Rais wa Uganda apuuza wasiwasi wa bei ya mafuta, aeleza vipaumbele vipya
Rais wa Uganda Yoweri Museveni amepuuza wasiwasi kuhusu bei ya juu ya mafuta kwa madereva, akisema wale wasioweza kumudu wanapaswa kubaki nyumbani na kwamba hahusiki na watu wanaosafiri kwa burudani, ikiwemo kwenda vilabu vya usiku.
Akizungumza katika Mkutano wa Africa We Build Summit 2026, Museveni alisema wasiwasi wake mkuu katika mazungumzo yake ya hivi karibuni na Rais William Ruto haukuwa ongezeko la gharama ya mafuta ya magari, bali bei ya mafuta ya ndege.
Alieleza kuwa mafuta ya ndege yana nafasi muhimu zaidi ya usafiri wa anga, akibainisha mchango wake katika sekta ya utalii na biashara ya mauzo ya nje, akionya kuwa gharama kubwa zinaweza kupunguza idadi ya wageni na kuathiri biashara.
Museveni alisisitiza umuhimu wa kupunguza bei ya mafuta ya ndege ili kuimarisha sekta muhimu za uchumi, huku akipuuza athari za bei ya juu ya mafuta kwa wamiliki wa magari.
“Msingemhangaisha sana Rais Ruto kuhusu mafuta, hasa watu wanaoendesha magari barabarani. Kama mafuta ni ghali, kaeni nyumbani, mnaenda wapi,” alisema.
“Sijali sana kuhusu nyinyi. Nilichokuwa nachojali ni mafuta ya ndege, kwa sababu si ya safari tu, bali pia utalii. Kama gharama ya mafuta ya ndege ni kubwa, watalii hawatakuja. Pia hutumika katika usafirishaji wa bidhaa nje kwa kuwa ndege zinatumika. Watu wanaoenda vilabu vya usiku na mambo mengine, siwajali sana. Kama huna fedha, kaa nyumbani. Unaenda wapi?”
Kiongozi huyo wa Uganda aliongeza kuwa amezitaka Kenya na Uganda kuwa na msimamo wa pamoja kuhusu usimamizi wa bomba la mafuta, hasa katika kuhakikisha uthabiti wa upatikanaji na bei ya mafuta ya ndege.
“Ndiyo maana nilizungumza na Rais Ruto ili serikali za Kenya na Uganda ziwe na sauti moja kuhusu bomba la mafuta, hasa kwa sababu ya mafuta ya ndege,” alisema.
Kauli yake inajiri wakati ambapo nchi za Afrika Mashariki zinakabiliwa na gharama ya juu ya maisha, inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na bei ya juu ya mafuta.
Soma zaidi: