Israel yaua wanahabari watatu katika shambulio la anga nchini Lebanon

Israel imekuwa ikituhumiwa kulenga wanahabari nchini Lebanon tangu vita ya Iran kuanza. Wiki iliyopita, mtangazaji maarufu wa Al Manar, Mohammad Sherri, na mkewe waliuawa katika shambulio lingine dhidi ya wanahabari.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Martha Saranga

  1. Waandishi wa habari watatu wauawa katika shambulio la Israel nchini Lebanon

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waandishi wa habari watatu wa Lebanon wameripotiwa kuuawa baada ya gari lao la kazi kushambuliwa na ndege ya Israel kusini mwa nchi hiyo, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani.

    Waliofariki ni pamoja na mwandishi wa Al Manar TV, Ali Shoeib, pamoja na wanahabari wa Al Mayadin, Fatima na Mohamed Fetoni, ambao waliuawa katika shambulio la anga katika mji wa Jezzine.

    Rais wa Lebanon, Joseph Aoun, amelilaani shambulio hilo akilitaja kuwa “uhalifu wa wazi” unaokiuka sheria za kimataifa, ambazo zinataka wanahabari kulindwa wakati wa vita.

    Jeshi la Israel limethibitisha kumuua Ali Shoeib katika shambulio hilo, lakini limedai kuwa alikuwa mshirika wa Hezbollah akijifanya mwandishi wa habari.

    Hili ni tukio la pili ndani ya muda mfupi ambapo Israel imetuhumiwa kulenga wanahabari nchini Lebanon tangu vita kuanza. Wiki iliyopita, mtangazaji maarufu wa Al Manar, Mohammad Sherri, na mkewe waliuawa katika shambulio lingine lililolengwa.

    Tangu kuanza kwa mashambulizi hayo, zaidi ya raia 1,100 wameuawa nchini Lebanon, wakiwemo watoto 120 na wahudumu wa afya 42. Wengi nchini humo wanaeleza wasiwasi kuwa Israel inatumia mbinu zinazofanana na zile ilizotuhumiwa kutumia Gaza, ikiwa ni pamoja na kulenga raia, wanahabari na wahudumu wa afya, madai ambayo Israel imekuwa ikiyakanusha.

  2. Iran yadai kuharibu ghala la mifumo ya Ukraine Dubai, Kyiv yakana vikali

    s

    Chanzo cha picha, Middle East Eye

    Iran imedai kuharibu ghala lililokuwa likihifadhi mifumo ya kupambana na ndege zisizo na rubani (anti-drone) inayodaiwa kumilikiwa na Ukraine katika mji wa Dubai, katika operesheni iliyohusisha vikosi vyake vya anga na majini.

    Kwa mujibu wa msemaji wa makao makuu ya kijeshi ya Khatam al-Anbiya, Ebrahim Zolfaghari, ghala hilo lilikuwa likitumika kuhifadhi vifaa vya kijeshi vya Ukraine vinavyodaiwa kusaidia operesheni za Marekani. Aliongeza kuwa watu 21 wa Ukraine walikuwepo katika eneo hilo wakati wa shambulio hilo, lakini hakukuwa na taarifa kuhusu hatima yao.

    Hata hivyo, Ukraine imekanusha vikali madai hayo, ikisema taarifa hiyo si ya kweli. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ukraine, Heorhii Tykhyi, amesema kuwa ni “uongo” na kuishutumu Iran kwa kueneza taarifa za upotoshaji.

    Kauli hiyo ya Ukraine imekuja muda mfupi baada ya vyombo vya habari vya Iran kuripoti kuhusu tukio hilo, huku mvutano ukiendelea kuongezeka katika ukanda huo.

    Tukio hili linajiri wakati rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akiendelea na ziara katika baadhi ya nchi za Ghuba, akilenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia katika kipindi hiki cha mvutano wa kimataifa.

  3. Yaliyojiri saa 24 zilizopita vita ya Iran, mashambulizi kila kona Mashariki ya Kati

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mashambulizi yameendelea katika eneo la Ghuba katika saa 24 zilizopita, huku makombora yakiripotiwa kupiga mji mkuu wa Iran, Tehran, usiku kucha, wakati Iran ikiendelea kurusha makombora kuelekea Israel na nchi nyingine za ukanda huo.

    Mamlaka nchini Israel, zinasema mwanaume mwenye umri wa miaka 52 amefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya kombora kulenga eneo la katikati mwa Israel mwishoni mwa Ijumaa.

    Jeshi la Israel (IDF) pia limesema limefanikiwa kuzuia kombora lililorushwa kutoka Yemen kuelekea Israel.

    Nchini Oman, mfanyakazi wa kigeni amejeruhiwa baada ya ndege zisizo na rubani (drones) kulenga bandari ya Salalah, kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la nchi hiyo.

    Wakati huo huo, mifumo ya ulinzi wa anga imewashwa katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Kuwait na Bahrain, ambapo ndege zisizo na rubani kadhaa zimedunguliwa.

    Nchini UAE, watu watano walijeruhiwa baada ya kombora kuzuiwa katika mji mkuu Abu Dhabi.

    Wizara ya Ulinzi ya Saudi Arabia imesema imefanikiwa kuzuia ndege tatu zisizo na rubani pamoja na kombora la balistiki lililokuwa likielekea mji mkuu Riyadh.

    Mashambulizi haya yanajiri kufuatia tukio la Ijumaa ambapo wanajeshi wasiopungua 12 wa Marekani walijeruhiwa baada ya shambulio katika kambi ya anga ya Prince Sultan nchini Saudi Arabia.

  4. Wahamiaji 22 wafariki baada ya kukaa siku sita baharini

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Ugiriki imekuwa na matukio mengi yanayohusisha wahamiaji kupoteza maisha baharini

    Wahamiaji 22 wameripotiwa kufariki dunia karibu na pwani ya Ugiriki baada ya kukaa kwa siku sita baharini wakiwa ndani ya boti ya mpira.

    Shirika la habari la AFP likinukuu manusura waliotoa taarifa hizo kwa walinzi wa pwani wa nchi hiyo.

    Kwa mujibu wa taarifa hizo, manusura walieleza kuwa walikuwa wakisafiri katika mazingira magumu baharini kwa siku kadhaa kabla ya tukio hilo, hali iliyosababisha vifo vya watu hao.

    Watu 26 waliokolewa na chombo cha shirika la ulinzi wa mipaka la Ulaya, Frontex, karibu na kisiwa cha Crete, kwa mujibu wa AFP ikinukuu walinzi wa pwani wa Ugiriki.

    Hata hivyo, taarifa hizi hazijathibitishwa mara moja na BBC.

  5. Ghana wameibiwa mali zao hotelini na wakachapwa 5-1 na Austria

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Timu ya taifa ya Ghana, Black Stars, imecheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Austria na kuchapwa mabao 5-1 lakini kabla ya mchezo huo wachezaji wawili wa timu hiyo, waliibiwa kwenye mji wa Vienna, Austria.

    Saa za Rolex na pesa taslimu $2,250 zilitoweka katika vyumba tofauti katika hoteli moja huko Vienna.

    Polisi wa Austria wanachunguza tukio hilo, na waziri wa michezo wa Ghana Kofi Adams amenukuliwa na vyombo vya habari vya ndani akisema CCTV haikuwa ikifanya kazi wakati huo.

    ‘‘Ripoti ya awali tuliyo nayo ni kwamba CCTV haikuwa ikifanya kazi, na polisi wanaangalia ni lini iliacha kufanya kazi na ni nani aliyehusika na mfumo wa ufuatiliaji wa hoteli wakati huo.’’ Adams alisema.

    Thamani ya saa hizo haijulikani wazi, lakini polisi wa Austria wanasema zina thamani ya ‘‘kiasi cha chini hadi cha kati cha euro elfu 10-50’’. Tukio hili limeripotiwa Vienna, jiji linalojulikana kwa ubora wa maisha.

    Ghana na Austria zote zilifuzu kwa Kombe la Dunia la FIFA mwezi Juni, lililoandaliwa na Marekani, Canada, na Mexico.

  6. Pakistan kuwa mwenyeji wa mazungumzo ya amani kati ya Saudi Arabia, Uturuki na Misri

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri wa mambo ya nje wa Pakistan Ishaq Dar anasema nchi hiyo itawapokea mawaziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia, Uturuki na Misri mjini Islamabad kuanzia tarehe 29-30 Machi.

    Watafanya "majadiliano ya kina", ikiwa ni pamoja na juhudi za "kupunguza mvutano katika eneo hilo", anaandika katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii X.

    Wizara ya mambo ya nje ya Misri sasa imetoa taarifa inayothibitisha kwamba waziri wake wa mambo ya nje amesafiri hadi mji mkuu wa Pakistan kwa mazungumzo hayo.

    Pakistan imekuwa ikifanya juhudi za kuchukua jukumu la upatanishi katika eneo hilo.

    Kando na hilo, imejitolea kuandaa mazungumzo kati ya Marekani na Iran – lakini bado hakuna uthibitisho wowote kama yatafanyika.

    Mapema wiki hii, Dar alisema "mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja" yanafanyika kupitia "ujumbe unaowasilishwa na Pakistan".

    Trump pia alichapisha picha ya chapisho la X kutoka kwa Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif mapema wiki hii, akichapisha kwenye Truth Social.

    Katika chapisho hilo, Sharif alisema Pakistan "iko tayari" kuandaa mazungumzo.

  7. Houthi yashambulia Israel kwa mara ya kwanza tangu vita ya Iran ianze

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran nchini Yemen wamesema wameishambulia Israel kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa vita kati ya Iran, Marekani na Israel, wakidai kurusha makombora ya balistiki kulenga maeneo nyeti ya kijeshi ya Israel.

    Kundi hilo limesema lilirusha makombora kadhaa yakilenga “maeneo nyeti ya kijeshi ya Israel” ikiwa ni sehemu ya kujibu mashambulizi yanayodaiwa kufanywa dhidi ya Iran pamoja na Lebanon, Iraq na maeneo ya Palestina.

    Houthi wameongeza kuwa mashambulizi yao yataendelea hadi kile walichokiita “uchokozi” dhidi ya pande zote utakapotamatika.

    Taarifa hiyo imekuja baada ya jeshi la Israel kusema limefanikiwa kuzuia kombora lililorushwa kutoka Yemen kuelekea Israel.

    Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema Marekani inatarajia kumaliza operesheni za kijeshi ndani ya wiki chache zijazo, huku mvutano ukiendelea kuongezeka katika eneo hilo.

  8. Huenda kombora la Marekani lilitumika katika shambulio lililosababisha vifo Iran - Wataalamu

    xcv

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wataalamu wa silaha wanasema huenda makombora ya kisasa ya Marekani yalitumika katika shambulio baya lililolenga eneo la makazi nchini Iran mwezi uliopita, kwa mujibu wa uchambuzi wa video za tukio hilo.

    Wataalamu hao walisema kuwa kifaa cha kurushwa kilichoonekana kwenye video ya shambulio dhidi ya majengo ya makazi katika mji wa kusini wa Lamerd kinafanana na kombora la Precision Strike Missile (PrSM).

    Silaha hiyo ni kombora jipya la masafa marefu linalotumiwa na jeshi la Marekani.

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Iran, watu wasiopungua 21 waliuawa katika mashambulizi mawili yaliyolenga mji huo siku hiyo, yakigonga majengo ya makazi pamoja na ukumbi wa michezo ulioko umbali wa takribani mita 300.

    Kamandi ya kijeshi ya Marekani inayosimamia operesheni za Mashariki ya Kati (Centcom) haijatoa maoni kuhusu tukio hilo.

    Unaweza pia kusoma:

  9. Meli ya kivita ya Marekani inaelekea katika eneo la mashariki ya kati

    xcv

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Meli ya kivita ya Marekani inayobeba ndege, USS George H. W. Bush, ambayo ni kama kambi ya anga inayosafiri baharini ikiwa na uwezo wa kubeba zaidi ya ndege 80, inatarajiwa kupelekwa katika eneo la Kamandi kuu ya jeshi la Marekani (CENTCOM) huko Mashariki ya Kati.

    Vyanzo kadhaa vimeliambia shirika la BBC kupitia mshirika wake wa Marekani, CBS News.

    Meli hiyo kubwa pamoja na kikosi chake cha mashambulizi ilikamilisha mafunzo ya maandalizi ya kupelekwa vitani mapema mwezi huu, na sasa inaweza kujiunga na operesheni za Marekani dhidi ya Iran, kwa mujibu wa maafisa wa Marekani walioliambia CBS.

    Wakati huo huo, manowari mbili za kivita zenye makombora ya kuongozwa, USS Donald Cook na USS Mason, pia zimeondoka Marekani wiki hii zikielekea kujiunga na operesheni hizo dhidi ya Iran.

    Nyingine, USS Ross, nayo imeondoka Marekani wiki hii, ingawa hadi sasa haijatajwa hadharani inaelekea wapi.

    Unaweza pia kusoma:

  10. Tiger Woods akamatwa kwa kuendesha gari akiwa amelewa, asababisha ajali

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mchezaji mashuhuri wa gofu Tiger Woods amekamatwa kwa tuhuma za kuendesha gari akiwa amelewa baada ya kupata ajali katika jimbo la Florida, mamlaka zimethibitisha. Polisi pia wamesema ameshtakiwa kwa kusababisha uharibifu wa mali na kukataa kufanya kipimo cha kisheria.

    Kwa mujibu wa Ofisi ya Sheriff ya Martin County, Woods mwenye umri wa miaka 50 alipindua gari lake aina ya Land Rover baada ya kugonga lori alipokuwa akijaribu kulipita kwa mwendo kasi katika eneo la Jupiter Island. Hakuna mtu aliyejeruhiwa katika ajali hiyo.

    Maafisa walisema hawakushuku uwepo wa pombe mwilini mwake, lakini walihisi huenda alikuwa chini ya ushawishi wa dutu isiyojulikana. Woods alifaulu kipimo cha pumzi (breathalyser) lakini alikataa kutoa sampuli ya mkojo kwa uchunguzi zaidi.

    Sheriff John Budensiek alisema uchunguzi wa awali ulionyesha dalili za ulevi, ingawa Woods alieleza kuwa ana historia ya majeraha na upasuaji ambayo yalizingatiwa wakati wa vipimo vilivyofanyika barabarani.

    Baada ya tukio hilo, Woods aliwekwa chini ya ulinzi wa polisi kwa muda kabla ya kuachiwa kwa dhamana. Mashtaka dhidi yake ni ya kiwango cha chini (misdemeanours), na mamlaka zimesema huenda isiwezekane kubaini kwa uhakika aina ya dutu iliyosababisha hali hiyo.

  11. Urusi na Iran zajadili uwezekano wa kumaliza vita kwa njia ya mazungumzo

    s

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mawaziri wa mambo ya nje wa Urusi na Iran wamejadili uwezekano wa kumaliza mzozo unaoendelea kwa njia ya kidiplomasia, huku wakisisitiza umuhimu wa suluhisho la kisiasa katika vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, alifanya mazungumzo na mwenzake wa Iran, Abbas Araqchi, kuhusu namna ya kuhamisha mzozo huo kutoka uwanja wa kijeshi kwenda kwenye mazungumzo ya kisiasa na kidiplomasia (Reuters).

    Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya mambo ya nje ya Urusi, mawaziri hao walijadili kwa kina hali ya kisiasa na kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati, wakieleza kuwa mgogoro huo umetokana na kile walichokiita uchokozi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Pia walibadilishana mawazo kuhusu uwezekano wa kufikia suluhisho la kudumu kwa kuzingatia sheria za kimataifa na maslahi ya nchi zote katika ukanda huo.

    Taarifa hiyo ilieleza pia kuwa Urusi imewasilisha misaada ya kibinadamu nchini Iran kama sehemu ya ushirikiano wao wa kimkakati unaojumuisha sekta za siasa, uchumi, kijeshi na nishati. Hata hivyo, makubaliano hayo hayajumuishi ulinzi wa pamoja kati ya nchi hizo mbili.

    Wakati huo huo, Mawaziri wa mambo ya nje wa Ulaya walitumia mkutano wa G7 kumueleza Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kuwa Urusi inashutumiwa kusaidia Iran kulenga majeshi ya Marekani katika vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati.

  12. Wanajeshi wa Marekani wajeruhiwa Saudi Arabia baada ya shambulio la Iran

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Angalau wanajeshi 12 wa Marekani wamejeruhiwa kufuatia shambulio lililolenga kambi ya anga ya Prince Sultan nchini Saudi Arabia, huku vita kati ya Iran na Marekani na Israel vikiingia mwezi wa pili.

    Idadi hiyo imeongezeka kutoka 10 iliyoripotiwa awali, kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Marekani.

    Vyombo vya habari vya Marekani vinaripoti kuwa wanajeshi hao walijeruhiwa katika shambulio la Iran lililohusisha angalau kombora moja pamoja na ndege zisizo na rubani (drones), kwa mujibu wa mshirika wa habari wa BBC, CBS.

    Inaelezwa kuwa angalau wanajeshi wawili wako katika hali mbaya sana baada ya jengo walilokuwemo ndani kulengwa moja kwa moja wakati wa shambulio hilo.

    Vyanzo visivyotajwa vimeeleza kuwa pia ndege kadhaa za kujaza mafuta angani ziliharibiwa katika tukio hilo.

    Hadi wakati wa kuripoti habari hii, Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) pamoja na Kamandi Kuu ya Marekani (US Central Command) hazikuwa zimetoa tamko rasmi kujibu taarifa hizo.

  13. Hujambo. Karibu katika habari zetu mubashara. Tarehe ni 28/03/2026.