Moja kwa moja, Vita vya Iran: Trump asema malengo ya Marekani 'yanakaribia kukamilika'

Akilihutubia taifa juu ya vita hivyo amesema Marekani itamaliza kazi hiyo na kutishia kushambulia miundombinu ya nishati ya Iran ikiwa viongozi wapya wa nchi hiyo hawatafikia makubaliano.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi

  1. Sekta ya majani chai nchini Kenya yaathirika na vita vya Iran

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Usafiri wa bahari Mashariki ya Kati umeathirika kutokana na vita vinavyoendelea Iran, na hii imesababisha zaidi ya kilo millioni 8 za majani chai kusalia katika maghala ya bandari ya Mombasa nchini Kenya, kwa wiki kadhaa, na kuathiri mapato ya wakulima wanaotegemea mauzo ya chai nje ya nchi.

    Mkuu wa chama cha wafanyabiashara wa majani chai Afrika Mashariki lenye kusimamia mnada wa majani chai mjini Mombasa, aliiambia shirika la habari la Reuters kuwa kuanzia tarehe 1 mwezi Machi, wamarekodi hasara ya dolla millioni 8 kila wiki.

    Mkurugenzi huyo amesema hakuna majani chai yanayosafirishwa kwa sasa kuelekea Mashariki ya Kati ambayo hununua takriban 25% ya mazao ya chai ya Kenya.

    Vita vinavyoendelea Iran vimeathiri usafiri wa baharini, huku meli nyingi zikisitisha usafirishaji wa bidhaa kupitia Mlango Bahari wa Hormuz na Bab el-Mandeb.

    Kenya huuza zaidi ya kilo millioni 100 ya majani chai Mashariki ya Kati kila mwaka, huku sasa meli zinazopeleka chai katika taifa la Pakistan zikilazimika kutumia njia ndefu ya bahari ambayo ni ghali mno.

    Vita vya Ukraine na Urusi pia viliathiri biashara ya majani chai nchini Kenya. Kabla ya vita hivyo, Urusi ilikuwa inaagiza kilo millioni 29 za majani chai kutoka Kenya, ila sasa idadi hiyo imepunguka hadi kilo millioni 5.

    Pia unaweza kusoma:

  2. Kiongozi wa kijeshi Libya anunua ndege zisizo na rubani licha ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kiongozi wa kijeshi wa Mashariki mwa Libya, Khalifa Haftar, amenunua kile kinachoonekana kuwa ndege zisizo na rubani za kivita za China na Uturuki, ripoti ya Reuters imebaini, licha ya vikwazo vya muda mrefu vya Umoja wa Mataifa vya kuuzia silaha nchi hiyo iliyogawanyika ya Afrika Kaskazini.

    Picha za setilaiti za kibiashara zinaonyesha takriban ndege tatu zisizo na rubani katika kambi ya anga ya Al Khadim, iliyoko jangwani yapata kilomita 100 (maili 62) mashariki mwa jiji la Benghazi, kati ya mwishoni mwa Aprili na Desemba. Kuwasili kwao hakujawahi kuripotiwa hapo awali.

    Kile kilichoonekana kama vifaa vya kudhibiti vya ardhini kwa ndege hiyo bado kilionekana mwaka huu, kulingana na wataalamu watatu wa silaha waliopitia picha hizo.

    Magari ya angani yasiyo na rubani (UAV) yalichukua jukumu muhimu wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya 2014-2020 nchini Libya, wakati Jeshi la Kitaifa la Libya (LNA) la Haftar lilipojaribu kuipindua serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa huko Tripoli kwa madai kwamba ilikuwa na magenge yenye silaha na "magaidi", jambo ambalo lilikana.

    Nchi ikiwa ni pamoja na Falme za Kiarabu (UAE), Misri na Urusi zilitoa uungwaji mkono muhimu kwa Haftar, kulingana na wachunguzi wa Umoja wa Mataifa, huku Uturuki ikiunga mkono utawala wa Tripoli. China iliepuka kuegemea upande wowote.

    Makundi yanayopigana ya Libya yalikubaliana kusitisha mapigano mwaka wa 2020, lakini nchi hiyo bado imegawanyika kati ya utawala wa Haftar upande wa mashariki na serikali yenye makao yake makuu Tripoli inayoongozwa na Waziri Mkuu Abdulhamid Dbeibah upande wa magharibi.

    Soma zaidi:

  3. Mashambulizi ya Marekani na Israel 'hayana maana' - Msemaji wa Jeshi la Iran

    .

    Chanzo cha picha, IRGC

    Msemaji wa jeshi la Iran anasema Marekani na Israel zimekuwa zikilenga shabaha "zisizo muhimu" huku akitishia kufanya mashambulizi "makubwa ya uharibifu" dhidi ya mahasimu wao.

    Katika taarifa iliyotolewa kwa shirika la habari la Tasnim na mshirika wa jeshi la Ulinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na shirika la habari la Fars, anasema nchi hizo mbili zina taarifa "isiyo kamili" kuhusu uwezo wa zana za kijeshi za Tehran.

    Msemaji huyo anaongeza kuwa utengenezaji wa silaha za kijeshi za Iran "unafanyika katika sehemu ambazo huwajui kabisa" - huku akipinga madai ya Trump kwamba hifadhi ya silaha za Iran imepungua sana.

    Anasema Marekani na Israel "lazima watalipia uchokozi walioanzisha".

    Huku hayo yakijiri msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Saudi Arabia anasema nchi hiyo imenasa wimbi jipya la ndege zisizo na rubani.

    Anasema ndege nne zisizo na rubani zilinaswa na kuharibiwa.

    Hapo awali, wizara hiyo iilitangaza kudondosha kombora la balestiki lililokuwa likielekea eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

    Soma zaidi:

  4. Milipuko katika ghala la risasi yawaua watu 13 Burundi - jeshi

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Takribani watu 13 wamefariki dunia na makumi ya wengine kujeruhiwa katika misururu ya milipuko mikubwa iliyotokea katika ghala la silaha mjini Bujumbura, Burundi, jeshi linasema.

    Katika taarifa yake hapo awali ili kwamba watu 57, pamoja na wanajeshi watatu, walijeruhiwa.

    Nyumba na magari ya kibinafsi yaliharibiwa, huku vifaa vya kijeshi viliharibiwa katika milipuko hiyo, iliongeza.

    Milipuko hiyo ilitokea Jumanne jioni katika kituo hicho, kilicho katika kitongoji cha Musaga, kufuatia hitilafu ya umeme, msemaji wa jeshi alisema hapo awali.

    Vipande vya silaha vilivyolipuka vilirushwa zaidi ya kilo mita tano sawa na (maili tatu).

    Hapo awali, jamaa za watu walioshuhudia tukio hilo waliiambia BBC kuwa walishuhudia vifo vinne tofauti mjini humo.

    Vyanzo vya usalama vililiambia shirika la habari la AFP kwamba makumi ya watu walifariki.

    Mwanamke mmoja aliiambia BBC Idhaa ya Maziwa Makuu kwamba jamaa, ambaye alikuwa amezuiliwa katika Gereza Kuu la Mpimba, alifariki baada ya bomu kupiga kituo hicho.

    Wafungwa kadhaa waliokuwa katika gereza hilo lililo karibu na ghala la risasi, wameripotiwa kujeruhiwa.

  5. Vita vya Iran: Hotuba ya Trump yatikisa masoko huku bei ya mafuta ikipanda

    Trump

    Chanzo cha picha, EPA

    Bei ya mafuta ilipanda bei na hisa kushuka soko lilipofungulia asubuhi ya Alhamisi barani Asia, kufuatia hotuba ya Rais wa Marekani Donald Trump, ambayo haikuhakikishia masoko ya kimataifa kwamba vita vilikuwa karibu kumalizika na kwamba usafiri wa meli kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz ungerejelea hali ya kawaida.

    Mara baada ya Trump kumaliza kuzungumza, bei ya mafuta ghafi ya Brent, ambayo inatathmini kiwango cha kimataifa cha mafuta, ilipanda kwa asilimia tano hadi dola 106 kwa pipa huku masoko ya hisa barani Asia pia yalianza kudorora.

    Ijapokuwa Trump alisisitiza ratiba yake ya wiki mbili hadi tatu, hakutoa hakikisho kamili kwa wawekezaji kuhusu jinsi vita hivi vitakavyoisha.

    Kauli yake ya kuipiga Iran kwa mabomu na kuirejesha "kurudi Enzi za Kale" ikiwa haitafikia makubaliano imeyumbisha hali ya biashara duniani.

    Hata kama mzozo huo utamalizika mwezi huu, bado itachukua muda mrefu kwa viwango vya kawaida vya usafirishaji kuanza tena kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz.

    Maelezo zaidi:

  6. Tetemeko la ardhi la ukubwa wa 7.4 lakumba Indonesia

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Tetemeko la ardhi la kiwango cha 7.4 limetokea katika Bahari ya Molucca karibu na kisiwa cha Ternate nchini Indonesia mapema Alhamisi na kusababisha kifo cha mtu mmoja.

    Tetemeko hilo, ambalo lilitokea saa 06:48 kwa saa za ndani (22:48 GMT) katika kina cha kilomita 35, lilisababisha kutolewa kwa tahadhari ya tsunami ambayo sasa imeondolewa.

    Mwanamke mwenye umri wa miaka 70 huko Sulawesi Kaskazini alifariki baada ya kuangukiwa na vifusi vya jengo, na mtu mwingine kuvunjika mguu baada ya kuruka kutoka kwenye jengo, shirika la habari la taifa la Indonesia Antara liliripoti.

    Ingawa eneo hilo hukumbwa na viwango vya juu vya mitetemeko ya ardhi, baadhi ya wakaazi wengine waliambia BBC kuwa hili lilikuwa mojawapo ya matetemeko ya ardhi yenye nguvu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka sita iliyopita.

    Pia unaweza kusoma:

  7. UAE inazuia makombora yaliyorushwa na Iran

    Tangu kuanza kwa vita, Iran imekuwa ikifanya mashambulizi dhidi ya miundombinu ya kiraia katika nchi za Ghuba, ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai.

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Tangu kuanza kwa vita, Iran imekuwa ikifanya mashambulizi dhidi ya miundombinu ya kiraia katika nchi za Ghuba, ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai.

    Umoja wa Falme za Kiarabu imekuwa ikikabiliana na vitisho vya kushambuliwa kwa makombora na ndege zisizo na rubani, wizara yake ya ulinzi ilisema muda mfupi, kabla ya hotuba ya Rais wa Marekani Donald Trump.

    Wizara hiyo ilisema mashambulizi hayo yametoka Iran na kuwatahadharisha wananchi wake kuhusu sauti zinazosikika kote nchini wakati ikifanyashughuli ya kuzuia makombora hayo.

    Katika hotuba yake kwa taifa kuhusu vita vya Iran hapo awali, Trump aliishukuru UAE na washirika wengine wa Ghuba, ambao wamekosolewa na Iran kwa kulipiza kisasi mashambulizi ya Marekani na Israel.

    Trump alisema kuwa utawala wa Iran ulikuwa ukianzisha "mashambulizi ya kigaidi yaliyoharibika" dhidi ya meli za mafuta na nchi jirani ambazo "hazina uhusiano wowote na mzozo huo" alipokuwa akizungumzia wasiwasi kuhusu kupanda kwa bei ya nishati.

    Soma pia:

  8. Tazama wakati Artemis iIiporuka angani kwenye safari ya kihistoria

    Maelezo ya video, Tazama wakati Artemi IIiporuka angani kwenye safari ya kihistoria

    Kwa mara ya kwanza katika zaidi ya miaka 50, binadamu anarudi Mwezini, akisafiri zaidi kutoka duniani kuliko mtu mwingine yeyote aliyewahi kuwa hapo awali.

    Kazi hiyo maalumu ya Nasa ya Artemis II, ambayo imezinduliwa usiku wa kuamkia leo imeelezwa kuwa italeta uelewa mpya wa mazingira ya mwezi.

    Wanaanga wanne wanafanya safari hii ya kihistoria, baada ya maaandalizi ya miaka kadhaa na hatimaye Mamlaka ya Taifa ya Anga nchini Marekani NASA- kuizindua katka kituo cha anga cha Kennedy Artemis II.

    Maelezo zaidi:

  9. Vita vya Iran: Trump asema malengo ya Marekani 'yanakaribia kukamilika'

    Trump

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema nchi yake imepata mafanikio makubwa katika vita dhidi ya Iran, kufuatia mashambulizi ya pamoja na mshirika wake mkuu, Israel.

    Akilihutubia taifa juu ya vita hivyo amesema Marekani itamaliza kazi hiyo na kutishia kushambulia miundombinu ya nishati ya Iran ikiwa viongozi wapya wa nchi hiyo hawatafikia makubaliano.

    Katika hotuba hiyo iliyochukua takribani dakika ishirini, Trump amesema mashambulizi dhidi ya Iran, yaliyoanza mwezi mmoja uliopita, yamesababisha uharibifu mkubwa katika vituo vya urutubishaji wa nyuklia nchini Iran, pamoja na kuuawa kwa baadhi ya viongozi wa juu wa serikali hiyo.

    Amesisitiza kuwa hatua hizo zimeudhoofisha kwa kiasi kikubwa uongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

    Trump pia amesema kwa zaidi ya miaka 47, Iran imekuwa tishio kwa Marekani na nchi jirani, akitolea mfano jinsi mamlaka ya Tehran ilivyoshughulikia maandamano ya raia wake waliopinga utawala.

    Rais huyo amesisitiza kuwa Marekani haitaruhusu Iran kumiliki silaha za nyuklia, akidai kuwa vituo vingi vya urutubishaji wa urani vimeharibiwa vibaya.

    Soma zaidi:

  10. Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja leo Alhamisi 02.04.2026