Kampuni kubwa za teknolojia zafunguliwa mashtaka ya vifo katika migodi ya kobalti

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Uchimbaji mdogo ni moja ya shughuli kubwa ya watu ya kiuchumi nchini DRC

Apple, Google, Tesla na Microsoft ni baadhi ya makampuni yaliyotajwa katika kesi ya madai ya fidia ya vifo na majeraha ya wachimbaji watoto wa migodi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,DRC.

Kesi hii ilifunguliwa na mawakili wa kimataifa wa haki za binadamu kwa niaba ya familia 14 DRC.

Wanayashutumu makampuni hayo kwa kujua kwamba madini aina ya kobalti yanayotumiwa katika bidhaa zao, yanatokana na ukiukwaji wa sheria kwa kuwaruhusu watoto wadogo kuchimba madini hayo.

DRC inazalisha asilimia 60 ya Kobalti inayosambazwa duniani kote.

Madini hayo yanatumiwa kutengenezea betri aina ya lithium-ion zinazotumika kuwasha magari ya umeme, komputa mpakato na simu janja.

Lakini, hatua za uchimbaji zimekuwa zikizua wasiwasi kuhusu uchimbaji haramu, ukiukwaji wa haki za binadamu na ufisadi.

Kesi hii iliyofunguliwa nchini Marekani inadai kuwa kampuni hizo za teknolojia walikuwa na ''uelewa wa kutosha'' kuwa kobalti inayotumika katika bidhaa zao inaweza kuhusishwa na kufanyishwa kazi kwa watoto kinyume cha sheria.

Wanasema makampuni hayo yameshindwa kudhibiti mifumo ya usambazaji wa bidhaa zao na badala yake kufaidika kutoka kwa utumikishwaji wa watoto hao.

Chanzo cha picha, AFP/Getty

Maelezo ya picha, DRC inazalisha asilimia 60 ya Kobalti inayosambazwa duniani kote

Makampuni mengine yaliyotajwa katika kesi hiyo ni pamoja na kampuni ya kutengeneza kompyuta mpakato Dell na kampuni mbili za uchimba madini za Zheijang Huayou Cobalt na Glencore, ambao wanamiliki migodi ambayo kwa mujibu wa familia za waathirika wanasema ndipo watoto hao walipokuwa wanafanyia kazi.

Glencore iliiambia gazeti la Telegraph nchini Uingereza kuwa ''hainunui, kusindika wala kufanya biashara yoyote ya madini yaliyochimbwa na wachimbaji wadogo,'' na haiungi mkono utumikishwaji wowote wa watoto, uwe wa kulazimishwa au hata ule wa kujitolea.''

BBC imejaribu kuwasiliana na kampuni ya Zhejiang Huayou Cobalt.

Kwa mujibu wa taarifa za mahakamani amabazo gazeti la Guardian la Uingereza limetoa mifano kadhaa ya wachimbaji watoto ambao walizikwa wakiwa hai na wengine kuumizwa vibaya baada ya mabomba kuanguka.

Familia hizo 14 zinataka makampuni hayo yawalipe kwa watoto zao kufanyishwa kazi kwa nguvu, kuumizwa kihisia na kutokuwa na usimamizi makini.

Katika majibu yao kwa habari ya Telegraph, Microsoft wamesema kuwa wao wamejikita katika kununua madini ambayo wanafanya uchunguzi wa kutosha wa kule yalipotokea na kama kuna ukiukwaji wa taratibu na sheria huchukua hatua.

BBC pia imetafuta maoni kutoka Google, Apple, Dell na Tesla.