Kwa nini ni vigumu kwa Marekani kuchukua madini ya urani ya Iran?
Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Daniel Bush
- Nafasi, Washington correspondent
- Author, Bernd Debusmann Jr
- Nafasi, White House reporter
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Wazo la wanajeshi wa Marekani kuvamia kituo cha siri cha nyuklia kilicho chini ya ardhi ili kutwaa akiba ya urani iliyoboreshwa ya Iran linaweza kuonekana kama hadithi ya kubuni, lakini inaripotiwa kuwa ni miongoni mwa chaguo anazozingatia Rais Donald Trump ili kufikia lengo kuu la vita: kuzuia Iran kutengeneza silaha za nyuklia.
Kwa mujibu wa wataalamu wa kijeshi na maafisa wa zamani wa ulinzi wa Marekani waliozungumza na BBC, operesheni kama hiyo ingekuwa ngumu sana na yenye hatari kubwa. Ingehitaji kutumwa kwa wanajeshi wa ardhini na inaweza kuchukua siku kadhaa au hata wiki kukamilika.
Kuitoa akiba ya urani kungekuwa moja ya "operesheni ngumu zaidi za kijeshi katika historia," alisema Mick Mulroy, afisa wa zamani wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani.
Hii ni moja tu ya hatua kadhaa za kijeshi ambazo Trump anaweza kuchukua dhidi ya Iran. Nyingine ni pamoja na kudhibiti Kisiwa cha Kharg ili kuishinikiza Iran kufungua kikamilifu mlango bahari wa Hormuz, au kutumia vitisho vya kijeshi kulazimisha mazungumzo.
Hata hivyo, alionekana kupunguza uzito wa akiba hiyo, akirejea uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel mwezi Juni mwaka uliopita.
"Imezikwa kwa kina kirefu sana, itakuwa vigumu sana kwa yeyote kuifikia," alisema Trump. "Iko chini kabisa. Kwa hiyo… iko salama kwa kiasi fulani. Lakini, unajua, tutafanya uamuzi."
Matamshi yake yalikuja baada ya Jarida la Wall Street kuripoti kuwa Marekani ilikuwa inazingatia operesheni ya kuchimba nyenzo hizo. Ikulu ya White House ilisema Trump bado hajafanya uamuzi wa mwisho.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Operesheni ya kulenga akiba ya urani ya Iran ingekabiliwa na changamoto kadhaa kubwa za kiutendaji na kiusafirishaji, kwa mujibu wa wataalamu.
Kwa mujibu wa maafisa waandamizi wa Marekani, mwanzoni mwa vita Iran ilikuwa na takriban kilo 440 za urani iliyoboreshwa kwa kiwango cha asilimia 60—kiwango ambacho kinaweza kufikishwa kwa haraka hadi asilimia 90, kinachohitajika kwa utengenezaji wa silaha za nyuklia.
Aidha, Iran ina takriban kilo 1,000 za urani iliyoboreshwa kwa asilimia 20, pamoja na kilo 8,500 zilizo katika kiwango cha asilimia 3.6, ambacho hutumika kwa shughuli za utafiti wa kitabibu.
Inaaminika kuwa sehemu kubwa ya urani yenye kiwango cha juu cha urutubishaji ambayo inaweza kubadilishwa kwa urahisi kuwa malighafi ya mabomu au makombora imehifadhiwa katika kituo cha Isfahan.
Kituo hicho ni miongoni mwa maeneo matatu ya nyuklia yaliyo chini ya ardhi nchini Iran ambayo yalilengwa katika mashambulizi ya anga ya pamoja ya Marekani na Israel mwaka uliopita.
Hata hivyo, bado haijulikani ni kiasi gani cha urani hiyo kimehifadhiwa katika maeneo mengine.
Kwa mujibu wa Jason Campbell, afisa wa zamani mwandamizi wa ulinzi wa Marekani katika tawala za Obama na Trump, operesheni ya kijeshi ya kurejesha urani hiyo ingekuwa rahisi zaidi ikiwa Marekani ingekuwa na taarifa sahihi kuhusu mahali ilipo.
"Hali bora ni pale unapojua mahali ilipo kwa uhakika," alisema Campbell. "Ikiwa imegawanywa katika maeneo manne tofauti, basi unazungumzia kiwango tofauti kabisa cha ugumu."
Mbali na Isfahan, inaaminika kuwa sehemu ya urani yenye kiwango cha juu cha uboreshaji pia imehifadhiwa katika vituo vya Fordo na Natanz ambavyo ni miongoni mwa vituo viwili vingine vya uboreshaji vilivyolengwa katika operesheni ya Operation Midnight Hammer mwaka uliopita.
Mkurugenzi wa mamlaka ya kitaifa ya nishati za atomiki, Rafael Grossi, alisema mwezi uliopita kuwa sehemu kubwa ya urani hiyo imehifadhiwa Isfahan, huku kiasi kingine kikiwa Natanz. Hata hivyo, alibainisha kuwa taarifa za kina zaidi hazipatikani kwa sasa, kwani wakaguzi hawajarejea katika maeneo hayo tangu walipoondolewa nchini Iran kufuatia mashambulizi ya anga ya pamoja ya Marekani na Israel mwaka 2025.
"Kuna maswali mengi ambayo tutaweza kuyafafanua tu pale tutakapopata fursa ya kurejea huko," alisema Grossi alipokuwa akizungumza na wanahabari.
Kupata ufikiaji wa urani hiyo yenye uboreshaji wa juu ni changamoto nyingine kubwa, hata kama Marekani itakuwa na taarifa sahihi ya mahali ilipo.
Kuna dalili kwamba Iran iliimarisha ulinzi wa miundombinu ya chini ya ardhi karibu na moja ya vituo vyake vya nyuklia kabla ya mashambulizi ya mwaka huu ya Marekani na Israel. Kwa mfano, picha za satelaiti za mwezi Februari zinaonyesha kuwa milango yote ya kuingia katika mtandao wa handaki wa Isfahan ilionekana kufunikwa kwa udongo, jambo linaloweza kufanya operesheni yoyote kuwa ngumu zaidi.
Tangu kuanza kwa vita, Marekani na Israel zimeweza kutumia mashambulizi ya anga pekee kudhoofisha jeshi la majini la Iran, kupunguza uwezo wake wa makombora ya masafa marefu na kuharibu miundombinu yake ya viwanda. Hata hivyo, tofauti na malengo hayo mengine ya kijeshi, wataalamu wanasema kuwa kulinda na kudhibiti urani iliyoboreshwa ya Iran hakuwezi kufanyika bila kutumia vikosi vya ardhini.
Inawezekana Marekani ikatumia baadhi ya vikosi vya 82nd Airborne Division, ambavyo tayari vimepelekwa Mashariki ya Kati kulinda maeneo yanayozunguka Isfahan na Natanz.
Baadaye, vikosi maalum vilivyofundishwa kushughulikia nyenzo za nyuklia vingetumwa kuichukua urani hiyo. Urani yenyewe ipo katika hali ya gesi na inaaminika kuhifadhiwa ndani ya mitungi mikubwa ya chuma.
Picha za satelaiti zinaonyesha kuwa milango ya kuingia katika vituo vya Isfahan na Natanz iliharibiwa vibaya na mashambulizi ya anga ya Marekani.
Hivyo, vikosi vya Marekani vingehitaji kutumia mitambo mizito kuchimba kifusi ili kufikia urani hiyo, ambayo inaaminika kuhifadhiwa ndani ya handaki zilizozikwa kwa kina kikubwa chini ya ardhi huku vikikabiliwa na hatari ya mashambulizi ya kulipiza kisasi kutoka Iran.
"Kwanza lazima uchimbe eneo husika na kubaini ilipo [urani], huku ukiwa katika hatari ya mara kwa mara ya kushambuliwa," alisema Jason Campbell.
Bado ni swali lisilo na jibu la wazi jinsi Iran inaweza kujibu, au kiwango gani cha tishio inaweza kuleta kwa vikosi vya ardhini vya Marekani vitakavyolenga vituo vikuu vya nyuklia vya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa Alex Plitsas, afisa wa zamani wa ulinzi wa Marekani na mtafiti mwandamizi katika mpango wa usalama wa Mashariki ya Kati, Marekani na Israel zimekuwa zikidhoofisha "uwezo wa ulinzi wa Iran ili kuwezesha aina hii ya operesheni iwapo itahitajika." Hata hivyo, alisisitiza kuwa bado itakuwa operesheni "yenye hatari kubwa."
Vikosi vya ardhini vya Marekani vingejikuta vimetengwa katika eneo la Isfahan, lililoko takriban maili 300 (kilomita 482) ndani ya nchi kutoka mji wa tatu kwa ukubwa nchini Iran. "Hali hii inafanya uokoaji wa kitabibu kuwa mgumu kutokana na umbali. Pia inawaweka wanajeshi katika hatari ya mashambulizi ya anga wanapoingia na kutoka, pamoja na kushambuliwa wakiwa kwenye kituo cha nyuklia," alieleza Plitsas.
Ingawa operesheni inaweza kuchukua sura mbalimbali, wataalamu wanasema huenda ikahusisha kuteka uwanja wa ndege au eneo la kutua ili vikosi vya Marekani viweze kuendesha shughuli zao, kisha kuondoa urani iliyoboreshwa kutoka Iran baada ya kuipata.
Kwa mujibu wa wataalamu wa kijeshi, 82nd Airborne Division, ambacho kina utaalamu wa kulinda viwanja vya ndege na miundombinu kinaweza kutumika pamoja na vikosi vingine kuanzisha kituo cha operesheni. Baada ya kudhibiti urani hiyo, Marekani itakabiliwa na uamuzi wa kuihamisha nje ya nchi au kuipunguza nguvu yake hapo hapo.
Maafisa waandamizi wa serikali walisema mwanzoni mwa vita kuwa Marekani inaweza kuzingatia kupunguza nguvu ya urani hiyo ndani ya Iran badala ya kuiondoa. Hata hivyo, kwa mujibu wa Jonathan Ruhe, mtaalamu wa mpango wa nyuklia wa Iran, hatua hiyo itakuwa kubwa, tata na ya kuchukua muda mrefu.
Aliongeza kuwa kuiteka na kuiondoa urani hiyo nje ya Iran ni njia ya haraka zaidi, na ingeiruhusu Marekani kuishughulikia ndani ya mipaka yake. Hata hivyo, alisisitiza kuwa operesheni hiyo itabaki kuwa hatari kubwa bila kujali itatekelezwa kwa njia gani.
"Kimsingi unazungumzia karibu nusu tani ya urani ya kiwango cha silaha ambayo lazima uiondoe," alisema Ruhe.
"Na ukweli ni kwamba kuna mambo milioni yanaweza kwenda mrama."
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid
Habari kuu
Gumzo mitandaoni
Zinazovuma zaidi
Haipatikani tena