Tetesi za soka Ulaya: Al-Ittihad warejea kwa Mo Salah
Chanzo cha picha, Getty Images
Al-Ittihad walikataliwa ofa yao ya £150m kwa ajili ya mshambuliaji wa Liverpool Mohamed Salah mwaka 2023, lakini klabu hiyo ya Saudi Pro League imefufua nia yao upya ya kumsajili nyota huyo wa Misri mwenye umri wa miaka 33, ambaye atapatikana bure baada ya kuondoka Liverpool mwishoni mwa msimu huu wa kiangazi (ESPN).
Salah hakupata ofa kutoka klabu zingine kama ilivyotarajia katika dirisha la Januari, na katika mazungumzo ya kuondoka msimu huu, wamiliki wa Liverpool Fenway Sports Group waliona kuendelea kung'ang'ania ili kupata ada kungeongeza mzozo (Telegraph).
Liverpool wamekuwa wakiwasiliana mara kwa mara na kocha wa zamani wa Real Madrid, Xabi Alonso, ambaye aliwahi kushinda ligi ya mabingwa akiwa mchezaji wa klabu hiyo, na Mhispania huyo yuko tayari kuchukua nafasi ya Arne Slot msimu huu iwapo masharti fulani yatatimizwa (Bild).
Liverpool wamehusishwa na winga wa Ufaransa Michael Olise kama mrithi wa Salah, lakini Bayern Munich hawana haraka kuhusu mustakabali wa mchezaji huyo mwenye miaka 24 kwani ana mkataba hadi 2029 na hana kipengele cha kuuzwa (Sport Bild).
Chanzo cha picha, Getty Images
Manchester United wanawafuatilia winga wa RB Leipzig raia wa Ivory Coast Yan Diomande (19), beki wa Newcastle United na England Lewis Hall (21), pamoja na mshambuliaji wa Everton na Senegal Iliman Ndiaye (26), wanapojiandaa kurejea kwenye mashindano ya Ulaya (Sky Sports).
Kiungo wa Manchester United kutoka Brazil Casemiro, ambaye ataondoka klabuni hapo msimu huu, alikubaliana Januari kuondoa kipengele kwenye mkataba wake ambacho kingeongeza mwaka mmoja iwapo angeanza mechi 35 msimu huu (Manchester Evening News).
Manchester United wana uhakika wanaweza kumuuza kwenda klabu nyingine mshambuliaji wa England Marcus Rashford, 28, iwapo Barcelona hawatafanya uhamisho wake wa mkopo kuwa wa kudumu kwa £26m (ESPN).
Chanzo cha picha, Getty Images
Barcelona wanamtaka beki wa Inter Milan Alessandro Bastoni, lakini wanaweza kukutana na ushindani kutoka Liverpool katika mbio za kumsajili mchezaji huyo mwenye miaka 26 (Football Italia).
Kocha wa Newcastle United Eddie Howe anaendelea kuungwa mkono na klabu licha ya baadhi ya mashabiki kutoridhika na matokeo kufuatia kutolewa kwenye ligi ya mabingwa dhidi ya Barcelona na kipigo kutoka kwa Sunderland (Times).
Winga wa Brazil Vinicius Jr amesema anafikiria kubaki Real Madrid kwa "muda mrefu", huku mchezaji huyo wa miaka 25 akitarajiwa kusaini mkataba mpya (Sport).
Kiungo wa Chelsea Moises Caicedo, 24, amesema hana mpango wa kuondoka klabuni humo licha ya kuhusishwa na Real Madrid (El Chiringuito TV, via Standard).
Juventus wako karibu kufikia makubaliano ya mkataba mpya na mshambuliaji wa Serbia Dusan Vlahovic, 26, ambaye mkataba wake wa sasa unaisha mwishoni mwa msimu huu (Gazzetta dello Sport).
Habari kuu
Gumzo mitandaoni
Zinazovuma zaidi
Haipatikani tena