Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Waliniambia amekufa': Wanajeshi wa Uingereza waliotelekeza watoto Kenya kufuatiliwa
- Author, Josephine Casserly
- Author, Ivana Davidovic
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 6
"Edward", mvulana wa Kenya mwenye umri wa miaka tisa, siku zote amekuwa akijua kuwa baba yake alifanya kazi katika jeshi la Uingereza. Rangi yake ya ngozi nyeupe kuliko wenzake imesababisha kudhihakiwa kwa miaka mingi. Baba yake alitoweka kabla yeye hajazaliwa, akimuacha mama yake akiishi katika umaskini mkubwa na kutengwa na baadhi ya ndugu zake.
Sasa mwanaume, aliyefanya kazi ya ukandarasi katika kambi ya jeshi la Uingereza nchini Kenya, pamoja na wengine 19 waliowahi kuhudumu kama wanajeshi miaka ya nyuma, wametambuliwa kupitia mchakato wa kipekee wa vinasaba (DNA) na kisheria kuwa ni baba wa watoto waliozaliwa karibu na kambi hiyo, na wamepatikana. Uthibitisho wa kisheria tayari umefanywa katika kesi 12 na jaji mkuu wa Mahakama ya Familia ya Uingereza.
Mchakato huo unatoa majibu kwa watoto ambao hawakujua walikotoka au hata ni nani baba zao, au waliokuwa wameambiwa kuwa baba zao wamekufa. Wote wamekuwa wakitafuta kujua asili yao na wamekumbana na changamoto za kifedha. Wengi katika kesi hizo 12 zilizothibitishwa, sasa wanastahili kujiandikisha kupata uraia wa Uingereza. Wale walio chini ya miaka 18 au wanaoendelea na masomo watastahili kupata matunzo ya watoto.
Mwanasheria wa Uingereza, James Netto, na Kelvin Kubai, mwanasheria nchini Kenya, wanasema kuna karibu kesi 100 zilizorekodiwa za watoto waliozaliwa karibu na Kituo cha Mafunzo ya Jeshi la Uingereza nchini Kenya (Batuk) kwa wanajeshi wa Uingereza. Netto anaamini huenda kuna visa vingi zaidi.
Batuk, iliyoanzishwa mwaka 1964 na hupokea zaidi ya wanajeshi 5,000 wa Uingereza kila mwaka, imekuwa na utata mkubwa katika mji wa Nanyuki, ulioko takriban kilomita 185 kaskazini mwa Nairobi.
Uchunguzi wa bunge la Kenya uliotolewa Disemba mwaka jana ulituhumu wanajeshi wa Uingereza kufanya kazi katika "utamaduni wa kutoadhibiwa", hali iliyosababisha unyanyasaji wa kingono, madai mawili ya mauaji, ukiukwaji wa haki, uharibifu wa mazingira, na kuachwa au kutelekezwa kwa watoto wa eneo hilo.
Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilijibu kuwa "inasikitika sana kwa changamoto hizo zilizotokea kuhusiana na uwepo wa jeshi la Uingereza nchini Kenya… na itaendelea kuchukua hatua kuzishughulikia".
Awali, James Netto alipata taarifa kuhusu suala hili mwaka 2024, kisha akaungana na mtaalamu wa vinasaba (DNA) Profesa Denise Syndercombe Court na kufika Kenya wakiwa na vifaa vya kupima DNA. Walilinganisha sampuli hizo na data ya vinasaba iliyoko katika mifumo maalumu na kufanikiwa kuwabaini baba zao.
Netto anasema hawakutarajia mafanikio makubwa kiasi hicho, lakini waliweza kupata hata ndugu wa mbali hadi kufikia kuwabaini moja kwa moja baba halisi wa watoto hao.
Mafanikio hayo yameleta matumaini mapya kwa Edward (si jina lake halisi) na mama yake Nasibo, kwani sasa anaweza kupata msaada wa kifedha kutoka kwa baba yake.
Nasibo anasema awali aliamini wanajeshi wa Uingereza ni watu wema. Alisema baba wa mtoto wake alimpenda, alimpa matumaini na hata kumvalisha pete ya uchumba kabla ya kutoweka ghafla alipokuwa na ujauzito wa miezi minne.
Baada ya hapo, Nasibo alifukuzwa nyumbani na baadhi ya ndugu zake, huku mtoto wake akidhihakiwa shuleni kutokana na rangi yake ya ngozi.
"Nilikuwa naamini wao ni watu wenye heshima," Nasibo anasema akirejelea jeshi la Uingereza. Aliamini kuwa baba wa Edward alimpenda kwa dhati na kumjali. Tumeona barua ambayo mama wa mwanajeshi huyo (mama mkwe) alimwandikia Nasibo kabla hajapata ujauzito, akimshukuru kwa kumfanya mwanawe (huyo mwanajeshi) awe na furaha. Na pale Nasibo alipomwambia kuwa alikuwa na ujauzito, anasema alionekana kufurahia sana. Alimshauri kumpa mtoto jina la ndugu yake kama angekuwa mvulana, na akarudi kutoka safari yake Uingereza akiwa na pete ya uchumba.
Lakini Nasibo alipokuwa na ujauzito wa miezi minne, anasema mwanaume huyo alimwambia alipaswa kurejea Uingereza kwa dharura, kisha akakata mawasiliano yote.
Nasibo anasema baadhi ya ndugu zake walimlazimisha kuondoka nyumbani kwa familia, huku mwanawe akidhihakiwa shuleni kutokana na rangi yake ya ngozi iliyo nyepesi.
"Wanampa jina la utani 'mkoloni Muingereza'," alituambia. Uingereza ilitawala Kenya kuanzia mwaka 1895 hadi 1963.
Netto alifanikiwa kumpata baba wa Edward baada ya mahakama kuamuru taasisi za serikali ya Uingereza kutoa taarifa zake. Hata hivyo, mwanaume huyo hataki kuwasiliana na mtoto wake kwa sasa, na kesi inaendelea ili alazimishwe kutoa matunzo.
Kwa upande mwingine, msichana Yvonne mwenye miaka 18 alikua akiamini baba yake alikufa. Kupitia DNA, ilibainika kuwa yuko hai nchini Uingereza, ingawa hataki mawasiliano kwa sasa.
Sio baba wote wamekataa kuwajibika. Mwingine aitwaye Phill amekubali uhusiano na mtoto wake aitwaye Cathy na ameanza kumpa msaada wa kifedha, akisema anajuta muda aliopoteza.
Katika kipindi hicho, Phill anasema alikuwa ameacha jeshi na kwa muda fulani aliishi bila makazi huku akipambana na changamoto za afya ya akili. "Kuzoea maisha ya kiraia haikuwa rahisi," anasema.
Cathy pia alikuwa akipitia wakati mgumu, hali iliyofikia hatua ya kujaribu kujiua.
"Nilipokuwa nakua, nilihisi nilihitaji sana uwepo wa baba kwa sababu kuna mambo ambayo mama yangu hakuweza kuyaelewa kutokana na tofauti za rangi na mengineyo. Hilo lilinifanya nijisikie mpweke sana.
"Kuna sehemu ya maisha yako ambayo huijui kabisa. Ni kama fumbo kwako."
Baada ya baba yake kuthibitishwa hivi karibuni na mahakama za Uingereza, Phill anasema anafurahi kupatikana, akielezea hali hiyo kama "furaha kubwa isiyotarajiwa".
Anasema sasa anawasiliana na Cathy, na tayari ameanza kumpa yeye pamoja na Maggie msaada wa kifedha.
"Nilimwambia Cathy… haijalishi nitafanya nini, siwezi kamwe kufidia muda wote niliopoteza nikiwa mbali naye. Ninachoweza kufanya ni kujitahidi kadri niwezavyo."
Kwa sasa Cathy anatarajia kwenda Uingereza kumtembelea baba yake.
Netto anasema, kwa kadri anavyojua, Phill ndiye baba pekee miongoni mwa wateja wake ambaye ameanza kutuma fedha kwa watoto wake hadi sasa.
Tulimuuliza mwanasheria wa Kenya, Kelvin Kubai, ambaye ameanzisha shirika la misaada liitwalo Connecting Roots Kenya kuwasaidia kifedha watoto wa wanajeshi wa Uingereza, kama anaamini inapaswa kuwepo kwa marufuku ya wanajeshi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wazawa kutokana na idadi ya watoto wanaozaliwa nje ya ndoa kuongezeka. Alipinga vikali wazo hilo.
"Hili lingeonekana ni ubaguzi ni kama kusema wanajeshi ambao wengi ni weupe wawaepuke wanawake weusi kwa sababu wanaweza kuwaletea matatizo. Suluhisho pekee ni kuhakikisha wanaume hawa wanawajibishwa wanapopata watoto wakati wa kipindi chao cha mafunzo nchini Kenya."
Netto na Kubai wanasema kazi yao inaendelea, huku kesi zaidi zikitarajiwa kufikishwa katika Mahakama Kuu katika miezi ijayo.
Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilisema: "Iwapo hakuna tuhuma za jinai dhidi ya wanajeshi wa Uingereza, na hakuna malalamiko maalum yaliyotolewa na polisi wa eneo husika, basi wizara haitachunguza. Baadhi ya madai yanaweza kuhusishwa na mahusiano ya hiari, ambayo si kinyume na sera ya wizara."
Brigedia Simon Ridgway, kamanda wa kikundi cha mafunzo ya jeshi la Uingereza, aliongeza kuwa wale wanaobainika kuwa na watoto wanapaswa kuwasiliana na na mamlaka za Kenya, ambayo hushirikiana na Uingereza kutoa msaada na kushughulikia madai hayo.
Uchunguzi wa bunge la Kenya wa Disemba uliitaka serikali kuweka mifumo mipya ya kuwawajibisha wanajeshi wa Batuk, ikiwemo kuhakikisha wanatoa matunzo kwa watoto, kufanya vipimo vya DNA, na kutoa msaada wa kisaikolojia kwa watoto hao.