Kutana na 'mmiliki' wa mwezi aliyeuza ardhi mwezini na kuwa bilionea
Wakati wanaanga wanne wa misheni ya Artemis II wakiwa njiani katika safari ya siku nne kurejea duniani baada ya kusafiri umbali wa kihistoria wa zaidi ya kilomita 406,000 kuzunguka mwezi, mjadala kuhusu anga na uchunguzi wake umeibuka upya. Lakini mbali na sayansi na safari hii ya kipekee, kuna simulizi ya kushangaza inayozua swali, je ni nani anamiliki Mmwezi?
Jaribu kufikiria, umetoka kuachana na mpenzi wako, hauna pesa, halafu unapata wazo la ajabu kwamba "Nitauza mwezi na kujipatia kipato"
Najua inakaa wazo ambalo ni la kipekee
Lakini Dennis Hope, raia wa Marekani, alipata motisha ya kuuza mwezi. Alitajirika na kuwa milionea baada ya kuuza vipande vya ardhi kwenye mwezi miaka ya 1980.
Alifaulu kufanya hivyo kivipi? Dennis Hope aliweza kupata mwanya katika sheria na mikataba ya kimataifa, na kwa ujuzi mkubwa akaitumia kwa manufaa yake.
Maktaba
Baada ya kupata wazo hili la kipekee, aliamua kutafuta maelezo Zaidi.
Katika mahojiano na gazeti la Vice kipindi hicho, anasema alienda kwenye maktaba na kutafuta mkataba wa 1967 Outer Space Treaty.
Hati hii ya Umoja wa Mataifa inasema kuwa anga za juu ni rasilimali ya Pamoja ya kimataifa, "Ni mali ya kila mtu" kwa hivyo hakuna taifa inayomiliki anga au inaweza kudhibiti jiografia ya anga yoyote.
Kifungu cha pili cha mkataba huo kinasema kwamba "Mwezi na sayari hazimilikiwi au kudhibitiwa na taifa fulani au kutumiwa kama makazi"
Hope alisema kuwa "ikiwa inamilikiwa na kila mtu, basi haimilikiwi na mtu yeyote na kwanini mtu binafsi asiimiliki?" alisema katika mahojiano na BBC.
Chanzo cha picha, Juan BARRETO / AFP via Getty Images
Swali kubwa ni je, aliwezaje kumiliki mwezi?
Hope alitumia mwanya wa kisheria na kukosa kujibiwa na Umoja wa Mataifa.
Aliwasilisha madai kuwa anamiliki mwezi na sayari kwa Umoja wa Mataifa.
Katika barua hiyo alisema anapanga kugawanya mwezi kwa vipande na kumuuzia yeyote aliyetaka, na kusema kuwa iwapo watakuwa na changamoto yoyote ya kisheria wamwambie yeye.
Hakuna aliyejibu madai yake.
Kuuza mwezi
Kuanzia hapo alianza kuuza vipande vya ardhi kwenye mwezi, kwenye sayari ya Mars, Venus na Mercury, kupitia setilaiti.
Wanunuzi walikuwa watu maarufu kama marais wa zamani wa Marekani Ronald Reagan, Jimmy Carter na hoteli kubwa kama Hilton na Marriot.
Pia inasemekana kuwa Rais wa zamani wa Marekani George Bush anamiliki ardhi kwenye mwezi.
Hope aliiambia BBC mwaka wa 2007 kuwa aliuza vipande vya ardhi 1500 kwa siku, na ilibidi achague ni nani atauzia kwa kufumba macho na kuchagua majina na kuchagua ardhi kwenye mwezi kupitia ramani.
"Haikuwa njia ya kisayansi ila ilinipa furaha" alisema Hope
Inasemekana Hope alipata faida ya takriban dola million 12, na kusema ni pesa pekee amewahi kumiliki tangu mwaka wa 1995.
Chanzo cha picha, VALENTINA PETROVA/AFP via Getty Images
"Ardhi ndogo zaidi unayoweza kununua kutoka kwetu ni ekari moja. Ardhi kubwa zaidi tunayouza ni ile tunayoita 'ardhi yenye ukubwa wa bara' ya ekari 5,332,740, ambayo inagharimu dola za Marekani million 13,331,000," aliiambia gazeti la Vice.
"Bado hatujauza ukubwa wa aina hiyo ya ardhi, lakini tumeuza vipande vingi vya ekari 1,800 na 2,000 . Tuna makampuni makubwa Zaidi ya 1,800 kote duniani ambayo yamenunua ardhi kutoka kwetu kwa madhumuni yao maalum ikiwemo hoteli za Hilton na Marriot." Aliongezea
Katiba ya Kiastronomia
Najua unawaza ni vipi umiliki wa ardhi hizo ungedhibitishwa.
Hope na wamiliki wengine wote waliwaza kuhusu hili na wakapata suluhisho.
Hope alielezea kuwa, waliamua kuanzisha jamhuri ya kidemokrasia inayoitwa "Serikali ya Galactic".
"Ilituchukua miaka mitatu kuandaa Katiba, na tukaichapisha mtandaoni mwezi Machi mwaka wa 2004, wakati huo tulikuwa wamiliki milioni 3.7 na kura 173,562 kwa ajili ya kupitishwa kwa katiba hiyo. Baada yah apo tulikuwa taifa huru lenye katiba iliyopitishwa kikamilifu," alisema.
"Tunaendelea kudumisha uhusiano wa kidiplomasia na serikali 30 duniani kote na tunajaribu kupata idadi kubwa iwezekanavyo kututambua, kwa sababu nia yetu ni kujiunga na shirika la fedha duniani IMF."
BBC haijaweza kuthibitisha madai haya yaliyotolewa na Hope.
Raia wa Chile aliyejaribu kumiliki mwezi
Mwaka 1936, hata kabla ya binadamu kuwaza uwezekano wa kutua kwenye mwezi, Dean Lindsay alidai kumiliki siyo tu mwezi, bali pia wa sayari yote ya angani. Pia alipokea maombi ya watu waliotaka kununua na kumiliki ardhi angani.
Jenaro Gajardo Vera pia alifanya vivyo hivyo.
Wakili huyo aliyezaliwa nchini Chile mwaka wa 1919, alidai kuwa tarehe 25 mwezi Septemba mwaka 1954, kuwa ana miliki mwezi na ana hati kamili za umiliki huo.
Chanzo cha picha, Archivo Judicial de Chile/BBC
Uthibitisho wa umiliki huo ulikuwa ni nyaraka iliyotiwa saini na wakili mmoja mkuu katika jiji la Talca, katikati mwa Chile, takriban kilomita 255 kutoka mji mkuu wa nchi hiyo. Hati hiyo sasa inahifadhiwa na mahakama ya Santiago.
Hati hiyo inasema kuwa
"Jenaro Gajardo Vera, wakili, amekuwa mmiliki,kabla ya mwaka 1857, akiunganisha umiliki wake na ule wa mababu zake, anamiliki mwezi na maeneo ya karibu nayo"
Umiliki wa mwezi
Hope anaendelea na biashara yake ya kuuza ardhi za angani miundo mingine ya kiastronomia, lakini licha ya hayo, wataalamu wanasema mwezi hauna mmiliki. Angalau si kwa njia halali.
Mkataba wa kimataifa wa mwaka 1967 unaweka wazi kwamba uchunguzi na matumizi ya anga yanapaswa kunufaisha mataifa yote.
Je, mtu binafsi anaweza kujitangaza kuwa mmiliki wa mwezi?
"Hapana," alisema Claire Finkelstein, profesa wa sheria katika chuo kikuu cha Pennsylvania.
Inapokuja katika suala la uchimbaji wa rasilimali za angani, sheria haiko wazi.
"Sheria za kimataifa hazieleweki vizuri kuhusu kampuni binafsi kuanzisha shughuli za uchimbaji angani," alisema Ian Crawford, profesa wa Sayansi ya Sayari katika chuo cha Birkbeck College mjini London.
"Ni lazima Mkataba wa Anga za Juu (Outer Space Treaty), isahihishwe na kuandikwa tena" alisema.
Lakini hadi wakati huu, na kwa mujibu wa sheria za anga, Mwezi hauna mmiliki binafsi.
Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula na kuhaririwa na Ambia Hirsi
Habari kuu
Gumzo mitandaoni
Zinazovuma zaidi
Haipatikani tena