Maswali muhimu kuhusu ripoti ya Oktoba 29 yanayohitaji majibu
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Ripoti ya tume iliyoundwa kuchunguza matukio ya vurugu yaliyotokea Oktoba 29, 2025 wakati na baada ya uchaguzi mkuu nchini Tanzania, imewasilishwa rasmi, ikiweka hadharani maelezo kuhusu vifo, majeruhi na muktadha wa matukio hayo.
Zaidi ya watu 500 walipoteza maisha na maelfu kujeruhiwa katika ghasia hizo ambazo pia zimesababisha uharibifu wa mali zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 125 za Tanzania, takribani dola milioni 50.
Hata hivyo, kama ilivyo kwa ripoti nyingi za kitaifa zenye uzito mkubwa, uwasilishaji wake umefungua mjadala mpya hasa kuhusu uwazi, uwajibikaji na hatua zinazofuata.
Mwenyekiti wa tume, Jaji Othman Chande, alieleza kuwa uchunguzi uliofanywa ulilenga kukusanya ushahidi, kusikiliza pande mbalimbali na kutoa mapendekezo. Kwa upande wake, Rais Samia Suluhu Hassan alisisitiza kuwa hii ni "ripoti ya rais," akiahidi kuwa serikali itachukua hatua zaidi kufuatia mapendekezo yaliyotolewa.
Katika mazingira hayo, maswali kadhaa muhimu yanaendelea kujitokeza miongoni mwa wananchi na wadau yakilenga si tu kuelewa kilichotokea Oktoba 29, bali pia kuhakikisha haki, uwajibikaji na kuzuia matukio kama hayo siku zijazo.
1. Wahusika wakuu na waratibu wa ghasia ni kina nani?
Moja ya maswali makubwa ni kuhusu utambulisho wa wahusika waliopanga, kuratibu na kufadhili ghasia.
Akizungumzia suala hilo, Jaji Chande alisema: "Matukio yalipangwa, yaliratibiwa na yalifadhiliwa na yalitekelezwa na watu waliopata mafunzo." Kauli hiyo inaibua swali la msingi, ni kina nani hasa waliofanya hivyo, na kwa nini hawajatajwa wazi kwa majina?
Ripoti pia inaeleza kuwa baadhi ya washiriki walipewa mafunzo na kulipwa kati ya shilingi 10,000 hadi 50,000 za kitanzania kama kati ya dola 3.5 hadi 20) kushiriki vurugu, lakini haijaweka wazi nani waliandaa mafunzo hayo wala namna malipo yalivyofanyika.
Badala yake, ripoti imetaja kwa ujumla vyama vya siasa na wanaharakati, bila kutaja majina ya watu binafsi au taasisi husika.
Hata hivyo kwenye eneo hili, tume ilieleza kuwa haina mamlaka ya kijinai:
"Tume hii siyo ya kijinai… huwezi kumtuhumu mtu bila kumpa fursa ya kujibu dai", anasema Chande.
Kutokana na hilo, tume ikapendekeza kuundwa kwa chombo cha uchunguzi wa kijinai ili kubaini wahusika wakuu pendekezo ambalo Rais ameonekana kuliunga mkono.
2. Je, waathirika wote watapata fidia?
Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa mujibu wa ripoti, watu 518 walipoteza maisha wakiwemo watoto 21, pamoja na majeruhi 2,390 waliopata madhara ya viwango tofauti. Aidha, askari wa vyombo vya ulinzi na usalama 16 walipoteza maisha huku wengine 120 wakijeruhiwa.
Katika ripoti ya tume, imependekeza majeruhi kupatiwa matibabu na msaada kama viungo bandia, jambo lililopokelewa vyema. Hata hivyo, kuna sintofahamu kuhusu fidia kwa waliopoteza maisha, mali zao ikiwemo nyumba, biashara na mali nyingine za binafsi.
Kwa mujibu wa ripoti, mali zenye thamani ya shilingi bilioni 125 (takribani dola milioni 50) ziliharibiwa katika ghasia hizo. Kati ya hizo, shilingi bilioni 89 (takribani dola milioni 36) ni mali za sekta binafsi, zikiwemo vituo vya mafuta, mali za CCM na taasisi za kifedha.
Hadi sasa, hakuna maelezo ya kina kuhusu nani atalipwa fidia, vigezo vitakavyotumika, na taasisi itakayosimamia mchakato huo.
Pia kuna familia za waliopoteza wapendwa wao au ambao bado hawajapatikana, jambo linaloongeza uzito wa swali la haki.
Katika hatua ya sasa kwenye hili Rais Samia alisema: "Serikali itaendelea kufanya uchunguzi wa kina na wa kitaalam, ili tujue mambo haya kwa usahihi."
3. Uwajibikaji uko wapi?
Chanzo cha picha, Getty Images
Swali la nani atawajibika kwa vifo vilivyotokea, vikiwemo vya kupigwa na risasi, majeruhi na uharibifu linaendelea kuwa zito.
Wiki chache baada ya ghasia hizo, BBC ilithibitisha video za baadhi ya watu wakishambuliwa kwa risasi katika maeneo mbalimbali.
Hata hivyo ripoti imeeleza kuwa tume haina mamlaka ya kuchukua hatua za kijinai, jukumu hilo liko kwa vyombo vya dola kama polisi.
Mwenyekiti wa tume Jaji Chande alisema: "Yapo maeneo yenye viashiria vya jinai… tunapendekeza kuundwa kwa tume ya uchunguzi wa kijinai." Kwa mujibu wake tume hii ndiyo itaweza kuchunguza matukio mahususi ya kijinai ili kupata majibu.
Hii ina maana kuwa uwajibikaji bado sio wa hivi karibiuni ni uko mbele, na ambao utategemea uchunguzi zaidi. Muda gani? Haijajulikana ingawa Rais anasema Serikali itachukua hatua.
Changamoto inayoweza kujitokeza ni kwamba baadhi ya washukiwa waliwahi kukamatwa na baadaye kusamehewa, hali inayozua swali kama hatua mpya zitachukuliwa endapo watahusishwa tena.
Wachambuzi pia wanaelekeza mjadala kwa taasisi, hasa vyombo vya usalama, wakijiuliza kama vilichukua hatua stahiki licha ya dalili za mapema za vurugu kuonekana.
4. Je, matukio haya yangeweza kuzuiliwa?
Chanzo cha picha, Getty Images
Ripoti inaonyesha kuwa kulikuwa na dalili za vurugu miezi kadhaa kabla ya Oktoba 29, 2025. Ilifahamika na Mamlaka, na hata kauli zilianza kutolewa na viongozi mbalimbali kutishia kuhusu watakaoandamana ama walioitisha maandamano ambayo sasa tuyme imesema hayakuwa maandamano bali ghasia.
Mchambuzi wa siasa Nicodemus Minde anasema: "Kilichotokea ni matokeo ya mkusanyiko wa changamoto za muda mrefu."
Anasisitiza umuhimu wa majadiliano ya kitaifa, akigusia hoja kama Katiba mpya, masuala ya demokrasia, mifumo ya uchaguzi na utengamano wa kijamii.
Ripoti pia inaeleza kuwa baadhi ya wanasiasa na wanaharakati walitumia changamoto za wananchi kuwachochea kushiriki vurugu kwa kutumia kauli mbiu mbalimbali.
Hivyo, swali linabaki kwa nini hatua za mapema iwe za kisiasa au kiusalama hazikuchukuliwa kuzuia ghasia zisitokee?
5. Masuala ya mtandao na ushahidi wa kidijitali
Chanzo cha picha, Getty Images
Kulikuwa na ukosefu wa huduma ya mtandao (internet) kwa takribani siku tano baada ya vurugu kuanza lakini suala hili halikugusiwa wazi katika uwasilishaji wa ripoti.
Hii inaibua maswali mapya, hasa ikizingatiwa kuwa: Tume ilitumia uchambuzi wa picha na video za mitandaoni. Haijaeleza wataalamu waliotumika ni kina nani na kutoka wapi?
Zaidi ya hayo, baadhi ya washiriki walidai kupewa simu maalum za kurekodi na kusambaza maudhui ya kuchochea hasira. Swali linalobaki ni je, walifanya hivyo lini wakati mtandao ulikuwa haupatikani?
Kwa ujumla, ripoti ya Oktoba 29 imeweka msingi muhimu wa kuelewa matukio hayo, lakini pia imeibua maswali mapya kadhaa
Mchambuzi wa kimataifa Salim Amin anasema: "Kilichotolewa ni muhtasari tu… ripoti kamili inaweza kuwa na majibu zaidi."
Kwa mujibu wa Jaji Chande, tume itaendelea kutoa ufafanuzi zaidi kupitia majadiliano na wadau.
Hata hivyo, kwa wananchi wengi, hatua zinazofuata, hasa utekelezaji wa mapendekezo ndizo zitakazoamua kama ripoti hii italeta suluhisho au itaacha maswali mengi zaidi kuliko majibu.
Habari kuu
Gumzo mitandaoni
Zinazovuma zaidi
Haipatikani tena