Papa asema hotuba ya 'madhalimu' haikuwa ikimlenga Trump

Chanzo cha picha, Getty Images
Papa Leo amesema hakutaka kujibizana na Donald Trump alipokosoa “madikteta” wanaotumia mabilioni ya dola kwenye vita katika hotuba aliyotoa mapema wiki hii.
Papa huyo amesema maneno yake yaliandikwa wiki mbili kabla, “kabla kabisa ya rais kutoa maoni yoyote kunihusu.”
Amesema haikuwa nia yake kuingia kwenye mjadala na rais huyo, jambo ambalo hapendezwi nalo.
Donald Trump hapo awali alimshambulia Papa huyo wa kwanza kutoka Marekani, akisema ni “mbaya kwa sera za nje,” hasa baada ya Papa kukosoa operesheni ya kijeshi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Papa huyo, ambaye yuko kwenye ziara barani Afrika, amesema kumekuwa na “simulizi isiyo sahihi” iliyojengwa kutokana na kauli za kisiasa za Trump.
Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance amesema anamshukuru Papa kwa ufafanuzi huo na akaongeza kuwa, ingawa mara nyingine kuna tofauti za maoni, hali halisi mara nyingi huwa ngumu zaidi kuliko inavyoonekana kwenye vyombo vya habari.
Awali, kabla ya hotuba ya Papa kuhusu “madikteta,” Vance alikuwa ameshauri Vatican ijikite zaidi kwenye masuala ya maadili.
Wakati wa hotuba yake nchini Cameroon siku ya Alhamisi, Papa aliwakosoa viongozi ambao "hupuuza ukweli kwamba mabilioni ya dola hutumika kwa mauaji na uharibifu, lakini rasilimali zinazohitajika kwa ajili ya uponyaji, elimu hazipatikani popote".
"Mabwana wa vita hujifanya hawajui kwamba inachukua muda mfupi tu kuharibu, lakini mara nyingi maisha yote hayatoshi kujenga upya," alisema.
Papa pia alilaani "mzunguko usio na mwisho wa uvunjifu wa utulivu na vifo" katika eneo "lenye damu" la Cameroon ambalo lilikuwa limekumbwa na uasi kwa karibu muongo mmoja.
Maneno hayo yalitafsiriwa na baadhi kama marejeleo ya Trump - ambaye baadaye aliwaambia waandishi wa habari: "Papa anaweza kusema anachotaka, na mimi nataka aseme anachotaka, lakini siwezi kukubaliana naye."
Unaweza kusoma;


