Familia ya Lungu yalaani kuondolewa kwa mwili na uchunguzi bila idhini
Familia ya aliyekuwa Rais wa Zambia Edgar Lungu imeshutumu mamlaka za Afrika Kusini na maafisa wa Zambia kwa kuondoa mwili wake kinyume cha sheria na kufanya uchunguzi wa maiti bila idhini, kwa mujibu wa taarifa yao.
Familia hiyo imesema polisi na wawakilishi wa Zambia waliuchukua mwili huo kutoka katika chumba cha kuhifadhia maiti jijini Johannesburg tarehe 22 Aprili, wakitaja amri ya mahakama ya mwaka 2025. Imesema amri hiyo iliruhusu tu urejeshaji wa mwili nchini Zambia na haikuruhusu uchunguzi wa kitaalamu wa kitabibu.
Mwili huo ulipelekwa katika kituo cha serikali jijini Pretoria, ambapo maafisa walifungua jalada wakitaja “shaka ya sumu,” madai ambayo familia hiyo imeyapinga.
Mawakili wa familia walipata amri ya dharura ya Mahakama Kuu baadaye siku hiyo, ikiagiza mamlaka kurejesha mwili na kueleza kwa nini hawapaswi kudharauliwa mahakama.
Familia imesema licha ya amri hiyo, uchunguzi wa maiti ulifanyika siku iliyofuata kabla ya mwili kurejeshwa tarehe 23 Aprili.
Mamlaka za Afrika Kusini na serikali ya Zambia bado hazijatoa majibu ya hadharani kuhusu tuhuma hizo.
Lungu, aliyekuwa Rais wa Zambia kuanzia mwaka 2015 hadi 2021, alifariki miezi kumi iliyopita.