Kufungwa kwa Mlango wa Hormuz kwaongeza uhitaji wa mafuta Marekani - Wataalamu

Chanzo cha picha, Getty Images
Kupitia chapisho kwenye jukwaa la mtandao wa Truth Social Jumatatu usiku, Rais Donald Trump alisema uongozi wa Iran "umelazimisha mamia ya meli" kuelekea majimbo yenye utajiri wa mafuta ya Marekani, kama vile Texas, Louisiana, na Alaska.
Ingawa haijulikani ni aina gani ya meli alizokuwa akizirejelea, wachambuzi wa meli na biashara wanaiambia BBC Verify kwamba hatua ya Iran kufunga Mlango Bahari wa Hormuz imesababisha ongezeko la uhitaji wa mafuta ghafi nchini Marekani.
Hatua hiyo ni kikwazo kikubwa cha usafirishaji wa mafuta ya Ghuba, lakini usafirishaji umevurugika zaidi tangu kuanza kwa vita vya Marekani na Israeli dhidi ya Iran mnamo Februari 28.
Kwa kuwa hawawezi kupata mafuta ghafi kutoka Mashariki ya Kati kupitia mlango huo, waagizaji wamelazimika kutafuta wauzaji mbadala.
Data kutoka kwa kampuni ya ufuatiliaji wa safari za bahari Kpler inaonyesha kuwa meli 71 za mafuta zinazojulikana kama Very Large Crude Carriers (VLCCs) zinaelekea Marekani kuchukua mizigo ikilinganishwa na wastani wa meli 27 kwa siku katika kipindi cha mwaka jana.



