Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump aongeza muda wa kusitisha mapigano Iran

Hatua ya Rais wa Marekani, Donald Trump kukubali kuongeza muda wa kusitisha mapigano na Iran bila kikomo maalum inatajwa kuwa ni mabadiliko makubwa ikilinganishwa na msimamo wake wa saa chache zilizopita.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Martha Saranga

  1. Rwanda: Serikali yaagiza asilimia 30% ya magari ya taasisi za umma yawe ya umeme

    Serikali ya Rwanda imeziagiza taasisi zake kuhakikisha kuwa angalau asilimia 30 ya magari mapya yanayonunuliwa ni ya umeme.

    Hatua hii inalenga kupunguza utegemezi wa mafuta ya petroli na dizeli pamoja na kupunguza uzalishaji wa gesi chafu.

    Kwa mujibu wa Wizara ya Miundombinu, taasisi zote za serikali zinapaswa kuoanisha mipango yao ya ununuzi wa magari na sera ya taifa ya ununuzi endelevu.

    Agizo hilo limetolewa kupitia barua ya tarehe 14 Aprili iliyoandikwa na Naibu Waziri wa miundombinu, Jean de Dieu Uwihanganye.

    Hatua hii inakuja wakati bei za mafuta zikiendelea kupanda nchini humo na katika ukanda.

    Bei ya petroli imepanda hadi faranga 2,938 kwa lita kutoka 1,989 mwezi uliopita, huku dizeli ikiongezeka kutoka faranga 1,948 hadi 2,205 kwa lita.

    Wakati huo huo, matumizi ya magari ya umeme yanaongezeka kwa kasi nchini Rwanda.

    Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa hadi mwisho wa mwaka 2024, zaidi ya magari 7,000 ya umeme yalikuwa tayari yamesajiliwa.

    Ili kuhamasisha matumizi yake, serikali pia imepunguza kodi kwa magari hayo, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuhamia kwenye usafiri rafiki kwa mazingira.

    Soma zaidi:

  2. Kim Jong-un afichua anakotoa fedha za ujenzi wa makombora

    Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa, Korea Kaskazini inajipatia mamilioni ya dola kupitia fedha za mtandaoni ili kufadhili programu zake ghali za kutengeneza makombora.

    Wachunguzi wanaoshughulikia suala hilo walisema kuwa dola milioni 50 za kidijitali ziliibwa kati ya mwaka 2020 na 2021 kupitia udukuzi wa mtandaoni.

    Maafisa wanasema kuwa mbinu hii ya kuvamia mifumo ya benki ni chanzo kikubwa cha mapato kwa Korea Kaskazini, kinachotumika kufadhili silaha zake za nyuklia na makombora ya masafa marefu.

    Iliripotiwa kuwa taarifa hizo ziliwasilishwa kwa Kamati ya Vikwazo ya Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa.

    Mashambulizi hayo ya mtandaoni yalilenga angalau maeneo matatu katika United States, Ulaya na Asia.

    Ripoti hiyo pia ilinukuu utafiti uliotolewa mwezi uliopita na kampuni ya usalama ya Chainalysis, uliobaini kuwa mashambulizi ya mtandaoni ya Korea Kaskazini yalisababisha upotevu wa dola milioni 400 za sarafu za kidijitali mwaka uliopita.

    Umoja wa Mataifa ulisema katika mojawapo ya ripoti zake za mwaka 2019 kuwa Korea Kaskazini ilipata dola bilioni mbili kupitia ulaghai wa mtandaoni ili kufadhili maendeleo ya silaha zake za maangamizi makubwa.

    Soma zaidi:

  3. Tangazo la Trump kusitisha mapigano 'halina maana yoyote' - Iran

    Mshauri mwandamizi wa Iran amesema kuwa tangazo la kusitisha mapigano lililotolewa na rais wa Marekani Donald Trump “halina maana yoyote” na linaonekana kuwa ni mbinu ya kuvuta muda ili kutekeleza shambulio la kushtukiza.

    Mahdi Mohammadi, ambaye ni mshauri wa spika wa bunge la Iran Mohammad Bagher Ghalibaf, aliandika kwenye mtandao wa X kwa lugha ya Kiajemi kwamba kuendelea kwa kile alichokiita “hali ya kuzingirwa” inayofanywa na Trump hakutofautiani na mashambulizi ya mabomu, na kunapaswa kujibiwa kijeshi.

    Aidha aliongeza kuwa “wakati umefika kwa Iran kuchukua hatua mapema.”

    Wakati huo huo, Jeshi la wanamaji la Marekani limekuwa likizuia eneo la Mlango Bahari wa Hormuz, na wanajeshi wake walivamia meli ya mizigo iliyokuwa na bendera ya Iran siku ya Jumapili.

    Hii inakuja baada ya Iran kufunga kwa muda njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani kwa wiki kadhaa.

  4. Rais wa Taiwan afuta ziara yake Afrika baada ya kufungiwa anga

    Rais wa Taiwan, Lai Ching-te, amefuta ziara yake katika taifa la Eswatini, akidai kuwa Beijing imeweka shinikizo kwa mataifa jirani ili kuzuia ndege yake kupita katika anga lao.

    Nchi za Seychelles, Mauritius na Madagascar zilifuta vibali vya anga kwa ndege ya Lai baada ya “shinikizo kubwa” na mbinu za kiuchumi kutoka China, kwa mujibu wa afisa wa Taiwan.

    China ilikanusha kutumia shinikizo hilo, huku ikiyasifu mataifa hayo matatu na kusema ina “thamani kubwa” kwao.

    Hii ni mara ya kwanza kufahamika hadharani ambapo kiongozi wa Taiwan amelazimika kufuta safari ya nje kutokana na kufutwa kwa vibali vya kupita anga za nchi nyingine.

    Eswatini, iliyojulikana zamani kama Swaziland, ndiyo mshirika pekee wa kidiplomasia wa Taiwan barani Afrika.

    Ni moja ya nchi 12 pekee nyingi zikiwa ndogo katika Amerika ya Kusini au Pasifiki zinazoitambua Taiwan.

  5. Matumaini ya mazungumzo ya amani Pakistan yafifia

    Donald Trump amejigamba kuhusu mabadiliko ya utawala huko Tehran lakini sasa anashughulika na kile anachokiita kupasuka kwa utawala.

    Sasa kwa kuwa viongozi wengi wakuu wa Iran wamefariki , swali la nani anayeongoza Iran kwa sasa ni halisi zaidi, jambo linalofanya jitihada za kidiplomasia kuwa ngumu zaidi.

    Huenda ni mapema kutathmini athari za hatua ya hivi karibuni ya rais, lakini dalili za awali kutoka Tehran hazionekani kuwa nzuri.

    Mshauri wa spika wa bunge na pia kiongozi wa mazungumzo, Mohammad Bagher Ghalibaf, amesema kuwa Trump anajaribu kuvuta muda kwa ajili ya kutekeleza shambulio jingine la kushtukiza.

    Msemaji wa jeshi alirejelea onyo kwamba Iran ilikuwa tayari kushambulia ikiwa hilo litatokea.

    Aidha Islamabad, mipango bado inaendelea kwa ajili ya duru nyingine ya mazungumzo, huku sehemu za jiji zikiwa bado zimefungwa. Lakini matumaini ya mkutano wiki hii yanaonekana, kwa sasa, yamefifia.

  6. Iran haijaamua kushiriki duru ijayo ya mazungumzo na Marekani - Msemaji

    Kabla ya Donald Trump kutangaza kwamba ataongeza muda wa kusitisha mapigano, wizara ya mambo ya nje ya Iran iliiambia BBC kwamba Tehran bado haijaamua kama itahudhuria duru mpya ya mazungumzo ya amani na Marekani baadaye wiki hii.

    Katika mahojiano na mwandishi wa kimataifa wa BBC Lyse Doucet, msemaji Esmail Baghaei alisema Iran imeingia katika duru ya kwanza ya mazungumzo ya Islamabad "kwa nia njema na hisia ya uzito, lakini kuna upande wa mazungumzo umeonyesha kukosa umakini na nia njema".

    Aidha alitaja "mapumziko yasiyo na maana, vitisho vya uhalifu wa kivita" kutoka kwa Marekani akirejelea mfululizo wa machapisho na mahojiano ya Trump kwenye mitandao ya kijamii katika siku mbili zilizopita, ambapo alitishia tena “kuharibu kila kituo cha umeme na kila daraja” ikiwa Iran haitakubali kile alichokiita pendekezo la Marekani “la haki na lenye busara sana.”

    White House ilithibitisha Jumanne usiku kuwa safari ya makamu wa rais JD Vance kwenda Pakistan kwa ajili ya duru ya pili ya mazungumzo ya amani imefutwa.

  7. Kufungwa kwa Mlango wa Hormuz kwaongeza uhitaji wa mafuta Marekani - Wataalamu

    Kupitia chapisho kwenye jukwaa la mtandao wa Truth Social Jumatatu usiku, Rais Donald Trump alisema uongozi wa Iran "umelazimisha mamia ya meli" kuelekea majimbo yenye utajiri wa mafuta ya Marekani, kama vile Texas, Louisiana, na Alaska.

    Ingawa haijulikani ni aina gani ya meli alizokuwa akizirejelea, wachambuzi wa meli na biashara wanaiambia BBC Verify kwamba hatua ya Iran kufunga Mlango Bahari wa Hormuz imesababisha ongezeko la uhitaji wa mafuta ghafi nchini Marekani.

    Hatua hiyo ni kikwazo kikubwa cha usafirishaji wa mafuta ya Ghuba, lakini usafirishaji umevurugika zaidi tangu kuanza kwa vita vya Marekani na Israeli dhidi ya Iran mnamo Februari 28.

    Kwa kuwa hawawezi kupata mafuta ghafi kutoka Mashariki ya Kati kupitia mlango huo, waagizaji wamelazimika kutafuta wauzaji mbadala.

    Data kutoka kwa kampuni ya ufuatiliaji wa safari za bahari Kpler inaonyesha kuwa meli 71 za mafuta zinazojulikana kama Very Large Crude Carriers (VLCCs) zinaelekea Marekani kuchukua mizigo ikilinganishwa na wastani wa meli 27 kwa siku katika kipindi cha mwaka jana.

  8. Majadiliano na Marekani hayana mantiki kwa sasa – Iran

    Mahmoud Nabavian, mbunge wa Iran ambaye alikuwa sehemu ya ujumbe katika duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya Iran na Marekani huko Islamabad, ameeleza kupitia mtandao wa X kwamba "kuanzia sasa", kujadiliana na Marekani ni "jambo la hatari na lisilo na mantiki".

    Kando na hayo, msemaji wa makao makuu ya Khatam al-Anbiya ya Iran, kamandi kuu ya kijeshi ya Iran, ameonya kwamba vikosi vya Iran, iwapo kutakuwa na shambulio dhidi ya Iran, "vitashambulia maeneo yaliyopangwa awali na kutoa somo, hata kali zaidi" kwa Marekani na Israeli.

    Katika chapisho la Nabavian na taarifa ya Khatam al-Anbiya, hakukutajwa muda wa kusitisha mapigano, ingawa vyote viliripotiwa na vyombo vya habari vya Iran baada ya tangazo la Donald Trump.

    Bado Iran haijatoa kauli yoyote kupitia wizara ya mambo ya nje ya Iran au maafisa wake, au kutoka kwa msemaji mkuu wa bunge la Iran Mohammad Bagher Ghalibaf.

  9. Waziri mkuu wa Pakistan amshukuru Trump kwa kuongeza muda wa kusitisha mapigano

    Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif amemshukuru rais wa Marekani Donald Trump baada ya kutangaza kuongeza muda wa kusitisha mapigano kwa muda usiojulikana muda mfupi kabla ya muda wa awali kuisha.

    "Ninamshukuru Rais Trump kwa dhati kwa kukubali ombi letu la kuongeza muda wa kusitisha mapigano ili kuruhusu juhudi zinazoendelea za kidiplomasia kuchukua mkondo wake," anasema katika taarifa ya mtandaoni.

    "Kwa imani na imani iliyopo, Pakistan itaendelea na juhudi zake za dhati za utatuzi wa migogoro kwa mazungumzo," taarifa hiyo inaongeza.

    "Ninatumai kwa dhati kwamba pande zote mbili zitaendelea kuzingatia usitishaji mapigano na kuweza kuhitimisha 'Makubaliano ya amani' kamili wakati wa duru ya pili ya mazungumzo yaliyopangwa kufanyika Islamabad kwa ajili ya kukomesha kabisa mgogoro huo."

  10. Trump aongeza muda wa kusitisha mapigano Iran

    Rais wa Marekani Donald Trump anasema Marekani itaongeza muda wa kusitisha mapigano na Iran, kwa ombi la Pakistan, na kuendelea na vizuizi vya kijeshi katika bandari za Iran.

    Tangazo la Donald Trump kwamba amekubali kuongeza muda wa kusitisha mapigano na Iran bila kikomo maalum ni mabadiliko makubwa ikilinganishwa na msimamo wake wa saa chache zilizopita.

    Trump alisema kupitia mitandao ya kijamii "kwa kuzingatia kwamba serikali ya Iran imegawanyika sana, jambo ambalo halikutarajiwa kuwa tofauti, na kufuatia ombi la Field Marshal Asim Munir pamoja na Waziri Mkuu Shehbaz Sharif wa Pakistan, tumeombwa kusitisha shambulio letu dhidi ya nchi ya Iran hadi wakati ambapo viongozi wao na wawakilishi wao wataweza kuwasilisha pendekezo la pamoja"

    Aliongeza; "kwa hiyo, nimeelekeza jeshi letu kuendelea na zuio, na katika mambo mengine yote, liendelee kuwa tayari kikamilifu. Hivyo basi, nitaongeza muda wa kusitisha mapigano hadi pendekezo lao litakapowasilishwa na mazungumzo kukamilika, kwa namna yoyote ile.”

    Awali akizungumza na CNBC, Trump alisema “natarajia tutakuwa tunashambulia” na kwamba jeshi lilikuwa “tayari kabisa kuanza.” Aidha alirejea tishio lake la kuharibu madaraja yote na mitambo ya umeme nchini Iran.

    Hata hivyo, saa chache kabla ya muda wa awali wa kusitisha mapigano kuisha, amekubali kusitisha mapigano kwa muda usio na kikomo. Katika kipindi chote cha mgogoro huu, Trump amejaribu kutumia vitisho dhidi ya serikali ya Iran kwa matamshi makali. Sasa inaonekana dhahiri hataki kuanza tena kuhusu mashambulizi dhidi ya Iran.

  11. Karibu katika habari zetu za moja kwa moja leo Aprili 22, 2026