Kutoka kwa Appolo hadi Artemis: Jinsi dunia ilivyobadilika katika miaka 58

Muda wa kusoma: Dakika 4

Baada ya wanaanga wa Apollo 8 kupiga picha maarufu ya Earthrise mwaka wa 1968, wanaanga wa Artemis walipiga picha nyingine kama hiyo, wakionyesha mabadiliko yanayoendelea katika sayari.

Wakati kamanda wa Apollo 8, Frank Borman, alipoona mwezi kwa mara ya kwanza kutoka kwenye chombo chao cha anga mwaka wa 1968, aliguswa sana na muonekano wake

"Uso wa Mwezi ulikuwa umeharibiwa sana na mashimo ya mabaki ya milipuko ya volkano," alisema katika mahojiano na BBC mwaka wa 2018. "Ulikuwa wa kijivu, mweusi au mweupe tu hakukuwa na rangi yoyote kwenye mwezi, na ulikuwa umevurugika kupita kiasi."

Lakini wakati chombo hicho kilipokamilisha mzunguko wake wa nne wa kuzunguka mwezi, ghafla walipata mandhari tofauti kabisa.

"Tuliangalia juu na tukauona dunia nyuma ya mwezi ikichomoza, na Bill Anders akapiga picha ambayo pengine ni moja ya picha muhimu zaidi zilizowahi kupigwa na binadamu," Borman alisema.

Mabadiliko ya tabianchi yamebadilisha sana uso wa dunia katika kipindi cha takriban miaka sitini iliyopita. Wataalamu wameiambia BBC kuhusu tofauti zinazoonekana kati ya picha za Earthrise na Earthset, na kile kinachoelezea kuhusu sayari.

Walipoulizwa na waandishi wa habari baada ya uzinduzi wa Artemis kuhusu mipango ya picha mpya ya Earthrise, ilionekana wazi kwamba NASA haikutaka kushtukia.

"Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha hilo linatokea," alisema Lori Glaze, ambaye anaongoza Idara ya Maendeleo ya Mifumo ya Utafiti ya shirika hilo.

Picha ya Earthset ilipigwa kupitia dirisha la chombo cha anga cha Orion, wakati wa safari ya saa saba karibu na mwezi.

"Upande wa Dunia unaoangazwa na jua unaonyesha mawingu meupe na maji ya buluu juu ya eneo la Oceania, huku maeneo meusi yakionyesha usiku. Picha hiyo pia inaonyesha kwa undani mkubwa uso wa mwezi wenye mashimo na mabonde," NASA ilifafanua picha hiyo.

Tofauti na mwaka wa 1968, mwaka wa 2026 setilaiti nyingi zimekuwa zikipiga maelfu ya picha za dunia kila siku.

Pia kuna mtiririko wa video kutoka Kituo cha Kimataifa cha Anga na vyombo vya anga visivyo na rubani pia vimeweza kupiga picha za dunia kutoka mwezini .

Hata hivyo, picha ya Earthset ilipigwa na binadamu wenyewe na ndiyo inayoifanya iwe ya kipekee na yenye maana zaidi.

Craig Donlon, ambaye anasimamia mipango ya kizazi kijacho cha setilaiti katika Shirika la Anga la Ulaya (ESA), anasema picha za binadamu huleta mtazamo tofauti.

"Picha zinazopigwa na binadamu huwa zimeundwa kwa fremu, zimezingatiwa kwa makini, na kuna maamuzi yanayofanywa kwa makusudi na bila kukusudia na mwanaanga anapobonyeza kifaa cha kupiga picha huwa ana kitu akilini mwake na hisia," anasema Donlon .

Lakini si tu uhusiano wa kibinadamu unaofanya picha za Earthrise na Earthset kuwa muhimu. Licha ya kuwa zimepigwa kwa tofauti ya takriban miaka 58, zinaweza pia kusaidia kuonyesha jinsi dunia ilivyobadilika katika kipindi hicho.

"Tangu picha ya Earthrise kuchukuliwa, kiwango cha kaboni katika anga kimeongezeka kwa takriban theluthi moja na joto la dunia limepanda kwa kasi, angalau kwa nyuzi joto 1°C," anasema Richard Allan, profesa wa sayansi ya tabianchi katika Kituo cha Kitaifa cha Ufuatiliaji cha National Centre for Earth Observation.

"Sayari imebadilika kadri shughuli za binadamu zinavyoongezeka. Muonekano wa ardhi kama inavyoonekana kutoka angani, miji ikipanuka, misitu imekatwa na kubadilishwa kuwa mashamba, na pia kuchangia kukauka kwa Bahari ya Aral ambayo imepungua hadi chini ya asilimia 10 ya ukubwa wake kuanzia mwaka wa 1960."

Baadhi ya mabadiliko hayo yanaweza hata kuonekana kwenye picha zenyewe, licha ya kwamba dunia imefunikwa na mawingu.

"Ingawa ni sehemu tofauti za dunia, jambo moja linaloonekana katika picha zote mbili, hata kama unaangalia maeneo tofauti, ni Antaktika na Bahari ya Kusini," anasema Benjamin Wallis, mtaalamu wa barafu katika Chuo Kikuu cha Leeds, Uingereza. "Rasi ya Antaktika ni mojawapo ya maeneo yanayopata joto kwa kasi zaidi duniani, na picha za sasa zinaonyesha kupungua kwa barafu."

Utafiti unaonyesha kwamba mabadiliko haya katika barafu ya Antaktika hayajawahi kutokea katika kipindi cha miaka 10,000 iliyopita. Maeneo mengine ya dunia ambako maji yapo katika hali ya barafu yanayojulikana kama cryosphere yameathiriwa pia.

"Dunia ukiitazama kutoka mbali inaonekana kuwa kitu kizuri sana, lakini unapokaribia, utaona madhara ya miaka 150 ya kile tunachokiita 'maendeleo',". "Lakini picha hiyo ilihamasisha kizazi chetu kuanzisha harakati za kulinda mazingira." anasema Kathleen Rogers, rais wa mtandao wa Earth Day.

Frank Borman alifariki mwaka wa 2023, lakini urithi wa misheni yake ya Apollo 8 bado unaendelea kudumu, na maneno yake bado yana umuhimu kwa kizazi kipya cha wanaanga wa mwezi, "Sidhani kama yeyote kati yetu alizingatia sana kwamba tungesafiri hadi mwezini na kuvutiwa zaidi kutazama dunia."