EU yataka wataalamu wa nyuklia washirikishwe katika mazungumzo ya amani na Iran

Chanzo cha picha, Reuters
Mbali na kuongezwa kwa muda wa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Lebanon, mkuu wa sera za mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa vitisho kutoka Iran vinaweza kuwa “hatari zaidi” ikiwa wataalamu wa nyuklia hawatahusishwa katika mazungumzo ya amani.
Akizungumza katika mkutano wa viongozi wa EU huko Cyprus, Kaja Kallas anasema kuna hatari kwamba makubaliano yoyote yanaweza kuwa dhaifu kuliko makubaliano ya nyuklia ya Iran yaliyokubaliwa mwaka 2015 wakati wa utawala wa Obama, ambayo Rais Trump alijiondoa katika muhula wake wa kwanza.
Chini ya makubaliano hayo Iran ilikubali kupunguza shughuli zake nyeti za nyuklia na kuruhusu wakaguzi wa kimataifa kuingia nchini humo ili kuondoa vikwazo vya kiuchumi.
"Ikiwa mazungumzo hayo yanahusu tu mpango wa nyuklia na hakuna wataalamu wa nyuklia wanaohusishwa, basi tutaishia kuwa na makubaliano dhaifu kuliko JCPOA," Kallas anasema.








