Tangazo la Trump kusitisha mapigano 'halina maana yoyote' - Iran
Mshauri mwandamizi wa Iran amesema kuwa tangazo la kusitisha mapigano lililotolewa na rais wa Marekani Donald Trump “halina maana yoyote” na linaonekana kuwa ni mbinu ya kuvuta muda ili kutekeleza shambulio la kushtukiza.
Mahdi Mohammadi, ambaye ni mshauri wa spika wa bunge la Iran Mohammad Bagher Ghalibaf, aliandika kwenye mtandao wa X kwa lugha ya Kiajemi kwamba kuendelea kwa kile alichokiita “hali ya kuzingirwa” inayofanywa na Trump hakutofautiani na mashambulizi ya mabomu, na kunapaswa kujibiwa kijeshi.
Aidha aliongeza kuwa “wakati umefika kwa Iran kuchukua hatua mapema.”
Wakati huo huo, Jeshi la wanamaji la Marekani limekuwa likizuia eneo la Mlango Bahari wa Hormuz, na wanajeshi wake walivamia meli ya mizigo iliyokuwa na bendera ya Iran siku ya Jumapili.
Hii inakuja baada ya Iran kufunga kwa muda njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani kwa wiki kadhaa.