Tsunami Tonga: Watu wanasubiri habari zaidi kwa hamu baada ya Tonga kutengwa na Tsunami
Raia wa Tonga wanaoishi ng'ambo wanasubiri kwa hamu habari za wapendwa wao baada ya volkano kusababisha tsunami katika visiwa hivyo.
Volkano ya chini ya bahari ililipuka siku ya Jumamosi, yapata kilomita 65 kaskazini mwa mji mkuu Nuku'alofa.
Mlipuko huo ambao ulisikika maeneo ya mbali hata hadi Marekani, ulisababisha mawimbi ya urefu wa zaidi ya mita moja yaliyogonga kisiwa cha Tonga.
Mamlaka za eneo hilo hazijathibitisha vifo vyovyote lakini mawasiliano yamekatwaa, na hivyo kufanya iwe vigumu kubaini ukubwa wa uharibifu huo.
Hatahivyo, kaka wa mwanamke raia wa Uingereza alisema alifariki baada ya kusombwa na mawimbi.
Alisema Angela Glover mwenye umri wa miaka 50, alisombwa na maji alipokuwa akijaribu kuwaokoa mbwa wake.
Umbali wa zaidi ya kilomita 10,000, watu wawili walizama kwenye ufuo wa bahari kaskazini mwa Peru kutokana na mawimbi makubwa yasio ya kawaida.
New Zealand na Australia zilituma ndege za uchunguzi kujua zaidi, huku New Zealand ikisema kumekuwa na "uharibifu mkubwa" kwenye pwani ya magharibi ya Tongatapu, kisiwa kikuu cha Tonga.
Lakini Shirika la Msalaba Mwekundu lilitoa sababu fulani za matumaini, likisema ripoti zilisema uharibifu haukuwa mbaya kama ilivyohofiwa.
Tonga haifikiki baada ya waya muhimu wa chini ya bahari unaounganisha visiwa vya Pasifiki na ulimwengu wa nje kukatwa. Inaweza kuchukua hadi wiki mbili kurejesha laini za simu na intaneti.
Lakini ishara za mawasiliono zimegunduliwa kutoka kwa visiwa viwili vidogo vilivyotengwa vya Tonga kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Siniva Filise, raia wa Tonga huko Wales, aliambia BBC kuwa hakuweza kuwasiliana na wazazi wake wazee.
"Nina wasiwasi sasa iwapo wana chakula? Au maji safi ya kunywa?"
Hoteli ya Ha'atafu Beach Resort huko Tongatapu "iilisombwa kabisa" na "ukanda wa pwani wa magharibi kuharibiwa kabisa", kulingana na chapisho kwenye ukurasa wa Facebook wa kituo hicho kilichoandikwa na watu wanaowasiliana nao ng'ambo.
Chapisho hilo lilisema wale wanaoishi huko "walifanikiwa tu kufika mahali salama wakikimbia vichakani na kutoroka", na "hawakuweza kuokoa chochote".
Shirika la Msalaba Mwekundu limesema hata simu za satelaiti, zinazotumiwa na mashirika mengi ya misaada, zina mawasiliano duni kutokana na athari za wingu la majivu. Shirika hilo linakadiria kuwa hadi watu 80,000 wanaweza kuwa wameathiriwa na tsunami hiyo.
Alexander Matheou, mkurugenzi wa kanda wa shirika la Msalaba Mwekundu, anasema kuna uwezekano vumbi la volkeno na tsunami vimechafua maji ya Tonga.
"Moja ya mahitaji makubwa ni kutoa huduma za kusafisha maji na maji safi ya kunywa," Bw Matheou alisema.
Your device may not support this visualisation
Maafisa wengine wameelezea wasiwasi wao juu ya juhudi za misaada na kusababisha kuenea kwa Covid nchini, ambayo ilirekodi kisa chake cha kwanza mnamo Oktoba.
Tonga ina visiwa 170 vilivyotawanyika zaidi ya kilomita 700,000 mraba. Takriban watu 100,000 wanaishi Tonga, wengi wao wakiwa kwenye Kisiwa cha Tongatapu.

Chanzo cha picha, EPA










