, huku miili ikiwa “imerundikwa kwenye mifuko ya gunia”, baada ya mchakato wa mchana mzima uliyotatizwa na mvua kubwa.

    Uchunguzi wa kina wa maiti ulitarajiwa kuanza leo Jumatano wiki hii, huku kukiwa na wito wa kutambua mara moja miili hiyo ya kuchunguza mazingira ya vifo hivyo.

    Njoroge ambaye ni mkaguzi wa maiti wa serikali alisema kulikuwa na watu wazima saba na watoto 25, huku watoto wakiwa wachanga na vijusi. Sehemu kadhaa za miili pia zilipatikana.

    Aliongeza kuwa baadhi ya miili ilionekana kutoka hospitali na mochari, jambo litakalothibitishwa zaidi baada ya uchunguzi wa kina. Pia alitaja kuwa miili ya watu wakubwa ilikuwa imeharibika sana, huku ile ya watoto ikiwa haijaharibika kwa kiwango hicho, ikionyesha vifo vilitokea katika nyakati tofauti.

    Jumanne, waendesha mashtaka wa mauaji na timu za uchunguzi, wakiwa wamevaa mavazi ya kinga meupe, glovu na barakoa, walifanya kazi chini ya ulinzi mkali huku wakichimba kwenye eneo hilo. Baadhi ya miili ilipatikana kamili, huku mingine ikipatikana sehemu tu na mifupa, ikihifadhiwa katika mifuko ya ushahidi.

    Polisi walifunga eneo hilo huku umati wa wakazi ukikusanyika karibu. Wengine walionekana wakiwa wameshikwa na hofu wakati wakaguzi waliporekodi kila hatua ya uchimbaji. Uchimbaji huu ulifanyika kufuatia taarifa kutoka kwa mlalamishi, iliyosababisha polisi kuanzisha uchunguzi.

    Siku ya Jumatatu, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ilisema matokeo yao ya awali yanaonyesha kuwa miili 13 isiyodaiwa ilitolewa rasmi kutoka hospitali iliyoko kaunti jirani ya Nyamira na kuhamishwa Kericho kwa mazishi Ijumaa iliyopita.

    Hata hivyo, maswali mengi bado yapo kuhusu miili ya ziada na jinsi ilivyozikwa.

    Soma pia:

  9. Ghana yadai fidia kwa utumwa katika upigaji kura wa kihistoria wa UN

    Takriban Waafrika milioni 12-15 walitekwa wakati wa biashara ya utumwa

    Chanzo cha picha, Universal Images Group via Getty Images

    Maelezo ya picha, Takriban Waafrika milioni 12-15 walitekwa wakati wa biashara ya utumwa

    Utumwa ulikuwa “dhambi mbaya zaidi iliyotokea katika historia ya binadamu,” amesema waziri wa mambo ya nje wa Ghana, akizungumza na BBC kabla ya upigaji kura wa kihistoria katika Jumuiya ya Umoja wa Mataifa (UN).

    Nchi wanachama zitaripoti kupiga kura juu ya azimio lililoongozwa na Ghana la kutambua biashara ya watumwa iliyofanyika nchi za pande zote mbili za Atlantiki, kwa kawaida Uingereza na Marekani kama “dhambi kubwa zaidi dhidi ya ubinadamu.”

    Mapendekezo hayo yanahimiza nchi wanachama wa UN kuzingatia kuomba msamaha kwa biashara ya watumwa na kuchangia katika mfuko wa fidia.

    Azimio hilo linaweza kukabiliana na upinzani, kwani nchi kama Uingereza kwa muda mrefu zimekataa kulipa fidia, zikisema taasisi za leo haziwezi kuwajibika kwa makosa ya zamani.

    Hata hivyo, wafuasi wa mapendekezo haya, wakiwemo Umoja wa Afrika, wanasema ni hatua kuelekea uponyaji na haki.

    Samuel Okudzeto Ablakwa, waziri wa mambo ya nje wa Ghana, alisema katika kipindi cha BBC’s Newsday: “Tunaidai fidia na tuwe wa wazi, viongozi wa Kiafrika hawaombi pesa kwa ajili yao wenyewe.

    “Tunataka haki kwa waathirika na kusaidia sababu zao, kama vile fedha za elimu, misaada ya kudumu, na mfuko wa mafunzo ya ujuzi.”

    Ablakwa pia alisema kuwa, kwa azimio hili, Ghana hailinganishi maumivu yake juu ya wa wengine, bali inarekodi tu ukweli wa kihistoria.

    Soma zaidi:

  10. Iran “inafuatilia kwa makini” harakati za wanajeshi wa Marekani - Spika wa Iran

    f

    Chanzo cha picha, Reuters

    Spika wa bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, amesema Iran “inafuatilia kwa makini harakati zote za Marekani katika eneo, hasa kuhamishwa kwa wanajeshi.”

    “Msijaribu uthabiti wetu wa kulinda ardhi yetu,” ameongeza katika chapisho kwenye mitandao ya kijamii.

    Pentagon inatarajiwa kutuma maelfu ya wanajeshi kutoka kikosi maalumu cha Jeshi la Marekani, 82nd Airborne Division, kwenda Mashariki ya Kati, kwa mujibu wa Reuters. Hatua hiyo itaoongeza nguvu za kijeshi za Marekani huku Rais Donald Trump akizungumza kuhusu uwezekano wa makubaliano na Tehran kuhusu kumaliza vita.

    Ripoti zisizothibitishwa zilisema kuwa utawala wa Trump ulikuwa ukizingatia Ghalibaf kama mshirika wa kisiasa, na labda hata kiongozi wa baadaye.

    Soma zaidi:

  11. Idadi ya wahamiaji waliokufa wakijaribu kufika rasi ya Uarabuni yaongezeka maradufu - IOM

    Wahamiaji hao walikuwa wameabiri boti

    Chanzo cha picha, EPA

    Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu uhamiaji IOM limesema idadi ya watu waliofariki dunia wakijaribu kufika Rasi ya Uarabuni wakitokea pembe ya Afrika iliongezeka maradufu hadi watu 922.

    Watu hao waliofariki dunia walikuwa miongoni mwa zaidi ya wahamiaji laki tano waliojaribu kuvuka Bahari ya Shamu, wakiwa na ndoto za kufika mataifa ya Kiarabu ya ghuba kwa lengo la kutafuta ajira katika nchi hizo tajiri.

    IOM imesema ongezeko hilo linaashiria mbinu mpya za wanaosafirisha watu kimagendo ambazo zinakwepa vituo vya ukaguzi vilivyopo Ethiopia, Djibouti na Somalia.

    Maelfu ya wahamaiaji waliojaribu kutumia njia hizo waliishia kukwama nchini Yemen ambako shirika hilo la kimataifa la uhamiaji linasema hali ya kibinadamu imezorota huku watu wakiwekwa vizuizini na wanawake kunyanyaswa na magenge ya wanaofanya biashara haramu ya kuwasafirisha wahamiaji.

    Yemen ni taifa masikini zaidi katika Rasi hiyo ya uarabuni na imekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa takriban muongo mmoja.

    Baadhi ya wahamiaji wanaojikuta nchini humo,huwa radhi kurejea makwao badala ya kusalia Yemen.

    Mkuu wa IOM Djibouti Tanja Pacifico amesema ikilinganishwa na mwaka 2024, mwaka jana 2025 ulikuwa mbaya zaidi kuwahi kurekodi idadi kubwa ya watu waliokufa au kupotea wakiwa njiani kuelekea nchi za Kiarabu na kwingineko.

    Wengi wa waathiriwa ni kutoka Ethiopia,taifa la pili Afrika lenye idadi kubwa zaidi ya watu likiwa na zaidi ya watu milioni 130.

    Ethiopia inakumbwa na mizozo mingi ya wenyewe kwa wenyewe na umasikini uliothiri,mambo yanayowafanya wengi wa raia wake kutaka kuihama nchi.

    Soma Pia:

  12. Maafisa wa Pakistan wasema Iran imepokea mpango wa Marekani wenye pointi 15

    Ufikiaji wa usafirishaji kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz umeripotiwa kujumuishwa katika mpango wa Marekani wenye pointi 15

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Ufikiaji wa usafirishaji kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz umeripotiwa kujumuishwa katika mpango wa Marekani wenye pointi 15

    Shirika la habari la Associated Press limeripoti kuwa Iran imepokea mpango wa pointi 15 kutoka kwa Marekani kwa ajili ya kufikia usitishaji vita wa Marekani na Israel dhidi ya Iran, likiwanukuu maafisa wawili wa Pakistan.

    Maafisa wa Pakistani waliripotiwa kusema pendekezo hilo linashughulikia kwa upana yafuatayo:

    • Msaada wa vikwazo
    • Ushirikiano wa nyuklia wa kiraia
    • Kurejeshwa kwa mpango wa nyuklia wa Iran
    • Ufuatiliaji na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki
    • Vikomo vya kombora, na ufikiaji wa usafirishaji kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz

    Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif alisema hapo awali kwamba nchi hiyo iko "tayari" kuandaa mazungumzo ili kusuluhisha mzozo huo.

    Televisheni ya Channel 12 ya Israel pia imeripoti juu ya mpango huo.

    Hakujakuwa na uthibitisho wa maelezo kutoka kwa Ikulu ya White House.

    Jeshi la Iran limekanusha kufanya mazungumzo na Marekani.

    Soma Pia:

  13. Tamasha la Shakira huko Doha laahirishwa kufuatia mzozo mashariki ya kati

    d

    Chanzo cha picha, Reuters

    Tamasha la mwanamuziki Shakira, ambalo lilikuwa limepangwa kufanyika Doha tarehe 1 Aprili, limeahirishwa kutokana na “hali ya sasa katika eneo hilo,” kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na tovuti ya utalii.

    Haya yanajiri wakati ambapo mashambulizi ya makombora kati ya Iran na Israel yakiendelea ingawa rais wa Marekani Donald Trump amedai kuwa mazungumzo yakuleta muafaka yanaendelea baina yake na watu sahihi Iran.

    Soma Pia:

  14. Urusi yaanzisha shambulio kubwa zaidi kuwahi kutokea dhidi ya Ukraine

    g

    Chanzo cha picha, Andriy Sadovyi/Telegram

    Urusi imetekeleza mashambulizi makubwa zaidi ya anga katika kipindi cha saa 24 zilizopita tangu kuanza kwa vita vinavyoendelea dhidi ya Ukraine, kwa kulenga miji kadhaa ya Ukraine kwa kutumia droni 948.

    Kwa mujibu wa Jeshi la Anga la Ukraine, droni 556 zilirushwa kuanzia saa 3:00 asubuhi kwa saa za huko Jumanne, katika shambulio la mchana lisilo la kawaida sana ambalo liliua angalau watu watatu na kujeruhi makumi ya wengine.

    Kwa mujibu wa mamlaka za mitaa, monasteri ya Bernardine ya karne ya 16 katika mji wa magharibi wa Lviv, ambayo ni sehemu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni, UNESCO Iliopo katikati ya jiji, iliharibiwa.

    Kwa mujibu wa uongozi wa Ukraine, droni 392 pamoja na makombora 34 vilirushwa usiku baada ya saa nane.

    Hata hivyo, hadi sasa hakujakuwa na majibu kutoka kwa jeshi au utawala wa Urusi kuhusu madai hayo ya Waukraine.

    Soma pia;

  15. Iran yasema Marekani inajadiliana peke yake

    .

    Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock

    Msemaji wa Makao Makuu ya Khatam al-Anbiya ya Iran, ambaye ni kamanda mkuu wa kijeshi wa nchi hiyo (bila kutaja jina la Marekani na Trump) amezungumzia kuhusu "taifa lenye nguvu kubwa duniani" - akisema "usiite kushindwa kwako makubaliano".

    Ebrahim Zolfaghari amesema katika ujumbe wa video uliochapishwa na vyombo vya habari vya Iran leo kwamba "je, kiwango cha mgogoro wenu wa ndani kimefikia hatua ambapo mnajadiliana wenyewe?"

    "Hautaona uwekezaji wako katika eneo hilo wala bei za zamani za mafuta tena, hadi utakapoelewa kwamba utulivu katika eneo unahakikishwa na mkono wenye nguvu wa vikosi vyetu vya kijeshi. Utulivu huja kupitia nguvu," Zolfaghari alisema.

    Aliongeza kwamba "mtu kama sisi hatuwezi kufikia makubaliano na mtu kama wewe. Sio sasa, wala milele".

    Soma zaidi:

  16. Waziri Lukuvi wa Tanzania afariki dunia

    Lukuvi

    Chanzo cha picha, Wizara ya ardhi

    Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,Uratibu na Wenye Ulemavu, na Mbunge wa jimbo la Isimani, William Lukuvi ameaga dunia.

    Kifo chake kimetokea leo tarehe 25 mwezi Machi mwaka 2026, saa moja asubuhi, katika hospitali ya Benjamini Mkapa jijini Dodoma, taarifa ya Ikulu ya Tanzania imeeleza.

    Lukuvi alikuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa mshtuko wa moyo hospitalini hapo.

    Lukuvi amekulia umoja wa Vijana CCM. Alianza kuwa Naibu Waziri baadaye Mkuu wa mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam wakati wa Rais Mkapa.

    Rais Kikwete alimteua kuwa Waziri katika wizara tofauti. ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge Sera na Uratibu.

    Katika awamu ya utawala wa John Pombe Magufuli, alimteua kuwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi.

    Rais Samia alimtoa kwenye baraza la mawaziri na kumfanya kuwa mshauri wa masuala ya uhusiano wa umma, kisha kumrejesha kuwa waziri baada ya uchaguzi wa 2025.

  17. Bei ya mafuta yashuka huku Trump akizungumzia mazungumzo ya amani ya Iran

    .

    Chanzo cha picha, CFOTO/Future Publishing via Getty Images

    Bei ya mafuta imeshuka barani Asia baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema mazungumzo ya kukomesha vita yanaendelea, huku Iran ikisema meli "zisizo na uadui" zinaweza kutumia njia muhimu ya meli katika Mlango Bahari wa Hormuz.

    Mafuta ghafi yalishuka kwa 5% hadi $99.29 (£74.16) kwa pipa, huku mafuta yaliyouzwa Marekani yakishuka kwa zaidi ya 5.5% hadi $88.41.

    Trump alisema Jumanne kwamba mazungumzo ya kukomesha vita yanafanyika kwa "sasa" na kwamba watu ambao Marekani ilikuwa ikijadiliana nao "wanataka kufanya makubaliano haraka iwezekanavyo" - dai linalopingwa na maafisa wa Iran.

    Siku ya Jumatatu, maafisa mjini Tehran walisema madai ya mazungumzo kati ya Marekani na Iran yalikuwa "habari bandia", huku mashambulizi kati ya Israel na Iran yakiendelea.

    Trump alisema Makamu wa Rais JD Vance na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio walihusika katika majadiliano ya kukomesha vita.

    Rais aliongeza kwamba mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yamesababisha "mabadiliko ya utawala", akirudia madai yake kwamba viongozi wa Iran wamekubaliana kwamba hawatakuwa na silaha ya nyuklia tena.

    Lakini Iran hapo awali ilikanusha madai kwamba ilikuwa imewasiliana na Marekani, ikisema hilo ni jaribio la kudanganya masoko.

    Soma zaidi:

  18. Iran yasema meli 'zisizo na uadui' zinaweza kupita salama Mlango-Bahari wa Hormuz

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Picha ya meli ya Thai ya Mayuree iliyoshambuliwa tarehe 11 mwezi Machi.

    Iran imesema kwamba meli "zisizo na uadui" zinaweza kupita kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz huku kukiwa na mlolongo wa usafiri baharini kupitia njia hiyo ya maji ambayo imesababisha mgogoro mkubwa zaidi wa nishati duniani.

    Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, ujumbe wa Iran kwa Umoja wa Mataifa ulisema meli zinaweza kupita "salama" kwenye njia ya baharini, "mradi tu hazitashiriki wala kuunga mkono vitendo vya uchokozi dhidi ya Iran na kufuata kikamilifu kanuni za usalama zilizotangazwa."

    Ujumbe kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ulitumwa kwa Baraza la Usalama lenye wanachama 15 na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres siku ya Jumapili. Kisha ukasambazwa Jumanne miongoni mwa wanachama 176 wa shirika la meli la Umoja wa Mataifa lenye makao yake makuu London linalohusika na kudhibiti usalama wa meli za kimataifa na kuzuia uchafuzi wa mazingira.

    Meli zitaruhusiwa kusafiri kwenye Mlango Bahari "kwa uratibu na mamlaka husika za Iran", taarifa hiyo iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii ilisema.

    Hata hivyo, Iran haikufafanua katika taarifa kuhusu kanuni ambazo vyombo vya majini vinapaswa kufuata ili kusafiri kwa usalama kwenye njia ya Mlango Bahari, ambayo karibu moja ya tano ya usambazaji wa mafuta na gesi asilia duniani hupitia.

    Matamshi ya Iran yalikuja huku Rais wa Marekani Donald Trump akisema mazungumzo yanaendelea ili kukomesha vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, licha ya Iran kukanusha hapo awali kwamba pande hizo zilikuwa katika mazungumzo.

    Soma zaidi:

  19. Qatar inasema "haishiriki" katika juhudi zozote za upatanishi kati ya Marekani na Iran

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Qatar imetangaza kwamba "haishiriki" katika juhudi zozote za upatanishi wa moja kwa moja kati ya Marekani na Iran, ikibainisha kwamba inaunga mkono "njia za kidiplomasia" zinazolenga kukomesha vita, kulingana na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar Majid Al-Ansari.

    "Kwa sasa hakuna juhudi za moja kwa moja za Qatar zinazohusiana na upatanishi kati ya pande hizo mbili," Al-Ansari alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari wa kila wiki katika Wizara ya Mambo ya Nje, akielezea kwamba "lengo la Qatar katika hatua ya sasa ni kuilinda nchi na kushughulikia hasara zinazotokana na mashambulizi mbalimbali ambayo imekabiliwa nayo

    Alibainisha kwamba msimamo wa Qatar tangu siku ya kwanza ya vita "umekuwa wazi, kwamba vita hivi lazima vimalizike kwa njia za kidiplomasia, na huu ndio msimamo wetu kuhusu migogoro yote duniani

    Katika muktadha huu, Al-Ansari alisema kwamba mawasiliano na Iran "kwa kawaida hutegemea misimamo na vitendo vyake, haswa kuhusu mashambulizi ambayo nchi za eneo hilo zimefanyiwa," akiongeza, "Iran lazima iamue jinsi inavyoweza kujenga upya uaminifu uliopotea kwa sababu ya mashambulizi yake dhidi ya uhuru wetu".

    Kuhusu "uratibu" kati ya Qatar na Marekani, alisema: "Sisi ni washirika wa upande wa Marekani, na tunafanya kazi kuwasiliana nao ili kuweka wazi taswira kamili, hasa kwa kuwa shambulio dhidi ya Jimbo la Qatar limesababisha matokeo mabaya kwa uchumi wa Qatar".

    Katika suala hili, Al-Ansari alisema kwamba "shambulio la vituo vya gesi huko Ras Laffan lilisababisha kupungua kwa uzalishaji kwa asilimia 17, huku hasara zikifikia takriban dola bilioni 100 kwa kipindi cha miaka mitano, na shughuli za ukarabati zinaweza kuchukua muda sawa".

    Soma zaidi:

  20. Marekani kupeleka maelfu ya wanajeshi zaidi Mashariki ya Kati

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Pentagon inatarajiwa kutuma maelfu ya wanajeshi kutoka kikosi maalumu cha Jeshi la Marekani, 82nd Airborne Division, kwenda Mashariki ya Kati, kwa mujibu wa Reuters. Hatua hiyo itaoongeza nguvu za kijeshi za Marekani huku Rais Donald Trump akizungumza kuhusu uwezekano wa makubaliano na Tehran kuhusu kumaliza vita.

    Reuters iliripoti kwa mara ya kwanza tarehe 18 Machi kuwa utawala wa Trump ulikuwa unafikira kutuma majeshi zaidi, hatua ambayo ingeweza kupanua uwezekano wa kuhusisha operesheni ndani ya ardhi ya Iran.

    Hatua kama hiyo ingeongeza hatari katika mzozo ambao tayari umeshaingia wiki ya nne na kuathiri masoko ya kimataifa. Maafisa hao, waliokuwa wakizungumza kwa sharti la kutotambulika, hawakutoa maelezo ya mahali ambapo wanajeshi hao watapelekwa au lini watapofika katika eneo hilo.

    Kuhusu hili, msemaji wa White House, Anna Kelly alisema “Kama tulivyoeleza, Rais Trump daima ana chaguo zote za kijeshi kwenye mikononi yake,”.

    Hadi sasa, hakuna uamuzi uliofanywa kutuma majeshi ndani ya Iran yenyewe, alisema chanzo kimoja, lakini hatua hii itaongeza uwezo wa Marekani kwa ajili ya operesheni zinazoweza kufanyika baadaye katika eneo hilo.