Mazungumzo ya amani ya Marekani na Iran yamweka Netanyahu njia panda

Netanyahu alitembelea eneo la shambulio la Iran huko Dimona siku ya Jumapili.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Netanyahu alitembelea eneo la shambulio la Iran huko Dimona siku ya Jumapili.
Muda wa kusoma: Dakika 5

Kukiwa na ishara zinazochanganya kuhusu mipango ya Marekani ya kufanya mazungumzo mapya na Iran, mapigano ya kurushiana makombora kati ya Iran na Israel, maadui wakubwa wa Mashariki ya Kati yanaendelea.

Iran ilirusha makombora kadhaa kuelekea kaskazini na kusini mwa Israel usiku kucha, baada ya Israel kufanya mashambulizi ya anga "kadhaa" ndani ya Iran siku ya Jumatatu. Jeshi la Israel limesema mashambulizi hayo yalilenga vituo vya uongozi vya Kikosi cha kijeshi na Wizara ya Ujasusi mjini Tehran, pamoja na maghala ya silaha na mifumo ya ulinzi wa anga.

Katika eneo la mlipuko wa hivi karibuni kaskazini mwa Tel Aviv, roshani za majengo zimekatika, na kuta zinamwaga vipande vya zege kwenye shimo lililotokea katikati ya mkusanyiko wa majengo ya makazi.

Ripoti za eneo hilo zinaonesha kuwa hili lilikuwa ni pigo la moja kwa moja kutoka kwa kombora la Iran ambalo lilipishana kwa karibu sana na majengo kadhaa ya ghorofa. Watu sita wanaripotiwa kujeruhiwa katika shambulio hilo, ingawa hakuna aliyepata majeraha makubwa.

Mwanaume mmoja anayeishi katika barabara iliyo nyuma ya eneo la mlipuko aliiambia BBC kwamba hakupata muda wa kufika kwenye hifadhi wakati ving'ora vilipopigwa, na alikuwa amefika tu mlangoni kwake wakati wa mlipuko huo.

Alieleza jinsi alivyokimbia kutoka kwenye nyumba yake akiwa peku huku vioo vikivunjika kumzunguka. Alipogeuka kuangalia nyuma, moto ulikuwa tayari umeanza kuwaka kwenye vifusi vilivyokuwa nyuma yake, alisema.

Bado kuna uvumi mkubwa kuhusu sababu za Donald Trump kuanzisha mazungumzo mapya na Tehran; mazungumzo yamewahi kutumiwa na Ikulu ya Marekani hapo awali kama njia ya kuficha ukweli kuhusu kuongezeka kwa hatua za kijeshi, na kwa sasa maelfu ya wanamaji wa Marekani wanapelekwa Mashariki ya Kati.

Lakini kwa baadhi ya watu nchini Israel, mazungumzo hayo yanaonekana kama ishara nyingine kwamba rais wa Marekani anatafuta njia ya kujiondoa katika vita, na kwamba malengo ya Israel na mshirika wake mkuu yanaanza kutofautiana.

"Netanyahu hataki makubaliano," anasema Michael Milstein, aliyekuwa afisa wa zamani wa ujasusi wa kijeshi nchini Israel na sasa ni mkuu wa Kituo cha Masomo ya Palestina katika Chuo Kikuu cha Tel Aviv.

"Kuna aina fulani ya mgongano kati ya msimamo wa Trump na wa Netanyahu," aliiambia BBC.

"Netanyahu anataka kuendelea na vita. Aliahidi kwamba vita hivi vingemaliza kabisa vitisho vyote vinavyohatarisha uwepo wa Israel, na labda hata kusaidia kuleta mazingira ya kubadilisha utawala nchini Iran. Lakini kwa sasa kuna pengo kati ya ahadi zake na hali halisi inavyoendelea uwanjani."

Ikiwa Trump yuko makini kutafuta njia ya kumaliza vita hivi, anasema, waziri mkuu wa Israel anaweza kujikuta katika hali ngumu sana.

"Ni kama hali ya 'Catch-22' kwa sababu kama kutakuwa na mazungumzo, hatoweza kuendeleza vita, na hawezi kumwambia Donald Trump, 'nitaendelea na vita bila wewe.' Anaelewa kwamba atalazimika kukubali hali hiyo."

“Matokeo ya baada ya shambulio la kombora la Iran katika eneo la makazi huko Tel Aviv siku ya Jumanne.”

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, "Matokeo ya baada ya shambulio la kombora la Iran katika eneo la makazi huko Tel Aviv siku ya Jumanne."
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lakini Netanyahu anatembea kwenye mstari mwembamba, baada ya kuwaahidi Waisraeli kwamba vita hivi vitamaliza tishio la haraka kutoka Iran na mtandao wake wa washirika katika eneo lote. Kiwango cha makubaliano ambacho anaweza kuwasilisha kwa wapiga kura wa Israel na washirika wake kikiwa kinahitaji kuwa cha juu sana katika hatua hii ya vita.

"Waisraeli wanataka vita viishe. Tunachotambua tu ni kwamba njia sahihi ya kuimaliza ni sisi kuishinda serikali hiyo, na siyo kuruhusu jambo hili liturudie tena na tena," alisema Dan Illouz, mbunge mwingine wa chama cha Likud.

"Tumejaribu sera ya kudhibiti hapo awali, tulifanya hivyo na Hamas, na tuliona ilivyoturudia vibaya tarehe 7 Oktoba, hivyo hatutaki jambo hilo hilo litokee tena na Iran."

Baada ya kuzungumza na Rais Trump siku ya Jumatatu, Netanyahu alisema Israel inaendelea kushambulia Iran na Lebanon, na kwamba "italinda maslahi yake muhimu katika hali yoyote ile."

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, alisema Jumanne kwamba majeshi ya Israel yataanzisha eneo la usalama katika sehemu kubwa ya kusini mwa Lebanon, kusini mwa Mto Litani, na kwamba wakazi hawataruhusiwa kurejea huko hadi jamii za Israel zitakapokuwa salama dhidi ya mashambulizi ya Hezbollah, kundi linaloungwa mkono na Iran.

Inatarajiwa kwa kiasi kikubwa kwamba Israel itaendelea na kampeni yake ya kijeshi dhidi ya Hezbollah, hata kama makubaliano yatafikiwa ya kumaliza vita na Iran.

Lakini mchambuzi wa masuala ya Iran, Danny Citrinowicz, kutoka Taasisi ya Masomo ya Usalama wa Taifa mjini Tel Aviv, anasema makubaliano kuhusu Iran hayawezekani, kwa sababu tofauti za misimamo na matarajio kati ya pande husika ni kubwa mno kufikia makubaliano.

"Kwa upande wa Iran, wanaona kama wanashinda, si kushindwa, hivyo watadai fidia na dhamana," alisema. "Kwa upande mwingine, unaye Trump akifikiri kwamba Iran itakubali masharti yote ya Marekani tangu mwanzo."

Ili kufikia makubaliano, anasema, Trump na Netanyahu watalazimika ama kubadilisha utawala, au kuachana na baadhi ya masharti yao.

"Utawala huu hautasalimu amri, hawatawapa Wamarekani kitu ambacho hawakuwapa kabla ya vita," alisema. "Wanadhibiti sehemu muhimu ya uchumi wa kimataifa, Mlango wa Bahari wa Hormuz, mojawapo ya njia zenye shughuli nyingi zaidi za usafirishaji wa mafuta duniani, ambao Iran imeufunga, na wanahisi wana nguvu zaidi katika mazungumzo."

Kujiamini huko pia kumeongezwa na hatua ya Trump kuondoa onyo kali alilotoa wiki iliyopita kwa Iran kufungua tena Mlango wa Hormuz, vinginevyo wakabiliwe na mashambulizi makubwa dhidi ya miundombinu yake ya nishati."

Aliondoa tishio hilo baada ya Tehran kutishia kulipiza kisasi kwa kushambulia maeneo ya nishati yanayohusishwa na Marekani katika eneo hilo.

Wachambuzi wameeleza kuwa Donald Trump hana cha kupoteza kwa kuonekana kuashiria kuwa Marekani iko tayari kwa duru mpya ya mazungumzo, iwe ni kwa lengo la kutuliza masoko ya nishati, kuleta mgawanyiko ndani ya uongozi wa Iran, au kuchelewesha muda kwa ajili ya hatua mpya za kijeshi.

Mchambuzi mmoja aliniambia haitashangaza kama ataamka Ijumaa na kukuta Marekani imeanzisha mashambulizi mapya ya kijeshi dhidi ya Iran.

Vita hivi sasa vinaonekana kusimama kati ya kusalimu amri na kuongezeka kwa mapigano, huku hakuna upande ambao bado ni dhaifu vya kutosha kukubali matakwa ambayo adui yake anataka.